
Mwaka 1963 na 1964 ndio wakati nilipokuwa nasoma Consolata Primary School, shule iliyokuja kuitwa shule ya msingi Chem chem. Eneo lote ambalo siku hizi linaitwa Frelimo lilikuwa ni pori tu, palikuwa na njia ya mkato iliyokuwa ikipita katika pori hilo kuelekea Makorongoni. Jina la Makorongoni lilitokana na eneo hilo awali kuwa na mabonde yaliyotokana na kijito kilichokuwa kikipita sehemu hizo. Kama nilivyosema awali miaka hiyo nilikuwa nikiishi Barabara mbili japo wakati huo jina hilo halikuweko mtaa huo uliitwa Tandamti Street. Pamoja na kuwa nilikuwa nikiishi si mbali sana na na shule, na kwa kweli ilikuwa nikitoka nje tu ya mlango wa kwetu, moja kwa moja naiona shule iliyokuwa mlimani lakini bado nilikuwa mchelewaji sana wa shule asubuhi. Kulikuweko na wenzetu waliokuwa wakiishi mbali sana na shule kama vile Nduli na Mawelewele lakini walikuwa wakiwahi kufika shuleni, na walikuwa wakiruhusiwa kuondoka mapema kutokana na umbali hadi kufika kwao. Asubuhi maprefect wa zamu walisimama kwenye maeneo yote ambayo kulikuwa na sehemu za kuingilia, lakini hata wakati huo rushwa ilikuweko hivyo ukichelewa hakikisha una hindi la kuchoma au matunda kama mifudu, misasati, na kadhalika ambayo ungemhonga prefect asikuandike jina. Mwenzangu mmoja ambaye alikuja kuwa kiongozi mkubwa wa Kitaifa alikuwa bingwa wa kupokea rushwa ya mitoo na misasati, kila nikimkumbusha kwa kweli hucheka mpaka machozi yanamtoka. Adhabu za uchelewaji zilikuwa nyingi ikiwemo viboko na adhabu nzito ya kusafisha vyoo. Vyoo vilikuwa ni mtaro mmoja ambao juu yake kumetengenezwa mashimo, hakukua na maji ya kuflash, hivyo adhabu kubwa ilikuwa ni kusafisha mitaro hiyo jioni baada ya kutumiwa na wanafunzi siku nzima. Dahh
Mara nyingi Alhamisi mchana kulikuwa na tukio ambalo lilitufanya tutoroke shule. Siku za Alhamisi kati ya saa tisa mpaka kumi basi la DMT kutoka Nyasaland (Malawi) lilikuwa likiwasili Iringa, wakati huo stendi kuu ya mabasi ilikuwa katika eneo ambalo kuna soko linaloangaliana na kituo kikuu cha polisi Iringa na lango la kwenda mochwari. Hili basi la DMT mara siku ya Alhamisi lilikuwa linarudi na watu ambao walikuwa wamepelekwa kwa mganga maarufu wakati ule kule Malawi aliyeitwa Chikanga. Chikanga alikuwa maarufu sana Uheheni akiwa na sifa ya kuagua na pia kuwaondoa uchawi watu waliodaiwa kuwa ni wachawi, alifanya hivyo kwa kuwachanja na kuwanyoa na kuwakanya wasirudie tena uchawi Kihehe ilijulikana kama ‘Kumogwa’. Kazi yetu wanafunzi wa shule mbalimbali siku hiyo ilikuwa kusubiri mtu akitoka na kipara ndani ya basi ni kumzomea na kumtupia makopo na kunfukuza mpaka atakakotokomea. Nakumbuka siku moja mtuhumiwa mmoja wa uchawi aliyeitwa Suvalinge alipowasili, watu wengi walikusanyika pale stendi kusubiria kumuona kwani ilisemekana aliua kichawi watu 99. Kuna wimbo Wahehe walimtungia Suvalinge wakati huo ukiwa na maneno yafuatayo:
Walye valinga Suvalinge, walye valinga
99 Suvalinge , 99 Suvalinge
Wina uhulo Suvalinge winauhulo Suvalinge
Tafsiri yake ikiwa, ulikula wangapi Suvalinge? 99, kweli we ni wa ajabu Suvalinge.
Siku Suvalinge aliposhuka alianza kusindikizwa na mawe akakimbilia ndani ya kituo cha polisi. Siku hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza na ya mwisho kuona kituo kikuu kile cha polisi kikiwa kimefungwa milango. Maana kililazimika kufungwa kuzuia watu wasimfuate Suvalinge ndani na kumuadhibu.
Waalimu wetu walikuwa wakali sana, viboko ilikuwa kawaida sana. Siku moja wanafunzi wachache wakapanga njama za kumuua mwalimu mmoja aliyekuwa mkali sana. Mwanafunzi mmoja aliyeitwa Shaibu alidai kuwa bibi yake alimwambia ukipata mchanga wa unyao wa mtu ukakaanga basi mtu huyo anafariki. Msako wa unyayo wa mwalimu huyo ukaanza. Haikuwa rahisi kuupata eneo la shule kwani eneo lilikuwa limesambazwa changarawe. Lakini kabla mpango haujatimia kwa namna ambayo sikumbuki mwalimu husika alipata taarifa kuhusu mpango huo. Siku hiyo shule nzima ghafla tukaitwa mstarini na wahusika wakaitwa mbele wote na kucharazwa viboko vingi tu na mwalimu huyohuyo, kisha akawapa mchanga wa unyayo wake akawaambia ‘Haya nendeni mkakaange sasa’
Kuimba lilikuwa jambo la kawaida sana shule, hata Wahehe tafsiri ya neno kusoma ni kuimba. ‘Akwimba sule’ maana yake anasoma shule, ‘Akwimbi kitabu’ anasoma kitabu. Kimsingi waliona kama kinachofanyika shuleni ni kuimba tu.Kuimba lilikuwa jambo la kawaida sana. Kuna wimbo ambao bado mpaka leo sijaweza kuufahanu labda wenzangu tuliosoma wote miaka hiyo (1963/64)wataweza kunifafanulia.
Nikiwa darasa la nne kuna waalimu wa mazoezi walikuja shuleni na mmoja akaja kutufundisha wimbo, ambao baadae tulifanya mashindano kati ya 4A na 4B, wenzetu wa 4A wakashinda. Wimbo wenyewe ambao tuliambiwa ni wa Kiingereza mimi nilikuwa nauimba hivi ….
My way, my way is cloudy my way God send ze chelenjez down
zea iz fire in ze east and fire in ze west
fire in ze chelenjez da
For God has sent his chelenjez down, God sent his chelenjez down, my lovely. Kila nikijaribu kutafuta maana siipati, na sijawahi kuusikia ukiimbwa na mtu mwingine tena.
Siku ya kufunga shule, hasa mwisho wa mwaka ilikuwa na shamra shamra nyingi sana. Wanafunzi wote waliambatana na wazazi wao, baada ya maelezo kuhusu hali ya shule yalianza kutajwa majina ya wanaopanda darasa, enzi hizo ukifeli mitihani, unabaki darasa hilohilo-unabunda. Mwalimu wa darasa anasimama na karatasi na kuanza kusoma, “Hawa ndio wanapanda darasa tutasoma kufuatia maksi zao, wa kwanza Naboth Mbembati”, watu wote heeeeeeeeeeeeeeeeeeee, “Wa pili Emmanuel Mkusa”…watu wote heeeeeeeeeeeeeeeeeeee. Itaendelea mpaka kufika na hawa ndio walio bunda..haya wasimame wanatajwa majina na mnaambiwa wazomeeniiii…..yuuuuuuuuuuuuuuuuuu. Hapo sasa bado kipigo cha wazazi kinawangojea na kejeli kutoka kwa wanafunzi wenzio wakati wote wa likizo na mwaka mzima unaofuatia kwa kuwa darasa la nyuma. Sentensi ya mwisho ya Mwalimu Mkuu siku ya kufunga shule ilikuwa ’Na sasa shule imefungwa na itafunguliwa tarehe 3 Januari’, Wakati vifijo na nderemo za kufurahia likizo zikiendelea kulikuweko na wanafunzi waliokuwa wakikimbia haraka toka eneo la shule, maana siku hii ilikuwa ya malipo, ngumi zilikuwa zinaumuka kila kona, huyu anadaiwa gololi, yule hajalipa mikusu , mwingine alimnyima mwenzie kashata. Basi ukisikia ‘Ngumi ngumi” unakimbilia kuona kuna nini na siku hiyo haziamuliwi mpaka atandikwe mtu.
Likizo ilikuwa raha sana mambo mengi ya kufanya,kutengeneza baiskeli za miti, magari ya maberingi, kwenda Itamba kuiba maembe, kuwinda ndege na manati.
Kutengeneza manati kulikuwa na taratibu zake, kwanza ukisha tengeneza manati yako unafanya chini juu umpige mbayuwayu, halafu unajichanja mkononi na kisha unapaka damu ya mbayuwayu, tuliamini hiyo inakufanya uwe na shabaha sana na manati yako!!!. Likizo ilikuwa ndio muda wa kula matunda mengi ya porini na kuwinda sana siku ya bahati mnapata sungura mnakula hukohuko porini lakini lazima uweke nafasi ya kula nyumbani kwa sababu ole wako ufike nyumbani useme umeshiba, ikijulikana ulikula kwa watu kipigo chake si kidogo……ITAENDELEA
Categories: Iringa
Manati John ya ufundi wake! kwanza mpira usiwe “lupu” Halafu kuna miti maalum ya kutengenezea kipago! Ufundi na umakini wa kukata “vinyutilo” na ufunga wake wacha mchezo Manati kwa kokoto au “mburungwa”! Sio mchezo kakaa!
LikeLike