Hadithi hadithi…..Katika maisha kuna mambo mtu unaweza uafanya yakakufedhehesha ukawa kila ukikumbuka maisha yako yote unasononeka au unaishia kucheka ukikumbuka akili zako za kitoto. Kuna jambo liliwahi kunikuta wakati niko darasa la sita lilinitesa sana maana nilitaniwa sana shuleni, nilitaniwa mpaka nikawa naogopa kwenda shule. Lakini miaka ikapita nikasahau, japo mara moja moja likija kichwani huwa nacheka tu kimoyo moyo. Nilikuwa nimeshasahau kabisa jambo hilo mpaka juzi nikiwa kwenye daladala nikamuona mama mmoja akiingia amebeba sinia lina mihogo anaenda kuuza, akili ikanambia kuwa namfahamu lakini nikawa sikumbuki wapi nimemuona, alipotaka kushuka namni nikaona nishukie palepale ili anikumbushe tumeonana wapi. Tuliposhuka, nikamgusa nikasema ‘Samahani mama’, akageuka, kuniona tu akapiga ukulele wa furaha na kunitaja jina langu, mimi nikawa bado gizani, nikamwambia ‘ Najua nakufahamu naomba unikumbushe’. Akanambia ‘Mie Zinduna, tulikuwa wote shule’. Dah kumbukumbu zikanirudia palepale nikakumbuka kuwa huyu ndie aliyeniletea wakati mgumu sana shule. Kisa kizima kilikuwa hivi, mimi na huyu Zinduna tulikuwa darasa moja, nilikuwa nampenda sana, jina lake nikajiandika mpaka kwenye kiganja, usiku nilikuwa namuota, kifupi niliamua kuwa lazima nije nimuoe Zinduna. Nilianza kujipendekeza kwa Zinduna, nikawa namletea mahindi ya kuchoma, karanga, siku nyingine namnunulia biskuti, alikuwa anapokea zawadi zangu lakini ilikuwa ni wazi ananidharau, yaani aligeuka ndio sababu ya mimi kuwahi shuleni, kufua nguo na kuwa msafi hata kujitahidi darasani. Sasa siku moja nikaona heri nimwambie wazi kuwa nampenda maana pamoja na zawadi nyingi nilizokuwa nampa Zinduna alikuwa hanijali kabisa, alikuwa mara nyingi anaongea zaidi na monita wa darasa letu Hamisi. Basi nikaamua kumuandikia barua, Mpenzi wa moyo Zinduna, usiku silali kwa kukuwaza wewe, mchana sili kwa mapenzi yaliyo mengi kama nyota za mbingu. Naomba uwe mpenzi wangu tukimaliza shule nikuoe. Na maneno mengine mengi ya namna hiyo. Nikaweza kumpa Zinduna barua hiyo. Zinduna akaipeleka barua ile kwa mwalimu mkuu. Kwanza ikasomwa mbele ya shule nzima pili nikachapwa viboko halafu ndio ukaanza utani. Nilikuja kumchukia sana Zinduna, sasa juzi nimemuona anauza mihogo nikanunua sinia lote nikaanza kugawa, wakati nikimuona machoni ananiangalia kama vile sasa ananipenda yeye, hakika nilipomrudishia sinia lake akaanza kunihoji ninaishi wapi Je nimeoa, na kunambia kuwa miaka yote alikuwa ananikumbuka sana na pia kuwa hajaolewa. NIkamuaga na kusepa
Categories: Daily Kiswahili Joke