
Weekend hii nimeona nikusanye maoni mbalimbali niliyotumiwa na waliosoma vipande hivi vya historia ya Iringa. Kwanza natoa shukrani kubwa kwa waliocomment humu, walionipigia simu na walioniandikia kwenye message na whatsapp wakitoa maelezo ya ziada au kumbukumbu zao kuhusu Iringa ya miaka hiyo. Nawakaribisha wote wenye kumbukumbu tukumbushane, kwani mimi naanzisha changamoto tu. Nianze na kumbukumbu aliyonitumia Mzee Evans Mapundi ambaye pia alinipigia simu kuniongezea maelezo mengi sana. Mzee Mapundi alikuwa mmoja wa waliosoma Iringa Middle School. Akiongelea hali ya kisiasa muda mfupi kabla ya Uhuru, Mzee alisema kuwa kulikuwa na chama cha siasa ambacho kilianzishwa na Gavana wa Tanganyika wakati ule kiliitwa United Tanganyika Party (UTP). Wafanyakazi wengi wa serikali walilazimika kujiunga na chama hicho kwa hofu ya kufukuzwa kazi, kati ya anaokumbuka walikuwa wanachama wa chama hicho ni Chief Adam Maomba Sapi, Mwalimu Francis Kitime, Mzee Amran Mayagila aliyekuwa District Education Officer, Dr Varty Mwanjisi ambaye 1958 alikuwa na hospitali binafsi yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 30, hospitali hiyo ilikuwa mwisho wa Makorongoni kama unaelekea Mwembetogwa. Mzee Mwingine aliyekuwa mwanachama wa chama hicho alikuwa Mzee Charles Nindi, ambaye ni babu ya Mzee Evans ambaye wakati huo alikuwa Bwana Afya wa Wilaya. Mzee Nindi ambaye alikuwa Mnyasa, baada ya kustaafu kazi ya Ubwana Afya alianza kazi ya uchungaji na ndie aliyeeneza sana kanisa la Kianglikana katika mji wa Iringa na vitongoji vyake. Nyumba ya Mzee Nindi ilikuwa ikiangaliana na ilipo stendi ya mjini kwa sasa.

Rafiki yangu, mkazi mwenzangu wa Barabara mbili, ambaye tuliathirika sana kwa upenzi wa kashata za nazi Bwana Shukuru ambaye sasa anaishi Tanga, na ni mwanasheria mahiri huko alikuwa na kumbukumbu hii ya utoto wake. “Hapo makorongoni barabara mbili ndipo nilipofundishwa kiingereza nikasoma kuanzia Oxford English Course kuanzia Book two hadi Book five. Nikifika shuleni nilikuwa nazungumza na kusoma kiingereza nikistajaabisha watu sana. siku moja niliitwa kusoma kitabu darasa la tano pale Shule ya Consolata Roman catholic primary school humo Darasani alikuwepo marehemu Esteriunus Mahingira baadae ndiye aliyekuwa Msajili wa Makampuni BRELA. Je unajua aliyekuwa mwalimu wangu wa tution hiyo? alikuwa ni babu yako Mr. Kitime wakati huo alikuwa amekwisha retire ambaye na mimi ni babu yangu kiumri na Mwalimu wangu mkuu wa kiingereza. Baba yangu akaamua kunihamishia shule nyingine ya English medium wakati huo inaitwa HIGH RIDGE PRIMARY SCHOOL. Hapo waalimu wote kasoro 2 walikuwa wahindi , wanafunzi wote Wahindi, Magoa na Shelisheli au Seychelles. Kule nikamkuta binti mmoja wa kishelisheli (Seychelles ) kwa jina akiitwa Lorna Silva, huyu alikuwa ni dada yake na rafiki mpenzi wa John Kitime akiitwa John Silva ambaye walikuwa wakicharaza magitaa pamoja hata siku ya Graduation day ya Form IV walipomaliza secondary school. Nikampenda kweli binti huyo bila yeye kujua, bali nikaishia kuzungumza kiingereza tu na yeye mambo ya kawaida. Mimi upande wangu nilikuwa bwege kweli maana nilishidwa kabisa kusema chochote nikabaki nameza mate tu hadi leo hii na sasa zimebaki memories tu kama hizo zako kasoro viboko. hakika siku hizo kweli zilikuwa tamu”.

Yahaya Shaaban alikuwa mkazi wa katikati ya mji wa Iringa. Nyumba ya baba yake ipo pale ilipo stendi ndogo ya daladala. Pale kulikuwa na kibanda cha bomba la maji ambayo yalikuwa yakiuzwa senti 1 kwa debe moja. Yeye alituma ujumbe huu kuhusu utengenezaji wa manati enzi zake za utoto pale Iringa. “Manati John yana ufundi wake katika kutengeneza, kwanza mpira usiwe “lupu”, halafu kuna miti maalum ya kutengenezea kipago!. Ufundi na umakini wa kukata “vinyutilo” na ufungaji wake wacha mchezo Manati kwa kokoto au “mburungwa”! Sio mchezo kakaa!

Mwenzetu mmoja ambaye sikupata jina alikuwa na haya ya kuongelea kuhusu Iringa, “Umenikumbusha sana historia hii. Napata kurejesha kumbukumbu na picha halisi za mji wa Iringa. Mimi nilikuwa mwenyeji wa Tosamaganga mwanafunzi wa primary baadaye Sekondari, tulikuwa tukija mjini kwa miguu siku za weekend. Tukirudi jioni tulikuwa tukibeba bagia, sukari-gulu na matunda ya mjini. Baadhi ya walimu uliowataja niliwafahamu kama: Mama Kalinga (Marehemu mama mdogo), Mwalimu Kalinga (mme), Mwalimu Luhanga, alikuwepo pia Mwl. Pancras(Mtelefu)nk.”
Asante sana mwenzetu wa Tosa, aka Mtelefu aliitwa Mwalimu Pancras Simbili, wanafunzi wa shule ya msingi Mlangali na shule ya msingi Mlandege katika miaka ya 70 walimfahamu vizuri sana. Hawa akina Kalinga walikuwa kadhaa kwa mfano alikuweko Mwalimu Kalinga (mama) ambaye ndie alikuwa mwalimu wa darasa la kwanza A pale Mlandege miaka 1960/61. Halafu alikuweko Mwalimu Kalinga mwingine alikuwa mwanaume alikuwa mwalimu wa Consolata, alikuwa smart sana kwa kumbukumbu zangu, nae alikuwa na adhabu moja ambayo sitaisahau nayo ilikuwa kukupa nyundo na kukwambia ujaribu kuvunja jiwe lililokuwa nje ya shule. Ilikuwa adhabu ngumu sana.


Naye Ceaser Hans Poppe alinipigia simu kuwa nimemkumbusha shule yake ya Consolata ambapo hata kaka yake Eddie alisoma hapo. Ceaser amekumbuka jinsi alivyokuwa akitamani kuwa mshika kifimbo katika bendi, sasa tatizo likawa ufupi wake hivyo kila akitaka kuzungusha fimbo ilikuwa ikikita chini kutokana na alivyokuwa mfupi wakati huo. Lakini hatimae alirefuka na kuweza kutimiza ndoto yake ya kuwa mshika kifimbo. Ukoo wa Hans Poppe ulianzishwa na babu yao Capt Max Poppe ambaye alikuwa askari katika jeshi la Mjerumani. Mjerumani huyu Capt Poppe, ambaye kabla ya kuingia Tanganyika, alipitia India na China, alipigana vita ya kwanza ya dunia katika sehemu mbalimbali za kusini mwa Tanganyika na hata kufika Msumbiji ambako alijeruhiwa vibaya katika mapigano yaliyofanyika Lioma Msumbiji. Hatimae alirudi Iringa na kuja kuanza familia yake. Kama ilivyokuwa kwa askari wenye vyeo wakati huo nyumba zao zilikuwa karibu na ofisi za utawala wa jeshi hilo, ambazo zilikuwa eneo kilipo kituo kikuu cha polisi kwa sasa. Nyuma ya jengo la kituo cha polisi kuna jengo la zamani la polisi, wakati wa wajerumani hapo ndio palikuwa makao makuu ya jeshi. Hivyo babu yake Ceaser nyumba yao ilikuwa nyumba ambayo baadae ilikuwa ikijulikana kwa jina la Omari Store. Na nyumba zote zilizokuwa zikiangalia polisi zilikuwa hasa za viongozi wa askari wa jeshi la Wajerumani. Sehemu lilipo soko lililo upande wa Mochwari ilikuwa sehemu ya kufanyia paredi askari wa enzi hizo, baadae ndio ilikuwa stendi ya mabasi ya kwanza kubwa kwa Iringa kabla ya kuhamishiwa pale ilipo sasa. Barabara kuu enzi za Mjerumani ilikuwa ni ile inayotoka polisi kupitia Uhindini, na na kunyyosha moja kwa moja na kuibukia jirani na round about ya kuingia Iringa mjini. Nigusie jambo moja, jeshi la Mjerumani lilikuwa na askari wengi Waafrika waliotoka sehemu mbalimbali za nchi na hata nje ya nchi. Kulikuwa na Wanyamwezi, Wanubi, Wamanyema, Wazaramo na kadhalika, hawa wengine walihamia Iringa na familia zao, ndio maana kuna Wahehe wa koo kama za akina Sakarani, Mrusali, Kibasila, Nzowa na kadhalika majina ambayo asili yao si Uheheni, siku moja tufika huko katika mwendelezo wa makala hizi……ITAENDELEEEEEEAAA
Categories: Iringa, Uncategorized
Simulizi nzuri Sana Mkuu John kitime.Hasa unafanya vyema kukumbuka utotoni wako.
LikeLike
Simulizi nzuri Sana Mkuu John kitime.Hasa unafanya vyema kukumbuka utotoni wako.
LikeLike
Njaribu kadri ntakavyoweza mzee
LikeLike