
Hatimae nikaanza shule pale Aga Khan, kama ilivyokuwa Aga Khan Mbeya shule hii nayo ilikuwa English medium . Sare za shule zilikuwa tofauti na shule nyingine, kaptura ilikuwa rangi ya kijivu shati jeupe. Haya mashati tuliyavaa kwa kuangalia label, zile alama kwenye kola. Wakati nasoma Consolata ilikuwa sifa sana kuvaa shati la label ya Gossage, kufika huku Aga Khan kukawa na shati za label ya Embassy, sifa ya mashati ya nembo hizi ilikuwa mashati haya ni meupe zaidi na ukipiga pasi upanga unadumu. Kulikuweko pia mashati ya Shikibo ambayo nayo wanafunzi tuliyapenda sanamiaka hiyo.
Kulikuwa na ushindani wa usafi. Katika hizi shule za Aga Khan hakukuwepo utaratibu wa ukaguzi, asubuhi tulipanga mstari, tukaanza na sala kwa mujibu wa ki Ismailia, kisha wimbo wa Taifa kama hakuna matangazo tuliingia darasani. Darasa letu lilikuwa na Waafrika kadhaa namkumbuka Hamisi Maganga ambaye miaka mingi baadae nilimkuta akiwa Katibu Tarafa sehemu moja kati ya Mikumi na Ifakara. Alikuweko Kisyeri Chambiri, yeye na kaka yake Chacha ndio walikuwa Waswahili peke yao waliokuwa wakiishi katika hosteli za Aga Khan. Nakumbuka kuambiwa kuwa baba yao alikuwa mkuu wa wilaya huko Tarime. Kisyeri alikuwa na akili sana, darasani alikuwa akichuana na binti ya mwalimu mkuu. Huyu akiwa wa kwanza mwenzie wa pili. Kisyeri hatimae alikuja kuwa Mbunge. Kama ilivyokuwa sheria wakati ule, darasa letu lilikuwa na wanafunzi 45. Mwalimu wa darasa alikuwa Mrs Saleh, mama wa Hasty Tasty. Waalimu wengine walikuwa ni Mr Pabani, huyu alikuwa ndie anaonekana mkali kidogo, alikuwa na Volkswagen ya bluu. Mr Khan alikuwa mwalimu wetu wa somo la sanaa, yeye alikuwa na Volkswagen ya kijivu, alikuwa mchoraji mzuri pia alikuwa daktari flani wa wanafunzi. ukiumwa unaenda kwake anakupima na hata sindano alikuwa akichoma. Alikuwa ndie mwalimu anaeogopwa kwa viboko. Mr Khan alikuja pata mkasa ambao ingekuwa zama hizi pengine angefungwa. Ilidaiwa alimbaka mtoto mdogo aliyekwenda kwake kutibiwa. Alifukuzwa akarudi kwao India. Mr Hassan, huyu alikuwa na Ford Anglia nyeusi, alikuwa mwalimu wa Jiografia, kupitia kwake tulijifunza kuhusu reli la kutoka China mpaka Vladivostok Urusi, aliweza kutufundisha tukawa tunajiona kama tuko Urusi ndani ya treni tunapita miji mbalimbali. Alikuweko Mr Daya huyu alikuwa ndie comrade wa wanafunzi, nadhani kwa kuwa alikuwa mwanamichezo pia. Alikuwa na gari lake Zephry ya rangi ya bahari. Baba yake Mr Daya alikuwa maarufu sana kwa Wahehe. Duka lake siku ya Jumapili lilijaa sana maana ilikuwa ukifika kwake kila atakachokutajia bei ukibisha tu anakuuliza “Ndumule?”. yaani ‘nichinje?’ akiwa na maana apunguze bei? Na kwa sababu hiyo akajulikana kwa jina la Ndumule. Wazazi walikuwa akitutuma tukanunue daftari, nguo na vifaa vingine vya shule kwa Ndumule.

Masomo yalianza saa 2 na ilipofika saa 4 tulipumzika kidogo, hii tuliita resses, kule Consolata tuliita ‘pausi’, nadhani ilitokana na neno la Kiingereza ‘pause’. Katika shule hizi za Aga Khan wanafunzi wa Kihindi walikuwa wakifungiwa vyakula na wazazi wao, ambavyo walikula wakati wa recess. Saa nne ile ungeona marafiki wanakusanyika kwa vikundi kuchangia chakula chao na kula pamoja. Wengine walikuwa wakienda nyumbani kwa mkuu wa shule Mrs Thakore, yeye alikuwa na kaduka kadogo ambako alikuwa akiuza soda, keki, na vitafunwa mbalimbali vya kihindi kama chana-bateta, cheuro, pia karanga na bisi. Wengine tuliendelea na michezo ya saa 4 kama kawaida.
Kwa kuwa shule ya sekondari na shule ya msingi vilikuwa pamoja kulikuwa na wanafunzi wengi sana nje muda huo. Mbele ya shule hizi mbili kulikuwa na viwanja tosha vya michezo vilivyotumika kwa shule zote mbili, japokuwa si kila wakati mambo yalikuwa salama. Mwaka mmoja baada ya mashindano ya mchezo wa hockey kati ya shule hizi mbili, kulianza uhasama mkubwa na kulikuwa na vita ya magongo ya hockey kati ya wachezaji wa sekondari na wale wa shule ya msingi, vita hii iliendelea kama siku mbili hivi, akikutwa mchezaji kutoka huku ilikuwa ni kumtwanga kwa magongo, ililazimika uongozi wa shule hizi mbili uingilie kati. Kulikuwa na kiwanja cha mpira wa miguu ambacho kilizungushwa tracks za kukimbia, kulikuwa na uwanja wa hockey ambao katikati yake kulikuwa nasehemu ya kucheza mchezo wa Cricket, kulikuwa na uwanja wa basket ball, netball na volleyball. Ilikuweko sehemu iliyotengenezwa maalumu kwa michezo ya high jump na pole vault. Viwanja hivyo vilikuwa mbele ya shule. Nyuma ya shule kulikuwa ndio sehemu ya assembly, huko ndiko tulijipanga asubuhi kabla ya kuingia madarasani kwa ajili ya sala na wimbo wa Taifa. Sehemu ambayo sasa ni ukumbi ilikuwa shamba la matunda mbalimbali.
Tuliingia darasani na kila mtu alikuwa na kiti chake na desk lake ambalo lilikuwa na sehemu ya kuweka vitabu na daftari zake. Wanafunzi wengi waliletwa shuleni na magari ya wazazi wao, saa sita walikuja kuchukuliwa kwa ajili ya chakula cha mchana. Wazazi wengine walikuwa na pickups kwa hiyo wanafunzi wenginebwaliweza kurudi nyumbani kwa vikundi.

Kuna kituko kimoja cha ajabu kilitokea siku moja katika hizi safari za mchana. Magazeti ya picha yaliyokuwa yakiitwa Film yalikuwa maarufu sana, na humo kulikuwa na steringi anaitwa Lance Spearman. Kwenye hadithi humo Spearman alikuwa akionekana akiruka kutoka kwenye magari yaliyokuwa yakitembea na kufika chini bila kuumia. Watoto fulani wa kihindi wakiwa kwenye pickup moja walianzisha ubishi kuwa zile zilikuwa trick tu za picha, kijana mmoja aliyeiltwa Jolly akadai inawezekana na yeye atawaonyesha. Na kweli alipofika karibu na kituo kimoja cha mafuta kilichoitwa Esso akajirusha na kuangukia uso, alikuwa kwenye Coma kwa muda wa wiki moja hospitalini, lakini alipona japo alikuwa na kovu kubwa usoni baada ya hapo….ITAENDELEAAA
Categories: Iringa, Uncategorized