LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 33


Luza Elyas John

Shule ya St Mary’s Primary School ilikuwa shule maarufu hasa kwa watoto wa Kihesa na kuelekea upande wa Nduli. Na shule hii pia ndio ilikuwa chanzo cha shule ya sekondari ya wasichana, Iringa Girls. Kabla ya hapo watoto ambao walitaka kusoma shule za misheni walilazimika kusoma shule ya Consolata iliyokuwa pembeni ya kanisa Katoliki la Mshindo, shule ambayo baada ya kutaifishwa iliitwa Chemchem. Wakati nasoma Chemchem tulikuwa na wenzetu wengine ambao walikuwa wakitoka Kihesa, Mgongo na hata vijiji karibu na Nduli. Hata nyakati hizo tulikuwa tukiwashangaa kuhusu uwezo wao wa kuwahi shule tena kabla sisi tuliokuwa jirani na shule hatujafika.
Baada ya misheni ya Kihesa kuanza pamoja na kujenga kanisa pia ikaweka zahanati, na baadae shule ya msingi ya St Mary na pia kulikuweko na shule ya chekechekea. Nyakati hizo shule za chekechekea zilikuwa zinaitwa shule za vidudu. Kwa hiyo ilikuwa ukimaliza shule ya vidudu pale kwa sista unahamia St Mary kuanza darasa la kwanza. Ilikuwa shule nzuri sana.
Kama ambavyo nilihadithia katika mlolongo wa makala hizi huko nyuma, eneo lilifuata baada ya kumaliza uwanja wa michezo wa shule ya Lugalo, lilikuwa ni eneo la kufanyia mazoezi ya kulenga shabaha askari wa FFU, wakati tulikuwa watoto tulikuwa tukienda huko kuokota maganda ya risasi. Na ni kwa sababu ya eneo hili, shule ya Aga Khan Primary ilipotaifishwa ikapewa jina la shule ya msingi ya Shabaha. Kutoka hapo hakukuwa na nyumba yoyote ya wenyeji mpaka Kihesa. Katikati kulikuwa na shule moja ya vidudu, na jirani yake kulikuwa na hostel iliyojulikana zaidi kuwa ni za Padri Balbanti, wanafunzi kadhaa wengine waliokuwa wakisoma Aga Khan sekondari waliishi hapa. Moja wao alikuwa mwanafunzi Mbena aliyeitwa Luza Elias. Luza alikuja kuwa mwanamuziki maarufu aliyepiga saksafon katika bendi za Jamhuri Jazz Band, baadae akahamia Simba wa Nyika na hatimae akawa mwanamuziki wa Mwenge Jazz Band, kwa sasa Luza yuko Marikani akiendelea na Saksafon lake katika muziki wa Injili nchini humo .
Na kwa upande mwingine kama ungetokea kwenye njia panda ya barabara ya kuingia Lugalo na kuelekea Kihesa, pande zote mbili za barabara zilikuwa ni pori tu. Kwa upande wa kushoto kulikuwa pori mpaka ukisha fikia kituo cha FFU, na baada ya kota za FFU tena kulikuwa hakuna nyumba mpaka ukisha fika karibu na sehemu ya sokoni Kihesa. Upande wa pili wa barabara ukishatoka Kihesa kama unaelekea mjini kulikuwa na nyumba chache lakini nyumba iliyokuwa ikionekana ni ya kisasa ilikuwa ya mama mmoja aliyejulikana kwa jina la Margreth au Mama Diana. Huyu mama aliyesemekana aliwahi kuolewa na mzungu alikuwa na gari lake Volkswagen Kombi, alikuwa mmoja wa wanawake wa kwanza wa kiafrika kuendesha gari Iringa. Baada ya nyumba hiyo hakukuwa na nyumba yoyote upande huo mpaka ukisha fika eneo lililojulikana kama Kingsway Garage. Barabara hii ya kutoka Kihesa ilijulikana kama Kingsway Road. Eneo lote baada ya shule ya Kichangani, yaani eneo kilipo chuo cha Klerruu, Shule ya Highland, uwanja wa Sabasaba, na eneo lote mpaka Ruaha International, lilikuwa na miti mingi hasa mikaratusi na lilijulikana kama Forest. Ilisemekana katikati hapo kulikuwa na sehemu yenye tope jingi laini ukikanyaga unazama, kukaitwa kwenye kisima cha bi. sehemu hiyo ilikuwa pori mpaka kukawa na vibao vya kukaribisha watalii waliokuwa wakitaka kuweka matent na kulala porini, kuliitwa ‘Camping Site’. Baadae sehemu moja ikagawiwa kwa klabu ya Wahindi na kuwa Gymkhana, waklajenga kibanda kidogo cha Club na kutengeneza uwanja wa tennis.

Uwanja wa michezo wa Kleruu ulikuwa na miti kama inavyoonekana pichani


Barabara kuu ya kutoka Dodoma kuingia mjini awali ilikuwa ni ile inayopita katikati ya chuo cha Klerruu na shule ya Highland, baadae ndio ikaja barabara inayotumika sasa. Barabara hii ina sifa moja kubwa inaitwa ‘The Great North Road’. Ndio barabara iliyokuwa na sifa ya kutoka Cape Town Afrika ya Kusini mpaka Cairo Misri. (From Cape to Cairo). Kulikuwa na gari lenye freezer lilikuwa likipita kila wiki likiwa linatoka Johannesburg na kwenda Nairobi, roli hili lililokuwa na rangi ya fedha lilifahamika sana japo kwa kuwa halikuwa linasimama Iringa tukiwa watoto tulibaki kutunga hadithi mbalimbali kuhusu kilichokuwemo ndani ya gari hilo. Tulikuwa tunaamini linasafiri mpaka MIsri.
Kwenye sehemu ambapo ipo shule ya Highland kilikuwa kituo cha kumpumzika wapigania Uhuru wakati wakitoka huko Kongwa wakiwa wanaelekea kwao kupigana. Hivyo kulikuwa na siku yaliweza kuwasili maroli mengi ya watu hao, na walikaa hapo siku mbili au tatu kisha mara nyingi usiku waliondoka na kutokomea.
Jina la Kihesa lilitokana na neno la Kitaliana Chiesa maana yake Kanisa, nategemea watu wa Kihesa sasa watakuwa wanajua chanzo cha jina la eneo lao.

Kwa Mfalanyaki

Kihesa ya zama hizi
Mwibalama

KAMA UNA HADITHI AU PICHA ZA ENZI NINAYOZUNGUMZIA NA AMBAZO UNGEPENDA WATU WAKUMBUKE NITUMIE jkitime@gmail.com au utoe maoni yako katika eneo la comment chini ya habari hii.

Categories: Iringa

2 replies

  1. Umenikumbusha Chuo cha Ualimu Kleruu niliposomea kazi ya Ualimu na kile Kimji cha Kihesa. Iringa yenyewe ya wakati huo ilikuwa bora sana. Niliingia Iringa na bus la abiria la Railway. Kleruu ilikuwa kama Uzunguni kwa wakati huo. Niliikuta band ya muziki pale chuoni na haikuwa nampiga sollo ndipo nilipoanza kuipigia sollo. Habari za Iringa zimenikumbusha na kunifurahisha.

    Like

Leave a comment