
Ukishuka chini toka mtaa wa Barabara Mbili unafika mtaa ambao barabara yake inatokea Kitanzini na kuelekea Mwembetogwa. Katika miaka ya 60 kwanza ilikuwa njia nyembamba sana ambayo ili kuvuka ililazimu uruke ule mfereji wa maji yaliyokuwa yakitoka Miyomboni. Maji haya yalichonga mfereji mwembamba lakini ulioenda chini sana, kuna siku moja mlevi mmoja alikosea hatua akatumbukia mle na kuvunjika shingo na kufariki, kwa muda mrefu tulikuwa tukipaogopa mahala hapo. Upande wa kulia wa barabara kama unaelekea juu Kitanzini kulikuwa na bustani za wakazi wa Makorongoni, Wahehe huita Ifyungu. Mama yangu alikuwa na eneo pale na kama ilivyo kawaida watoto wote tulikuwa na zamu ya kwenda kumwagia maji mchicha, nyanya, vitunguu na kadhalika. Tulikuwa tunaishi na shangazi yetu ambaye ndie alikuwa akihakikisha tunaenda kwenye fyungu kumwagilia wakati yeye kasimama pembeni. Baada ya muda shangazi akazoeana na kijana mmoja aliyekuwa akifanya kazi Iringa Dry Cleaners iliyokuwa mali ya Singasinga mmoja. Nyumba hii ya dry cleaners baadae ilikuja kuwa bar maarufu iliyoitwa Mawenzi Bar, na kwa sasa ni Guest House inaitwa Highland Lodge, ipo kwenye njia panda ya barabara kuu na barabara inayoshuka kwenda Makorongoni. Huyu kijana alikuwa na baiskeli spoti na akawa anajiita Shariff Jamal. Wakati huo Shariff Jamal wa ukweli alikuwa muhindi mmoja tajiri aliyekuwa na mashine za kusaga unga kule Mlandege. Baadae tulikuja jua kuwa jamaa alikuwa Muhehe mmoja wa ukoo wa akina Salufu. Nilipokuwa mkubwa ndipo nilipokuja kumuelewa huyu jamaa, maana alikuwa akija kuongea na shangazi muda mrefu, na mara nyingine alikuwa akitoa machozi, na shangazi nae akawa anatoa machozi, wakawa siku nyingine wanakaa pembeni ya kisima wameshikana lakini wote wanatoa machozi. Ili nisiwasumbue, Shariff Jamal alikuwa akiniletea sukari guru nisimwambie mama kuwa huwa anakuja pale shambani. Siku moja hakuja na hongo, mjumbe Ikalazimika nimwambie mama. Tukiwa tunakula nikamwambia mama, ‘Shariff Jamal huwa anakuja shambani halafu yeye na shangazi wanalia’. Nadhani mama alielewa somo mapema, maana ghafla kukawa na ugomvi mkubwa, shangazi akaambiwa atarudishwa kijijini.
Mtaa huu wa Makorongoni ulikuwa unashuka na huko mwisho wa Makorongoni kabla hujaaianza Mwembetogwa kulikuwa na sehemu ambapo Wabaniani walikuwa wakichoma maiti za wafu wao, huko pia kulikuwa na machinjio ya ng’ombe na mbuzi. Kabla hujafika Ilala lilikuweko dampo la mji wa Iringa. Hapa pia palikuwa sehemu tuliyotembelea sana kujaribu kuokota hiki na kile kwa ajili ya kuchezea. Kuna wakati tulikuwa tukienda kuokota betri zilizotupwa kwani tulikuwa tumeanza kujua kuwa betri zinaweza kuwasha balbu. Huku dampo tuliokoteza betri na kuunganisha kupata mwanga. Kuna mtu alianzisha habari kuwa betri zile ukiunganisha halafu uzitumbukize kwenye shimo la choo zinakuwa haziishi tukawa tunawaza namna ya kuwa na taa za umeme wa betri majumbani mwetu. Pia tulienda dampo, wenyewe tulikuita tu jalalani, tulienda dampo kuokota mabox ili kutengeneza sinema. Kwa kutumia vivuli vya picha tulizokata na mwanga wa bulb za tochi tulikuwa tukionyesha sinema za aina yake hasa uvunguni mwa vitanda kwenye giza. Mwishoni mwa mwaka 1964 baba akalazimika kuhamia Mbeya kwa mwaka mmoja, tukahama…….ITAENDELEEEEA
Categories: Iringa