
Moja ya taasisi ya zamani katika mji wa Iringa ilikuwa shirika lililoitwa EAR&H. East African Railways and Harbour, aarufu kwa jina la Relwe. Shirika hili la usafiri la Afrika ya Mashariki lilianza mwaka 1948, kwa vile Kenya Uganda na Tanganyika zilikuwa chini ya Waingereza basi walianzisha shirika moja la usafiri kwa nchi zote tatu, shirika lilishughulika na usafiri wa reli, barabara na majini. Iringa ilikuwa makao makuu upande wa usafiri wa barabara. Iringa ndio ilikuwa na gereji kubwa ya magari na ilikuwa na magari mengi ya mizigo na mabasi. Kulikuwa na usafiri wa mabasi na magari ya mizigo kutokea Iringa kwenda Mbeya, Njombe, Dodoma, Tunduma, Kyela, Chunya, Moshi na Dar es salaam. Kulikuwa na mabasi yaliyoondoka asubuhi na mengine yaliyoondoka usiku kwenda sehemu hizo nilizotaja, na kwa kuwa shirika hili lilikuwa pia ni la reli na majini, iliwezekana kukata tiketi Iringa ukasafiri na basi mpaka Dodoma na huko kuingia katika treni mpaka Mwanza na ukapanda meli kwa tiketi hiyohiyo. Awali ilikuwa ukitaka kwenda Dar es Salaam kutoka Iringa ilikuwa lazima upande basi mpaka Dodoma na kule unapanda treni mpaka Dar es salaam. Lakini wakati nilipokuwa naishi Makorongoni mwaka wa 63/64 tayari usafiri wa basi wa moja kwa moja mpaka Dar es salaam ulikuweko.
Mabasi ya relwe yalikuwa na madaraja mawili. Daraja la pili na daraja la tatu, hivyo kulikuwa na nauli mbili tofauti katika basi moja. Nyuma ya dreva kulitengenezwa chumba ambacho kilikuwa na viti vichache vyenye sponji nene na hicho ndicho kilikuwa chumba cha daraja la pili, kwa tiketi ya daraja hili ungekuwa pia daraja la pili kwenye treni na meli ikiwa utalazimika kusafiri huko. Kupata nafasi hiyo ililazimika kubook. Viti vyake vilikuwa na sponji zaidi ya vile vya daraja la tatu, na katika miaka ya ukoloni pasenja wa daraja hili ndio walikuwa wakiingia katika hoteli za shirika kupata chai na vitafunio. Relwe ilikuwa pia na hotel, hoteli ya kwanza ilikuwa jengo linalounganika na benki ya Mkombozi kwa siku za leo, baadae ikahamia katikajengo la hoteli iliyokuwa inajulikana kama White Horse Hotel, jengo lililokuwa likiangaliana na kanisa la Anglikana, miezi michache iliyopita jengo hilo limevunjwa. Relwe ilikuwa na timu kali ya soka na ilikuwa kati ya timu bora mjini hapa. Lakini pia ilifahamika kwa utemi, kwani madereva wa magari ya Relwe hawakuwa watu wa mchezo mchezo. Jirani na ofisi za mkoa za CCM ndipo zilipokuwa nyumba za wafanyakazi wa relwe, tuliziita ‘kota za relwe’. Watoto wa Makorongoni na wa kota tulikuwa marafiki hata timu zetu za mpira zilichanganya watoto wa sehemu zote. Kulikuwa na mechi nyingi za mitaa, zilizoishia ngumi mara nyingi. Watoto wa Kitanzini tulikuwa tunawaogopa kwa ngumi. eneo kuanzia nyuma ya maktaba ya Iringa mpaka shule ya Wilolesi lilikuwa eneo la wazi lililokuwa uwanja wa mchezo wa gofu. na pia ulikuwa uwanja wetu wa kurushia vishada/tiara. Ulikuwa umepandwa majani mazuri ya kijani na kukawa na miduara iliyomwagiwa mchanga uliochanganywa na lami na hayo yalikuwa mashimo ya mchezo wa gofu. Wale wajanja walikuwa wakija hapa na kuomba kibarua cha kubeba mifuko ya magongo ya gofu. Na sie tukawa tunachonga magongo yetu ya miti na kuibia kucheza gofu uwanjani hapo. Nyuma ya benki ya NMB kulikuwa na nyumba ya klabu iliyoendesha uwanja huu ilikuwa inaitwa Iringa Club. Ilikuwa ni kwa Wazungu waingereza tu. Wagiriki walikuwa na klab yao karibu na shule ya Gangilonga, Wahindi walihamishwa kutoka ulipo uwanja wa Samora na kuhamishiwa jirani na uwanja wa Sabasaba.

Nyuma ya kota za relwe kulikuweko majengo ya tofali, kwa sasa zimekuwa ofisi za shughui mbalimbali. Majengo haya yalikuwa mali ya Sisal (Labour Bureau SILABU). Silabu ilikuwa taasisi ya kutafuta vibarua wa kwenda kwenye mashamba ya mkonge. Hivyo vibarua walikusanywa sehemu mbalimbali na kuja kufikia hapa kabla ya kuendelea safari kwa malori kuelekea Tanga, Morogogo na kwingineko kwenye mashamba ya katani. Tulikuwa tunafurahi sana ujio wa hawa watu waliojulikana zaidi kama manamba kwani walitambuliwa kwa namba zao walikuja pewa na SILABU (angalia pichani wameshika karatasi za namba zao zilizoitwa ‘vipande’). Ujio wa watu hawa ulitupa ulaji, kwani tulikuwa tunaenda kwa Bwana Mikate, Mgiriki mmoja ambaye alikuwa ana oka mikate na kusambaza Iringa yote, yeye alikuwa akiitupa mikate iliyokosa wateja baada ya siku kadhaa, sisi tukawa tunaomba mikate hiyo na kwenda kuwauzia Manamba…...ITAENDELEA TU
Categories: Iringa, Uncategorized