LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 23


Shilingi kumi 1964

Mwaka 1966 ada ya shule za serikali ilikuwa shilingi 10 kwa mwezi, inaweza kuonekana kichekesho kwa leo lakini fedha hii ilikuwa kubwa na kuna watu walishindwa kuendelea na masomo kwa kukosa ada hiyo. Ada ya Aga Khan Primary School ilikuwa shilingi 12/- Kulikuwa na tofauti kubwa kati ya huduma katika shule hii na shule nyingine nyingi. Wanafunzi tulikuwa na malezi ya ‘Kihindi’, tulikuwa hatufanyi kazi hata zile ndogo ambazo ni kawaida kabisa katika shule nyingine. Kwa mfano usafi wa shule na madarasa ulikuwa ukifanywa na watu walioajiriwa, ukikuta mwanafunzi anafagia ujue huyo kapewa adhabu. Hayakuwa mazingira mazuri kwa malezi ya mtoto wa Kiafrika kwa kweli. Kulikuwa na mambo mengi mazuri pia kwa mfano, darasani kulikuwa na madeski ya kutosha, vitabu vilikuwa vya kutosha vya karibu kila somo. Kulikuwa na spika kila darasa, mwalimu mkuu akitaka kuongea na wanafunzi alikuwa akiongea nao akiwa ofisini kwake, na spika hizo zilitumika katika vipindi vya redio vilivyokuwa vikirushwa na RTD. Kati ya kipindi nilikipenda ni kile cgha kujifunza kiingereza kilichoitwa ‘ A thousand miles to Tanga’. Shule ilikuwa na maktaba kubwa na kulikuwa na ratiba ya kila wiki ya darasa kuingia maktaba, kila mwanafunzi alilazimika kumaliza idadi fulani ya vitabu kila mwezi,na hii ilikuwa njia mojawapo ya kuwa ‘Best Student’ wa mwezi. Iringa ilipata maktaba ya serikalimwaka 1963/4, makataba ambayo ipo jirani na jengo la Bima ya Taifa. Wanafunzi tulikuwa tukijazana pale kutumia makataba hii, na kwa kweli tuliendelea kuitumia kwa miaka mingi sana. Mwaka jana nilijitolea vitabu kadhaa kuendeleza maktaba yetu iliyonilea. Maktaba hii ilikuwa pia sehemu muhimu kwa wapenzi walioko kwenye mashule kukutana, kwa kisingizio cha kuwa wameenda kujisomea. Nakumbuka tulianzisha makataba yetu mtaani kwetu. Mzee Lofa huyo anakuja alimjengea mwanae, Alnasir, banda la bati sisi tukachanga vitabu na macomic na tukawa tunajiazima wenyewe, ilikuwa ukiingia ndani ya lile banda hakuna ruksa kupiga kelel maana watu wanasoma dah vichekesho vitupu.
Kulikuwa na mkutubi mmoja pale Iringa ambaye baadae alikuja kuwa mtunzi mzuri wa vitabu vya hadithi, kimoja wapo kikieleza kuhusu ujambazi uliofanyika Ipogolo, tulikipenda kitabu hicho maana tulikuwa tukiona kama ni wahusika katika hadithi ile. Nyuma ya makataba ilikuwa ndio mwisho wa uwanja wa gofu ambao kwa upande wa pili uliishia jirani na shule ya Wilolesi. Eneo lote lile lilikuwa mali ya Iringa Club. Kwa sasa kuna ofisi mbalimbali za Mkoa na Chuo Kikuu.

Wanafunzi wa Aga Khan wakicheza ngoma mwaka 1967


Nilieleza hapo nyuma kuwa wakati wa mapumziko, wanafunzi wa Kihindi walikuwa wakikusanyika na kula pamoja chakula walichofungiwa, hali hii ilikuwa ikibadilika zikikaribia sikukuu za serikali, ghafla waswahili tulikuwa tukikaribishwa kushiriki mlo huo. Kulikuwa na sababu kubwa. Shule za ‘private’ na wazazi wao walikuwa wavivu sana kushiriki siku za Kitaifa, mara nyingi yakipita maandamano walikuwa wakichungulia madirishani au magorofani, kwa kuwa zilikuwa enzi za Chama kimoja kilichoongoza serikali, amri ikatoka kila mtu ashiriki maandamano, na kama hashiriki basi asigeuze wenzie sinema. Shule yetu nayo ikaanza kushiriki maandamano, hatukuwa na bendi hvyo tukawa tunaenda kibubu bubu, na pia shuleni hatukuwa na tartibu za paredi basi watu walienda kihobelahobela. Kulikuwa na shida kubwa kwa watoto wa Kihindi wakishakutana na watoto wa Kiswahili, mabinti walivutwa nywele, masingasinga walivuliwa vilemba, wavulana walichokozwa tu na hata kunyang’anywa chochote walichokuwa nacho hasa pesa. Basi ilikuwa ni uonezi mkubwa. Sasa ndicho kikawa chanzo cha kukaribishwa ule mlo wa saa nne. Hapo utaulizwa ‘John, if vi eat together you vill be my friend in mandomando no?’ Kwa hiyo siku za maandamano Waswahili tukawa na ajira ya ubodigadi, wengine walilipwa chakula wengine pesa basi ndo siku zikaenda. Kadri siku zilivyoenda shule ikalazimika kuingia katika taratibu za shule nyingine. Walikuja jamaa kutoka Zanzibar kuja kutufundisha ‘goose’ march. Hilo lilikuwa parade la Kimapinduzi. Amri zilikuwa za Kiswahili tofauti na tulivyozoea paredi kuwa na amri za Kiingereza mfano. Attention, Left turn, Right turn at ease. Katika paredi mpya tukaanza kufundishwa, kushotoz geuka, kuliaz geuka, mbelez tembea, na mwiliz legeza. Sina haja ya kukwambia vituko vya watoto wa shule hii kujaribu kuwatembeza kiparedi, hapo ndio ungeshangaa mguu wa kushoto na mkono wake vyote vinaenda pamoja badala ya kupishana. Shule ikalazika kuanzisha kundi la kwaya na kundi la ngoma kushiriki sherehe za kitaifa. Ni burudani kuona mtoto wa Kihindi akijaribu kukata viuno vya Kimakonde

Categories: Iringa, Uncategorized

Leave a comment