LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO 1



Baba yangu alikuwa akifundisha Iringa Middle School kati ya mwaka 1958 na 1962, shule hiyo iliyokuwa imejengwa eneo lililoitwa Mshindo hatimae ilikuja kuitwa Mshindo Primary school mwishoni mwa miaka ya 60. Kwa akili fulani ya viongozi wa mji wa Iringa, waliamua kuvunja shule hiyo na kujenga uwanja wa michezo wa Samora  Stadium.
Iringa Middle School ilikuwa shule iliyofuata baada ya mwanafunzi kumaliza Government Primary School, shule ambayo sasa inaitwa Shule ya Msingi ya Mlandege. Shule ya  Goverment iliishia darasa la nne, na Middle School ilianza darasa la tano hadi la nane
Nakumbuka kuanza shule Mlandege darasa la kwanza, ambapo madarasa yalikuwa mawili 1A, na 1B. Nilikuwa 1B mwalimu wetu alikuwa Mwalimu Chitigo, mzee mmoja ambaye alikuwa akitukumbusha kila mara kuwa alitoka Tanga, Tanga  miaka hiyo ulikuwa mmoja wa miji maarufu Afrika ya Mashariki. Mwalimu Chitigo alitufundisha kila kitu, kusoma kuandika , hesabu, kuimba na michezo. Mwalimu Chitigo alikuwa anahifadhi kiboko chake juu ya kabati lililokuwa darasani, mwenyewe alikiita kiboko chake, ‘mzee kamwene’. Tulijitahidi sana kuiba kiboko kile lakini tulikuwa wafupi hatukuweza kufika juu ya kabati. Miaka mingi baadae nilikuja kufundisha shule ya Mlandege nilishangaa sana jinsi kabati lile lilivyokuwa fupi, ina maana tulikuwa wafupi sana sana.  Darasa la 1A walikuwa wanafundishwa na Mwalimu Kalinga, mama huyu alikuwa rafiki wa mama yangu, namkumbuka sana.
Mlango wa kwanza kulia ni darasa 1A, mlango wa pili ni 1B
Mwalimu Mkuu alikuwa mwalimu George Nyakunga, ambaye bahati mbaya alifariki mapema miaka hiyo hiyo. Namkumbuka Mwalimu George, alikuwa mweupe sana na alikuwa anachana nywele kwa staili ya kuweka ‘way’. Kwa kuwa alikuwa rafiki wa baba yangu nilimfahamu kabla sijaanza shule. Yunifom za shule zilikuwa zinashonwa na fundi maalumu hivyo wazazi walilipa shilingi moja na senti hamsini (ilitwa shilingi mojaunusu) na siku ya kupewa yunifom mpya tulipanga mstari na Mwalimu George aliita majina na kutugawia nguo zetu. Kaptura 2 na shati 2 ambazo hazina vifungo zimekaa kama tshirt lakini zilishonwa kwa kitambaa cha jinja nyeupe, kitambaa hicho baadae kilikuwa maarufu kwa kutumika kama sanda. Kati ya watu maarufu ninao wakumbuka wakati huo ni David Mwaibula na Karama Masudi ambaye kwa sasa yuko Tabora, huyu Karama namkumbuka kwa kuwa alikuwa golikipa wa shule na siku moja aliumia vidole wakati wa kudaka ana akapelekwa hospitali. Sitasahau mkasa uliotokea wakati huo ambapo ilizuka hadithi kuwa kwenye choo kimoja cha wasichana kuna jini, ambalo wasichana wakienda kujisaidia linawavuta chupi. Hii ilikuwa shida kubwa kwani ili ufike choo cha wavulana ilikuwa lazima upite jirani na choo cha wasichana. Watu wengi waliamua kukojoa darasani kuliko kupambana na jini njiani. Hadithi ya jini ilipotea baada ya Mwalimu George kutuita wote na kutuambia kuwa walichinja mbuzi chooni hivyo jini limeondoka. Nadhani ilikuwa hadithi ya kuondoa hofu tu.
Mbele ni choo kilichodaiwa kuwa na jini, nyuma choo cha wavulana
Nilipofika darasa la tatu, nikahamia kwa babu yangu Mzee Raphael Kitime aliyekuwa anaishi Barabara mbili Makorongoni, nyumba tuliyokuwa tukiishi ni nyumba ambayo sasa ni kilabu maarufu cha pombe za kiasili cha Barabara mbili, na pia darasa la tatu likanikuta nimehamia shule ya misheni iliyoitwa wakati huo Consolata Primary School, siku hizi inaitwa Shule ya Msingi Chemchem, kwa kuwa kulikuwa na chemchem maeneo ya shule hiyo.
Mtaa wa Barabara mbili
Hapo nikakutana na waalimu kama mwalimu Daudi Luhanga, mwalimu aliyeogopwa na wanafunzi wa mji wote, na pia alikuwa ndie mwalimu wa bendi ya shule. Bendi ya shule ya Consolata ilikuwa kati ya bendi bora wakati ule ilizidiwa na bendi ya Jamatini ya wahindi kwani wao walikuwa na vifaa bora zaidi vya muziki. Bendi hapa ni zile bendi za paredi za shule ambapo bendi ilikuwa na ngoma kubwa moja , mpiga ngoma kubwa maarufu alikuwa Naftari Kigahe. Halafu kulikuwa na ngoma ndogo tatu na wapiga filimbi kadhaa, mbele yao alikweko mshika fimbo. Huyu alipambwa vizuri sana ana alikuwa na vituko vyake vilivyoongeza utamu wa muziki wa bendi. Mwalimu Kalinga huyu alikuwa mwanaume tofauti na mama aliyekuwa mwalimu wa darasa la 1A Mlandege, alijipenda sana mara nyingi alikuwa akivaa suti, alipenda kutoa adhabu ya kumpa mtu nyundo akavunje jiwe kubwa lililokuwa nje ya shule, ilikuwa adhabu moja ngumu sana, kwani jiwe lilikuwa halivunjiki.
Jiwe la mwalimu Kalinga
Mwalimu Filangali huyu nilimuogopa sana maana alikuwa mwalimu wa hesabu na alikuwa haoni tabu kucharaza viboko, mara nyingi alivaa kaptura nyeupe na shati jeupe, soksi ndefu nyeupe ambapo alichomekea kalamu kwenye soksi, na viatu vya kahawia, mwalimu Filangali ndie aliyesababisha nitoroke shule kwa mara ya kwanza kwani sikuwa nimemaliza ‘homework’ aliyoitoa na nilijua kuwa nikiingia tu kwenye kipindi chake nitakumbana na viboko, nikashuka zangu Ruaha kuogelea na kula mitoo, japo siku niliporudi shule, nilikumbana na vitisho kuwa nitatandikwa viboko 12 vya chumvi. Ilikuwa inadaiwa kuwa wafungwa hutandikwa viboko vya chumvi ambapo kitambaa kilicholoweshwa maji ya chumvi hulazwa kwenye matako na kisha mtu hutandikwa viboko, ilisemekana viboko hivyo huuma sana, sikupigwa viboko hivyo lakini tishio hilo lilinifanya nisitoroke tena shule  mpaka nilipohama shule ile. Mwalimu wa darasa nilipofika darasa la nne aliitwa mwalimu Consolata. Huyu mama alikuwa mpole japo mara kwa mara alituchapa fimbo za mikono. Mwalimu Mkuu akiwa Mwalimu Mwinuka.
Consolata Primary School muonekano wake wa sasa
Ninakumbukumbu nyingi sana za shule ya Chemchem kwani hapa ndipo utundu nao ulianza kwa nguvu, katika shule hii nilitoroka shule kwa mara ya kwanza nilianza kuzurura mjini peke yangu kwa mara ya kwanza na nilipata marafiki ambao  tunawasiliana mpaka leo.  Baadhi ya wanafunzi niliyokuwa nao darasani kwetu ni Emmanuel ‘Katuluta’ Mkusa, Naboth Mbembati, Mage Manase, Pius Mlowe, Chesus Lutego, Emmanuel Mahingila japo alikuwa akitumia ubini tofauti, Lester Nindi, huyu alikuwa jirani yangu Makorongoni, baba yake alikuwa Mchungaji, tulifanya vituko vingi sana na Lester lakini hii ntahadithia baadae. Wengine nawakumbuka kwa majina ya kwanza tu, akina Jelasi, Macdonald, Fred, pia walikuweko wengine waliokuwa madarasa ya juu kama John ‘Mzungu’ Komba, Gerald Mkusa, Raphael Lutego, Abbas Kandoro aliyekuwa prefect kazi yake kuandika wachelewaji, Ibrahim Sareva, na jamaa aliyeitwa Odongo, ambaye alikuwa kazi yake kukamata wanaotakiwa kutandikwa ili wasikimbie.  Katika shule hii pia kulikuwa na madarasa A na B nami nilikuwa darasa la 3B na hatimae darasa la 4B. Je kiliendelea nini?



Categories: Iringa, Uncategorized

8 replies

  1. You are a very good narrator. Nakukumbuka ulifanya kazi Daily News sitakosea kuamini ulifaidika na uandishi. Nimependa

    Like

Leave a comment