LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 8


Shule ya msingi Chem Chem ilivyo sasa.

Katika kumbukumbu ya mwisho niliandika jinsi tulivyokuwa tukimaliza siku darasani kwa kukimbilia nyumbani tukiwa tumevaa kaptura za ‘stakapoti’. Je stakapoti ni nini? Katika masharti ya shule miaka ya mwanzo ya Uhuru na miaka kadhaa baada ya hapo, sare za shule zilikuwa kaptura ya khaki na shati jeupe. Kaptura ilikuwa lazima iwe khaki iliyotengenezwa Uingereza katika mji wa Stockport. Shati ilikuwa lazima kiwe kitambaa cheupe kiichoitwa Jinja iliyotengenezwa na kiwanda cha nguo cha serikali ya mkoloni huko Uganda. Wakati tunaanza darasa la kwanza pale Goverment Primary School kulikuwa na fundi maalumu anakuja kutupima pale shuleni na nguo tuligawiwa tukiwa kwenye mistari na mwalimu George Nyakunga aliyekuwa Headteacher alituita mmoja mmoja na kututupia sare zetu. Shati ilishonwa kwa mfano wa tshirt yenye shingo ya mviringo, haikuwa na vifungo. Ilikuwa furaha kubwa kugawiwa nguo mpya , kazi ilikuwa kuziweka safi, kwani kila asubuhi kulikuwa na ‘ukaguzi’ kabla ya kuingia darasani. Wote tulijipanga kwa mistari na huku bendi ya shule ikipiga, waalimu walipita mistarini kwanza walikagua usafi wa kucha kwa kila mtu kunyoosha mikono yake mbele kuangalia urefu na usafi wa kucha, kisha kunafwata ukaguzi wa usafi wa nguo, na baadae usafi wa mwili kwa kukwangua nyuma ya kisogo, ukitoka uchafu maana yake hujaoga muda mrefu. Amini usiamini katika shule nyingine ilikuwa hakuna ruksa kuvaa viatu vya ngozi, ni viatu vya raba tu kwa wanafunzi na kwa zile shule ambazo viatu vya ngozi viliruhusiwa kulikuwa na viatu maalumu vilivyoitwa scout, kiukweli asilimia kubwa ya wanafunzi walikuwa hawana viatu. Ndoto ya kuvaa suruali ilikuwa haipo kabisa. Kama tutakavyoona mpaka nilipomaliza kidato cha nne miaka mingi baadae, sare ilikuwa kaptura tu.
Mwaka 1963 nilihamia shule jirani iliyokuwa inamilikiwa na kanisa Katoliki. Shule hiyo iliitwa Consolata Primary School. Hata huku sare za shule zilikuwa zile zile ila hapa ilitakiwa kuchora nembo ya shule kwenye mfuko wa shati. Hivyo shati ilishonewa maandishi ya bluu yaliyosomeka CPS. Nakumbuka mama yangu aliyadarizi maandishi yale nikawa najiona mjanja sana. Kama nilivyoeleza kabla shule hii ndipo nilipoanza kujifunza Kiingereza,na masomo mengine kama Maarifa ambamo ndani yake kulikuwa na Jiografia na Historia. Lilikuweko pia somo la Afya. Namkumbuka sana mwalimu wangu wa hesabu darasa la nne alikuwa anaitwa mwalimu Mfilinge, sababu ya kumkumbuka zaidi ni mkasa ulionitokea siku moja kutokana na kipindi chake ambacho kwa kweli nilikuwa sikipendi kabisaaaaa. Kipindi cha kwanza Jumatatu kilikuwa hesabu, baada ya kipindi alitoa ‘homework’ ambayo ilitakiwa tuionyeshe kweye kipindi chake siku ya Jumanne mchana. Jumanne ilipofika sikuwa nimefanya kazi ile na nilimjua mwalimu Mfilinge lazima atanichapa viboko, nikaamua kutoroka shule na kwenda chini mtoni Ruaha ambako pamoja na kuogelea na kuvua samaki kulikuwa na matunda mengi ya porini hivyo ukiwa huko unakuwa bize na pia utakutana na watoro wenzio kutoka shule nyingine. Nilishinda huko nilikla mitoo na matunda mengine. Kesho yake nililazimika kutoroka kwa kuwa nilitoroka jana yake. Nilikuwa sasa nimetenda makosa mawili sikufanya homework na nilitoroka shule, hivyo adhabu sasa zitakuwa zimeongezeka. Niite bahati nzuri nilikuwa nasoma na mdogo wangu akaulizwa niko wapi akajibu niko darasani kwangu, waalimu wakajua mimi ni mtoro, wakamwambia mdogo wangu amwambie mama kuwa sionekani shule. Kesho yake baada ya uji wa asubuhi, nikawa najitayarisha kujongomea kusikojulikana, mama yangu akanambia nioshe baiskeli yake maana tunaenda wote shule. Mama alikuwa mama maendeleo kwa hiyo serikali ilimpa baiskeli ya kuzungukia vituo mbalimbali vya akina mama. Kikweli kwa lugha ya siku hizi nilijua soo limebumbuluka. Mama alipokuwa tayari tukelekea shuleni, yeye akiwa anasukuma baiskeli yake. Tulipofika shuleni waalimu ambao wote walikuwa wakifahamiana vizuri na mama walianza kwa vigelegele, ‘Lululululu, Christina umetuletea mtoro wetu?’ Mama akajibu, ‘Nimemleta ananisumbua sana huyu mtoto’. Mwalimu mmoja akaanza. ‘ Mimi nina kipindi saa hizi lakini huyu ana viboko vyangu 6 nikimaliza kipindi’, waalimu wengine kama watatu wakaaga kwa mtindo huohuo, nikaanza kulia kwa kuwa tayari nina mkopo wa zaidi ya viboko 20. Baadae akaingilia mwalimu tuliekuwa tunamuogopa sana, Mwalimu Daudi, yeye akakoleza mazungumzo kwa kusema hivi’ Huyu mtoto dawa yake tumtandike viboko vya chumvi ndio atakoma kutoroka shule’. Wakati huo tulikuwa tukihadithiana kuwa wafungwa magereza huwa wanatandikwa viboko vya chumvi. Kitambaa kinalowekwa kwene maji ya chumvi kisha kinatandikwa kwenye matako, halafu ndio anachapwa viboko. Tulijiaminisha kuwa hakuna viboko vichungu kama hivyo. Niliposikia hivyo nikawa namuomba msamaha mama, yeye alichofanya nikuwa ambia waalimu haya huyo nawaachieni kazidi sana. Nikaambiwa niende darasani nitaitwa baadae kulipa madeni. Nadhani wote mtafahamu hali yangu ilivyokuwa mbaya. Siku ile ikapita na nyinyingine na nyingine sikupigwa hata kiboko kimoja , lakini sikutoroka shule tena mpaka nilipomaliza kidato cha nne……ITAENDELEAAA

Categories: Iringa, Uncategorized

1 reply

  1. hah hah hah kweli ulipitia mengi Kijana wa siku nyingi, mimi nilikuwa natoroka kuwinda ndege na kwenda Old Salender bridge kuvua samaki, wakati huo tupo pale four flat Upanga tulipohamia mwaka 1961
    Thanks very much for flash back

    Like

Leave a comment