LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 9


Padri Henry Chelula (RIP)

Wazazi wangu walikuwa watu wa ‘dini’, wote wawili walikulia Tosamaganga na kusoma katika shule za misheni za hapo Tosamaganga. Baba aliwahi kusoma Mpwapwa kwa muda mfupi kwa kuwa babu yangu alikuwa mwalimu huko lakini baadae kuanzia darasa la nne mpaka kupata kozi ya ualimu alisoma Tosamaganga. Mama, yeye alianza darasa la kwanza mpaka kozi ya ualimu palepale Tosamaganga, hilo liliwafanya wakulie katika mazingira ya Kikatoliki na walitulea watoto wao katika dini hiyo pia. Kama ilivyo kawaida ya watoto wa Kikatoliki lazima waanze na ‘Mafundisho’. Naikumbuka vema siku baba ananipeleka kuanza mafundisho. Nilikuwa nina miaka sita. Tulitoka nyumbani, nyumba ilikuwa ulipo uwanja wa Samora na kutembea kwa miguu mpaka kanisa la Mshindo. Siku hiyo iko kwenye kumbukumbu zangu kwa kuwa kulitokea ajali nje tu ya lango la kanisa. Pale nje ya kanisa kuna njia panda ya barabara itokayo Mshindo na ile itokayo Uhindini, gari lililotoka Uhindini liliingia barabara kuu wakati kuna mzungu mmoja akiwa kwenye skuta, siku hizi huitwa zaidi vespa, anaelekea Miyomboni, ile vespa ikajigonga ubavuni mwa ile gari, baba alikuwa akiongea na mtu tulikutana nae pale barabarani, mimi nikawa namshtua baba aangalie. Tukakimbilia pale na watu wakambeba yule mzungu na kumuingiza kwenye gari aliyogonga. Baada ya hapo nikapelekwa kwa sista kuandikishwa kuanza mafundisho. Darasa tulilokuwa tukifanyia mafundisho lilikuwa nyuma ya kanisa Katoliki la Mshindo, nyakati za asubuhi darasa hilo lilikuwa ni ‘supu standad’ rasmi ni sub standard yaani siku hizi madarasa hayo yanajulikana kama Nursery au Chekechea. Jioni linakuwa darasa la mafundisho. Kwanza nikapewa kitabu cha rangi ya pinki kilichoitwa Katekismo, hicho ndicho kitabu cha mafunzo ambacho baada ya miezi kadhaa ilikuwa kunamtihani, ukipasi ndipo unapata Kipaimara. Basi ungekuwa umepita saa za mchana jirani na darasa hilo miaka hiyo ungetusikia tukijibu maswali kama haya;
Tu duniani kwa sababu gani?
Tu duniani kumtumikia Mungu na kusali
Tena
Tu duniani kumtumikia Mungu na kusali
Tena
Tu duniani….

Ukiwa mdogo kanisa huwa linaonekana kubwa sana, huwa nikiingia kanisa lile nashangaa naliona kama limekuwa dogo, pia huwa nakumbuka mengi yaliyowahi kutokea ndani ya kanisa lile. Kwa kuwa kila Jumapili na sikukuu ilikuwa lazima kwenda kanisani, mambo mengi yasiyo ya kawaida yalifanyika pale. Siku moja siku ya Ijumaa Kuu, wakati wa misa ya usiku, kila mtu alikuwa na mshumaa, siku hiyo nilikuwa nimekaa na mama upande wa akina mama, mshumaa niliokuwa nao ukaangukia kwenye kanga ya mama mmoja aliyekuwa mbele yetu na kanga ikashika moto, ni miaka mingi sana toka tukio hili lakini nakumbuka jinsi vurugu iliyotokea hapo kanisani na kichapo kilichofuata nilipofika nyumbani. Mpaka leo nimekuwa mwangalifu sana wa mishumaa. Mapadri na mabruda wengi walikuwa Wataliano, Padri Rioli au Padri Oli mpaka leo sijajua lipi sahihi, huyu alikuwa akitugawia pipi siku za siku kuu, kulikuweko na majina kama Padri Balbanti, Padri Muso, Bruda Modestus huyu alikuja kuwa maarufu sana pale Iringa kwani alikuwa refarii wa soka, pia alikuwa na pua ndefu iliyokuwa kama nembo yake. Kulikuweko Bruda Gwerino, halafu alikuweko Buruda Anjelo huyu alikuwa na sauti nzito sana. Wakati wa ibada ya wiki ya Pasaka kwenye maigizo ya Mateso ya Bwana Yesu, yeye ndie aliyekuwa akishika nafasi ya Yesu. Na hakika tulipokuwa watoto tuliamini kuwa sauti ya Yesu ilikuwa nene vile. Tulikuwa tukisubiri sana yale maneno ‘Yesu akasemaaaaa’ ‘Mwamtafuta nani?’ na ‘Ndiyeee mimi’.

Mbele Henry, Sister Michaelanjela, mimi 1964


Watoto tulikuwa tukiwahi mafundisho ili tucheze ‘kutereza’ kwenye kuta za mlango mkuu wa kuingia kanisani, hakika kaptura nyingi zilichakaa katika kuta zile. Ndani ya eneo la kanisa pia ndipo kulikuwa na zahanati wenyewe tuliita ‘dispenzali’, Sista mmoja mzungu ndie alikuwa akitibu kila kitu kuanzia kung’oa meno mpaka malaria, na kugawa pipi ukishachomwa sindano.
Baadae nilihamia Kihesa na huku likawa ndio kanisa langu kuu, kiukweli mpaka leo najisikia ni mwanaparokia ya Kihesa. Hapo ndipo nilipoanza kutumikia kanisani, nilizunguka vigangwe vingi nikiwa na Padri Cosmas, Padri Kangalawe na Padri Mario Mgulunde ambaye baadae akaja kuwa Askofu Mgulunde katika Misa kubwa iliyofuatiwa na sherehe iliyofanyika katika viwanja vya Boma (Garden). Kulikuwa na raha za kusafiri na padre, kwani kule vigangoni waumini walikuwa wakitayarisha chakula cha padri, mara nyingi wali kuku na soda, we acha tu. Jumapili nyingine nilikuwa nawahi kutumikia misa ya asubuhi kisha kuanza kuuza magazeti ya Mwenge na Kiongozi mbele ya kanisa mpaka misa zote zilipoisha, magazeti yalikuwa mradi wa masista, nikimaliza kuuza nawapelekea hela na magazeti yaliyobaki kama yapo, naondoka hapo na mkate au keki.
Kanisa la Kihesa lilikuwa lile dogo pembeni mwa kanisa la sasa. Nyuma ya kanisa ilikuwa ndio hosteli ya kwanza ya wasichana wa Iringa Girls.
Nyuma ya lilipo kanisa ndipo kulikuweko na Zahanati ambayo nilitibiwa mara nyingi sana. Huku kuzunguka na mapadri na kushinda kanisani muda mwingi kukanifanya nianze kutaka kuwa padri. Ari ya kuwa Padri iliongezeka nilipoenda kutumia likizo yangu kwa mjomba wangu aliyekuwa padri. Mjomba wangu huyo Padri Henry Chelula alikuwa akisimamia kanisa lililokuwa Kitanewa jirani na Idodi, likizo nzima nikawa huko. Kusali kila baada ya masaa machache, muda mwingine shughuli za shamba na kadhalika, yeye alikuwa na maktaba ya vitabu vya watoto, katika vitabu hivyo kulikuwa na hadithi nyingi za watoto walioenda mbinguni kutokana na kusali na kujiunga na upadri na kadhalika, nikawa sasa na mimi nikaojiona naweza na ni muhimu kuanza kujitayarisha kwenda mbinguni. Sijui mipango ile ilipoteaje, ngoja nijipange upya……ITAENDELEAAAAAA


Categories: Iringa, Uncategorized

Tagged as: , ,

1 reply

  1. so wonderfull, really, I like it very much and reflect my life as I was at MSIMBAZI BOYS PRIMARY SCHOOL IN EARLY 60s
    Good staff, thanks

    Like

Leave a comment