Mwishoni mwa mwaka 1962, nilihamia kwa babu yangu aliyekuwa anaishi Barabara Mbili Makorongoni, kisha mwanzoni mwa mwaka 1963 nikahamishwa shule kutoka shule ya serikali ya Goverment Lower Primary School (Mlandege) na kuhamia shule iliyokuwa ikiendeshwa na kanisa Katoliki, Consolata Primary School (Chem Chem). Hapa nikapata marafiki ambao wengine ni watu muhimu kwangu mpaka leo. Mwaka 1963 nilianza darasa la 3, nikapangwa darasa la 3B. Wasomi wazuri kadhaa walikuja patikana kutoka darasa hilo, Profesa Mbembati, Injinia Lutego, pia alipatikana Mkuu wa wilaya Mlowe hao ni kati ya wachache ambao nina taarifa zao. Rafiki yangu mkubwa alitoka 3A, alikuwa anaitwa jina la utani Katuluta, ilisemekana jina lake lilitokana na kutoweza kusema kaptura na kuiita katuluta wakati akiwa bado mdogo, Katuluta alikuwa bingwa sana wa hesabu, aliwahi kushinda mashindano ya hesabu ya nchi za Afrika Mashariki tulipokuwa kidato cha pili, na aliendelea kuwa mtaalamu wa hesabu mpaka kifo chake. Marehemu mkuu wa mkoa maarufu Abass Kandoro alikuwa mmoja wa wanafunzi katika shule yetu, tena alikuwa kiranja. Kati ya wanafunzi ambao walijitokeza pale shuleni ni John Mzungu, na jamaa mmoja ambaye alikuwa kajengeka vizuri kiafya hivyo kutumiwa na waalimu kufukuza na kukamata wanafunzi waliokuwa wakitoroka adhabu, nakumbuka alikuwa anaitwa Odongo. Nadhani alikuwa Mjaluo. Waalimu maarufu walikuwa Mwalimu Lucia huyu alikuwa ndie mwalimu wa darasa letu, waalimu wengine walikuwa mwalimu Mfilinge, aliyekuwa mwalimu wa hesabu aliyependa kuvaa kaptura nyeupe na shati nyeupe, soksi ndefu zilizofika kwenye magoti. Kulikuweko mwalimu Kalinga , jamaa smart sana aliyekuwa ana vaa miwani na anapenda kuvaa suti nyeusi. Halafu kulikuweko na mwalimu aliyejulikana kwa kila mwanafunzi mjini, huyu aliitwa Mwalimu Daudi, alikuwa yuko katika kila kona, alikuwa mwalimu wa muziki na ndie aliyekuwa anaifundisha bendi ya shule, alikuwa kwenye michezo, na hata baadae akawa refa muhimu katika soka pale Iringa, alikuwa mchoraji, ndie aliyekuwa akifuatilia kama tumeenda kanisani kila Jumapili na alikuwa hachelewi kutumia kiboko.

Katika miaka hiyo wanafunzi tulianza kujifunza Kiingereza darasa la tatu kwa kutumia kitabu cha Oxford English Book one. Sababu ya kuanza kufundishwa lugha ngeni darasa la 3 ni kuwa wanafunzi wengi walianza shule wakiwa wanajua lugha yao ya asili tu, hivyo hata Kiswahili ilikuwa lugha ngeni. Tulipata tabu sana kuanza kujua namna ya kutamka, this is a door na that is a book, tuliweza sana kusema zi zi a doo, zat iz a buku. Babu yangu alikuwa mwalimu msataafu wakati huo, hivyo nilipata bahati ya kuwa na darasa jingine niliporudi nyumbani saa za jioni.
Nyumba yetu ilikuwa kilipo kilabu cha Barabara mbili,ulikuwa mtaa mzuri kulikuwa na taa za barabarani hivyo tulikuwa nje kucheza hata baada ya kuingia giza. Maji yakuwa yakipatikana aidha kwa kununua kwa watu waliokuwa wakipitisha wakiwa wamebeba, tulikuwa tunawaita ‘ ‘Mzegamzega’, debe la maji lilikuwa linauzwa senti tano kama unanunua toka kwa Mzegamzega, au uliweza kwenda bombani ambako kulikuwa na mashine ambayo ukiingiza senti moja unapata debe zima la maji. Kibanda cha kuuzia maji kilikuwa pembeni ya barabara inayotokea stendi ya mabasi ya sasa na kushuka bondeni. Hapo ilipo stendi ya basi palikuwa ni makaburi. Eneo la makaburi lilikuwa kubwa kuanzia ilipo stendi na kuelekea upande wa Mashine tatu hadi kule ambako inakutana barabra ya Mashinetatu na ile ya kutoka Makorongoni. Sehemu hii kwa sasa ni sehemu ambayo imejaa wafanya biashara ndogondogo. Kwa vile tulikuwa tukiishi Barabara mbili , hiyo sehemu ya makaburi ambayo sasa ni stendi, ilikuwa ndio sehemu yetu ya kucheza, kwani kufikia mwaka 1964, mazishi yalikuwa yakifanyika katika makaburi ya Mlandege. Barabara mbili kama lilivyojina ina barabara mbili ya juu na ya chini. Ya Juu ilipewa jina la Mtaa wa Tandamti. Nyumba ya kwanza mtaa huu ilikuwa ya mzee mmoja aliyekuwa mganga hodari sana. Nyumba ya pili ilikuwa ya Mwarabu na kulikuwa na duka. Nyumba hii ilikuwa muhimu sana hasa wakati wa sikukuu za Iddi, hapa ndipo tulipoweza kula pilau, chakula ambacho hakikuweko nyumbani kabisa.

Pamoja na kuwa mahala ambapo tuliweza kufaidi pilau siku ya Iddi, kwa Mwarabu kulikuwa duka la vitu ambavyo vilikuwa muhimu kwetu kama vile, peremende kifua, peremende kijiti, peremende mbinga, bazoka, sukari guru, kashata na kadhalika, na juu ya hayo yote kulikuwa na Kasuku, ambaye tulikuwa tukimchokoza kila siku. Tulikuwa tukifukuzwa kila siku na tulikuwa tunarudi tena kila siku. Katika moja ya nyumba ambazo zilikuwa zikiangaliana na makaburi alikuwa akiishi Pasta mmoja mzee kutoka Malawi, lakini alikuwa na mwanae ambae alikuwa rafiki yangu sana, siku moja tukaamua lazima na sisi tuanzishe bendi kama ile tuliyokuwa nayo shule. Kwa mbinu ambazo si halali tuliweza kupata shilingi tano, fedha ambayo iliweza kutufanya tununue ngozi ya ngombe ya kuwamba ngoma. Tulienda kuiloweka ngozi hiyo kwenye kisima kilichokuwa bondeni mwisho wa barabara inayotoka stendi. Baada ya siku chache tulienda kuangalia ngozi yetu hatukuikuta ilikuwa imeibiwa. Katika kupepeleza kujua mwizi wetu, tukaambiwa ngozi ile aliichukua bwana mmoja aliyekuwa mwalimu wa shule ya chini ya mti, hizi zilikuwa shule za nursery za kujitolea, zilikuwa zikianzishwa chini ya miti. Huyu bwana tulimfahamu alikuwa akiishi mtaa wa pili toka kwetu, lakini tuliogopa sana kumuuliza maana aliwahi kujaribu kujinyonga bahati mbaya/nzuri kamba ikakatika, hivyo akili yake haikuwa sawa alikuwa haongei na wakubwa ila watoto wadogo aliokuwa akiwafundisha, tukalazimika kuachana na mpango wa kuanzisha bendi kama ya shule na kuendelea kutengeneza ngoma za makopo…..ITAENDELEA
Categories: Iringa