LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 27


Highland cinema
Tivoli/Paradise Cinema

Moja ya burudani muhimu katika maisha yetu wanafunzi wa Aga Khan Primary miaka ya 66 na 67 ilikuwa ni kwenda sinema. Kulikuwa na kumbi mbili za sinema, Highland cinema na ukumbi wa pili ambao uliwahi kubadilika jina kutokana na kuwa katika umiliki tofauti, uliwahi kuitwa Tivoli Cinema na baadae Paradise Cinema. Katika kumbi hizi kulikuwa na sinema za Kiingereza na Kihindi na kulikuwa na watemi mbalimbali katika sinema hizo na katika utoto wetu tulijidai kuwafuatilia sana. Kwa vile nilikuwa shule ya Wahindi sinema nyingi za kihindi hazikunipita niliwafahamu waigizaji wengi maarufu kama Asha Parekh, Dilip Kumar, Sunil Dutt, Joy Mukerjee, Dev Anad, Shashi Kapoor, Shami Kapoor na kadhalika. Kama nilivyokuambia tulikuwa tukiishi jirani na watoto wa Mzee Kamrudin Anand, nakumbuka mwanae Moez Anand aliwahi kujaribu kunambia kuwa yeye na muigizaji Dev Anand ni ndugu, ilikuwa fiksi tu kwa lugha ya siku hizi. Katika filamu za Kiingereza kulikuwa na sinema za ma cowboy, maarufu kama Westerns. Huku nako kulikuwa moto, waigizaji wake maarufu walikuwa wakina Gulliano Gema, Clint Eastwood, Lee Van Cleef, Eli Wallach, Franco Nero, , Klaus Kinski, Yul Bryner (kipara), Terence Hill na mwenzie Bud Spencer, Robert Woods wa My name is Pecos ni kati ya orodha ndefu ya waigizaji wa sinema hizi. Filamu hii ya My name is Pecos ndio ilikuja fanya jina la suruali zilizokuwa pana chini kuitwa pekosi. Nia aina ya suruali aliyovaa huyu Pecos kwenye filamu zake
Simena za wanamuziki akina Elvis Presley nazo zilikuwa filamu muhimu kutozikosa, tulikuwa tukifwata muziki na vituko vya huyu jamaa aliyekuwa handsome sana na mtu wa totoz sana. Katika mlolongo huu huwezi kuacha filamu za James Bond, star wake alikuwa Sean Connery. Umaarufu wa filamu za James Bond na namba yake ya utanmbulisho 007, ilifanya vijana dunia nzima kutaka kuwa na bidhaa yenye alama ya 007, kulikuwa na pete, bangili, saa mikanda ya suruali, chupi za kiume, na kwa wakati huo wajanja wote walikuwa na moja ya vitu hivi.


Matangazo ya filamu yalikuwa yakiandikwa kwa usanii mkubwa sana kwenye magunia yaliyopakwa chokaa nyeupe kisha kuandikwa kwa ufundi maandishi makubwa ya rangi ya bluu yakielezea ukumbi na filamu husika, pia kama filamu hiyo inafaa kuangaliwa na kila mtu au ya watu wazima tu. Kwa kuweka tarakimu U, filamu hiyo ilikuwa ruksa kuangalia watu wote, alama A, ilikuwa ina maana lazima mlezi ahusike wakati wa kuangalia filamu hiyo, mara nyingine ukija na mtoto mdogo mno kwenye filamu, uongozi ulikataa kuruhusu mtoto kuingia. Na kwa filamu zenye alama ya X, watu wazima tu waliruhusiwa. Mabango ya matangazo yaliwekwa sehemu mbalimbali za mji. Kiingilio cha filamu kilitegemea umekaa sehemu gani katika ukumbi, mbele karibu na ‘screen’ kulikuwa na viti vya mbao na hivyo bei kuwa ndogo, na nyuma kabisa viti vya sponji na bei ilikuwa juu zaidi. Pia kulikuwa na bei tofauti kati ya wakubwa na watoto. Watoto wadogo sana waliingia bure kabisa. Tulikuweko sisi wengine ambao tulikuwa tunatumia njia iliyoitwa mkuki. Ilikuwa hivi, kila sinema ilipokuwa ikionyeshwa, kulikuwa na muda wa mapumziko na kama ni filamu ndefu sana kulikuwa na mapumziko mara mbili. Wakati huu wa mapumziko watu walitoka nje kununua vitafunwa na soda. Baada ya dakika chache kengele ililia kuashiria kuanza sehemu ya pili ya filamu, hapo ndipo tusio na fedha ya kiingilio tulikuwa tunajichanganya na wanaoingia, mkononi ukiwa tumeshika soda au bisi na kudai tulitoka kwa kununua vitafunwa. Mara nyingine ilikuwa kwa makubaliano na mlinzi wa mlangoni tu, unampa sigara au pesa kidogo unaingia ‘mkuki’.
Filamu ambazo zilikuwa na wahudhuriaji wengi zilikuwa zikiongezwa ratiba, ilikuwa filamu inaweza ikaonyeshwa Jumapili saa nne asubuhi, ikarudiwa saa nane mchana na kisha kuonyeshwa tena katika ratiba za kawaida za saa 12 na saa 3 usiku. Kwa kawaida kila siku kulikuwa na filamu inaonyeshwa katika kumbi hizi, ratiba ya kawaida ilikuwa ni kuonyesha filamu saa 12 jioni na saa 3 usiku…….itaendeleeeeea


Categories: Iringa, Uncategorized

Leave a comment