Mapema mwaka 1966 baba aliamua turudi tena Iringa. Alituambia amekwisha pata nyumba hivyo familia nzima tukajazana kwenye gari yake, wakati huu alikuwa na Renault Roho, tukafanya safari ya kurudi Iringa. Tuliingia Iringa kama saa 5 usiku. Nyumba ambayo tulikuwa tuishi ilikuwa kwenye mitaa kama ileile ambayo tumeliiacha Mbeya, ilikuwa sehemu ambayo asilimia kubwa ya wakazi ni Wahindi. Maeneo sasa yanayopakana na shule ya sekondari ya Lugalo. Tuliambiwa funguo za nyumba tunayohamia zitakuwa nyumba ya pili, tulipofika tukagonga nyumba hiyo akatoka bibi mmjoa mzee sana wa Kihindi, akasema funguo anazo lakini hawezi kutoa kwani haamini kama sisi ndio tunaohamia pale. Ilikuwa mara ya kwanza maishani kuonja kubaguliwa kwa kuwa tu ni Waswahili. Tulilala nje, wakati huo mdogo wangu wa mwisho akiwa na miezi michache tu kwani alizaliwa Mbeya Baptist Hospital tarehe 20 Desemba 1965. Hata ilipofika asubuhi yule bibi ambae baadae tulikuwa tukimuita tu ‘Mama mzee’, bado aligoma kutoa funguo alidai tukihamia pale tutachafua nyumba!!!. Hatimae mwenye nyumba aliyekuwa Mhindi mwenzie akaja kutupatia funguo kama saa tano hivi. Mama Mzee alipata tabu sana kwetu maana alikuwa na kinyongo wakati sie na utoto wetu hatuna habari, basi alikuwa akipiga kelele kila siku, alilalamika mara tuna piga kelele mno, mara tunavunja ukuta, mara hili mara lile mradi visa tu lakini hakutusumbua akili kwa namna yoyote ile, ila tulimsumbua zaidi kwa kumuibia makomamanga yake tu kila yakiiva.


Kushoto Typewriter, kulia Ford Anglia
Tulikuwa familia mbili tu za Kiafrika sehemu zile, familia nyingine ilikuwa ya Mzee Anselm Mkwawa. Alikuwa na watoto watatu, Richard, Charles na Joseph. Mimi na Richard tulikuwa umri sawa haraka sana tukawa marafiki, pia tulikuwa mabinamu, na mama yake Richard alisoma na mama yangu Tosamaganga, basi nikapata mwenyeji mapema. Richard ndio akanionyesha shule ya Aga Khan Primary ambayo ndiyo nilikuwa nijiunge baada ya muda mfupi na pia mama yangu alikuwa anajiunga kama mwalimu shule hiyohiyo.
Richard nilimuona mjanja sana kwani alikuwa anaweza kuendesha gari, na baba yake alikuwa akimruhusu kuzunguka nalo barabara za maeneo yetu, wakati huo Richard alikuwa na miaka 11 tu. Basi alikuwa akiingia kwenye gari lao Ford Anglia, kisha kuwasha na kuzunguka kwenye mitaa nilimuonea wivu sana, baba yangu pia alikuwa keshanifundisha kuendesha gari toka tuko Mbeya lakini ilikuwa lazima awepo ndio napata nafasi kuendesha, mwenzangu alikuwa akizunguka peke yake japo hakuruhusiwa kuingia barabara kubwa. Kitu kingine kikubwa ni kuwa akina Richard walikuwa na typewriter. Ni kama siku hizi kuwa na laptop. Pia chombo hicho muhimu alikuwa anajua kukitumia,akaandika jina langu,basi kile kikaratasi nilikitunza sana. Na kwa kweli niliiiona typewriter kwa mara ya kwanza kwa akina Richard. Muda mfupi baada ya sisi kufika Iringa akina Richard wakahama. Baba yake alikuwa mtumishi wa serikali tukaachana, mtaani nikabaki na Wahindi. Richard alikuja kuwa mwanajeshi mwenye cheo kikubwa, Charles pia alikuja jiunga na National Service na kupanda vyeo , Joseph ni mfamasia.

Shule inayoitwa Lugalo sekondari kwa sasa, ilikuwa shule mbili 1966. Kulikuwa na Aga Khan Primary School na Aga Khana Secondary School, kwa hiyo ilikuwa mkusanyiko mkubwa wa wanafunzi kuliko ilivyokuwa Mbeya ambapo kulikuwa na shule ya msingi tu. Nilijiunga shule ya msingi, kama ilivyokuwa ile ya Mbeya shule ilikuwa safi,na zaidi ya hapo ilikuwa imepambwa na maua mbalimbali ya aina ya Rose. Kulikuwa na mawaridi meupe, mekundu, njano na kadhalika, mbele pakiwa na majani mafupi mazuri ya kijani. Kulikuwa na mtu maalumu wa kutunza mimea hii. Mwalimu Mkuu alikuwa Mr Thakore ambaye baadae alichangia sana katika uchumi wa mji wa Iringa na Tanzania kwa ujumla. Nyumba ya kwanza kutoka shule ilikuwa nyumba ya daktari wa hospitali ya Aga Khan, kisha ikaja nyumba ya ‘Mama Mzee’, halafu ikaja nyumba tuliyopanga. Miaka michache baadae wazazi wangu wakainunua nyumba hiyo iliyokuwa ya daktari na mpaka leo ndio nyumba ya familia. Nyumba iliyofuata na ndio ilikuwa ya mwisho katika mtaa upande ule ilikuwa nyumba ya Mhasibu mmoja aliyeitwa Kabir, tulikuwa tukimuita daima Baba Adil. Mwanae wa kwanza aliitwa Adil, wa pili Aluba na watatu Salima. Kabir alikuwa anajua kupiga gitaa hivyo siku nyingine alikuwa akija kwetu kupiga magitaa na baba yangu, na Salima akiwa mdogo alikuwa akiweza kuimba wimbo wa Kihindi wa Kabhie khabie, baba yake alikuwa anaona sifa sina sana kumpandisha kwenye meza aimbe wimbo huo. Mama Adil alikuwa rafiki mkubwa wa mama, ujirani ulisaidia na pia huyu Aluba aliyekuwa na matatizo kidogo ya akili alikuwa anapenda kula kwetu, mama yake alikuwa kila mara analalamika ‘ Hii toto yangu napenda chakula ya kiafrika, jumbani hataki kula’.
Upande wa pili wa barabara nyumba ya kwanza ilikuwa ya Shariff Jamal , muhindi alikuwa akiendesha mashine kubwa za kusaga na kukoboa unga kule Mlandege, alikuwa na mbwa wengi na wakali, siku moja nyuki walikuja na kuwashambulia wale mbwa, mmoja akafa na yule mwingine ukali wote ukaisha, tulifurahi maana ilikuwa wabawafungulia mbwa wale saa moja jioni, hivyo ilikuwa lazima tuhakikishe saa moja tuko nyumbani. Kwa sasa katika mtaa huo nyumba ya kwanza ni Bhesania. Nyuma ya nyumba ya Shariff Jamal kulikuwa na njia panda, ulielekea barabara la kushoto, nyumba ya kwanza ilikuwa ya Mzee Kamrudin Pir Mohamad Anand. Mzee huyu ndie aliyekuwa akiendesha Green Hotel, hoteli iliyokuwa jirani kabisa na Jamatini,nadhani ni hoteli pekee iliyokuwa mtaa huo wa Uhindini. Mzee Kamru kama tulivyozoea kumuita alikuwa na mke mnene sana alikuwa akikalia kochi hata jikoni wakati ana pika ila alikuwa mpishi mzuri sana yule mama. Alikuwa akijitahidi sana anaweza kutembea mpaka nyumbani kwetu kiasi cha mita mia moja tu lakini alikuwa akilalamika njia nzima. walikuwa na watoto wengi sana. Walikuwa na kaka yao ambaye nimemsahau jina ambaye alikuwa akisoma Iyunga, akawa na urafiki wa kimapenzi na mwalimu wake wa kike, bahati mbaya siku moja wakiwa matembezini na gari wakapata ajali yule mwalimu akafariki, kijana akasimamishwa shule ila akarithi kammbwa kazuri keupe kalikuwa kakiitwa Fifi. Tulikuwa tukimuona mtu wa ajabu alikuwaje mpenzi wa mwalimu. Paia walikuwa na dada yao mkubwa, kisha wakaja watoto ambao nilisoma nao na kucheza nao. Alikuweko Mahmud, huyu alikuwa bonge lakini kazi yake kulia kila wakati, akichokozwa alikuwa akienda kushtaki kwa mdogo wake aliyeitwa Moez. Moez alikuwa yule mtoto mkorofi wa familia, mgomvi mcheza korokoro, Wahindi wenzie walimuogopa sana. Baba yao alikuwa mkali sana na alikuwa akitandika viboko kama waalimu Consolata, lakini haikumkomesha Moez. Moez ndie mtu wa kwanza mimi kutwangana ngumi rasmi. Aliwachokoza wasichana fulani waKishelisheli wakaja kunishtakia nimpige, sasa si unajua tena mwanaume ukishawekwa kona ile lazima ujitose. Stori hiyo baadae kidogo. Ila Moez pia alikuwa rafiki yangu mkubwa pale mtaani, nyuma ya nyumba zetu na shule ya Lugalo kulikuwa pori tu, mimi na Moez tulikuwa tukijua kila mti wa matunda uko sehemu gani, mitoo, misasati, migola na kadhalika. Mdogo aliyemfuata Moez alikuwa msichana Leila na mdogo wao wa mwisho alikuwa Iqbal, huyu nae alikuwa kama kaka yake Moez, muda mwingi yuko Uswahilini, alikuja kufariki kutokana na kinywaji cha Brandy aliyodaiwa alikunywa kutoka kwenye bar moja. Watu kadhaa walifariki kutokana na kunywa pombe aina hiyo kipindi hicho lakini hiyo ni hadithi ya miaka mingi baadae, ntaifikia. Mbele ya nyumba ya akina Moez kulikuwa na akina Dharamsi, hawa walikuja kuwa maarufu baada ya baba yao kuandika mbele ya gari lake, ‘Lofa huyo anakuja’ na nyuma akaandika ‘Lofa huyo anakwenda’. Jirani na nyumba hiyo baadae walikuja kuhamia Singasinga fulani kutoka Nairobi, baba yao akikuwa akiitwa Mota Singh Sethi, watoto walikuwa Manjit, Harbinder, Parvinder na dada yao. Huyu Harbinder ndie ambaye yupo mahabusu kwa kesi ya IPTL. Mwisho wa barabara hii inapokutana na barabara ya lami ilikuwa nyumba ya mwalimu mkuu wa sekondari ya Aga Khan, katika kipindi hiki mwalimu Mkuu wa sekondari ya Aga Khan alikuwa mwalimu Sheikh, aliyekuja kuwa mwalimu mkuu mwanzilishi wa Highlands Secondary School. Upande wa pili nyumba inayoangaliana na kituo cha bus cha Sabasaba ilikuwa nyumba ya mwalimu wa darasa langu, Mrs Saleh , mumewe alikuwa akifanya kazi Baclays Bank. Mrs Saleh alikuja kuwa maaarufu kutokana na mgahawa wake wa Hasty Tasty. Ukirudi tena kwenye njia panda jirani na kwa akina Jamal na kuelekea barabara inayopanda juu, kwa wakati huo baada ya nyumba ya Kabir kulikuwa na nyumba moja tu iliyokuweko baada ya nyumba ya akina Staki. Nyumba hiyo aliishi Mr Hassan mwalimu wa Jiografia wa Aga Khan Primary. Baada ya nyumba hiyo palikuwa na korongo kubwa ambalo ukivuka unakuta nyumba nyingine zilizokuwa zikifanana na za kwetu. Huko alikuweko mzee Manji ambaye alimuoa pacha wa mke wa Mzee Kamru nae alikuwa mnene vile vile japo yeye kidogo alikuwa afadhali. Mzee Kamru alikuja kuishi na Mama Asnati baada ya mkewe kufariki, na mama huyu alikuwa akiuza pale hotelini kwa miaka kadhaa.
Mtaa wetu ulikuwa mtaa kimya sana kwanza kwa sababu kulikuwa na mbwa wakali kila nyumba, ilikuwa hata mwenyeji huwezi kutembea kwa miguu baada ya saa kumi na mbili jioni. Pili kulikuwa na uhusiano mdogo sana na Kihesa kwani baada ya shule lilikuwa pori lenye njia nyembamba ya miguu kwenda Kihesa. Na si mara moja wanyama kama nyati walifika mpaka maeneo ya shule. Digidigi na sungura walikuwa wanyama wa kawaida sana maeneo yetu. Baada ya kuvuka uwanja wa shule ya sekondari, lilikuweko tuta ambalo askari wa Field Force walikuwa wakifanya mazoezi ya kulenga shabaha, ndio maana shule ya msingi Aga Khan ilikuja kuitwa shule ya msingi Shabaha, hawa Field Force Unit walikuwa na majina mengi, FFU, Motolaizi, Fanya Fujo Uone……………ITAENDELEEEEEA
Categories: Iringa