Katika makala hizi si mara nyingi nimetaja wasichana, nilipokuwa mdogo wasichana walikuwa na yao na wavulana na yetu. Ila naweza kukumbuka baadhi ya mambo yenye kumbukumbu yaliyojitokeza yaliyohusu wasichana. Jambo la zamani kabisa ni kumbukumbu ya mmoja wa wasichana wa kwanza kusoma Iringa Middle School kati ya mwaka 1960 na 1961, ambaye alijinyonga kwenye pori lililokuwa nyuma ya shule hiyo. Niliambiwa kisa cha kujinyonga yule msichana ni baada ya kugundua kuwa amepata mimba. Swala la msichana kupata mimba halikuwa linachukuliwa kirahisi rahisi na hasa kwa kuwa alikuwa bado mwanafunzi, tena kati ya wasichana wa kwanza kuingia Middle School ile ambayo awali ilikuwa na wavulana tu. Nakumbuka wanafunzi wa Middle School walipita mbele ya nyumba yetu wakielekea kwenye msiba. Kwa vile kuna wasomaji wa makala hizi ambao walikuwa wanafunzi wa shule hiyo wakati huo pengine wataongeza kumbukumbu ya tukio lile lililokuwa gumzo mjini siku hizo.
Nikiwa darasa la nne shule ya msingi ya Consolata, nakumbuka mkasa wa msichana aliyepakwa upupu na wanafunzi wavulana wakati wa kukata fagio. Sehemu ambayo sasa ni Frelimo lilikuwa pori tulikuwa tukienda kukata majani ambayo iliwezekana kutengeneza fagio nzuri sana. Sijui kwa sababu gani wavulana wakampaka upupu mwili mzima msichana mmoja aliyeitwa Mage. Aliugua wiki nzima, alipopona alikuja na mzazi wake shuleni kuelezea ule mkasa ilikuwa hatari kuna watu walichapwa viboko visivyo idadi.
Nikiwa darasa la saba nikampata rafiki aliyehamia shule yetu jina lake lilikuwa Kudra, sikumbuki tulifikiaje muafaka ule, lakini tukaanza kusindikizana kutafuta dawa za mapenzi. Pale sokoni, upande wa soko ulio jirani na mochwari, wakati huo lilikuwa soko jipya, kulikuwa na watu kadhaa wanauza dawa za miti shamba, kwa kweli walikula sana thumni thumni zetu katika jitihada ya kupata dawa ya mapenzi. Kwa mfano tuliwahi nunua dawa tukaambiwa tuwe tunatafuna kidogo iliyobaki tunaacha chini ya ulimi na kuhakikishiwa kuwa tukimsalimia msichana au kumchekea tu, basi ataanza kutupenda. Lengo langu wakati ule ilikuwa msichana wa Kishelsheli alikuwa anaitwa Marlyn. Nadhani atakuwa alikuwa akinishangaa sana jinsi nilivyokuwa namfwata fwata kila kona na kumchekea bila sababu, nikiwa nafuata masharti ya mganga, sikuona mapenzi wala nini, kila tukirudi pale sokoni tukawa tuna ambiwa tumevunja masharti. Ila dawa moja tuliambiwa hiyo ni gerentii, tatizo ikatushinda masharti,tuliambiwa ili dawa ifanye kazi ni lazima tuchanjwe kwenye ulimi na hata bei yake ilikuwa juu sana we fikiria ilikuwa kuchanjwa ni shilingi mbili kila mtu, hizo shilingi nne tungepata wapi? Hatukurudi tena, labda ingefanya kazi ningeoa mtoto wa Kisherisheri nikiwa darasa la sita tu. Miaka mingi baadae nilikuja kukutana na Kudra kule Tabora alikuwa afisa mkubwa wa jeshi. Tulicheka mpaka machozi yalitutoka tulipokumbushana kipindi hiki. Niliwaona askari wengine wakituangalia na kujiuliza Afande ana siri gani na huyu mwanamuziki?
Kumbukumbu nyingine ya wasichana utotoni ni pale nilipopigana ngumio kwa mara ya kwanza shuleni. Kulikuwa na binti mwingine wa Kisherisheri anaitwa Mary ann, huyu akaja kunishtakia kuwa kuna jamaa anamchokoza, sasa kama mwanaume ililazimika niende nikamkoromee yule jamaa. Jamaa hakunisubiri niongee akanitwanga ngumi moja ya jicho na kisha kunikata ngwala ngumi zikaeisha mimi niko chini, jamaa kakimbilia darasa, yule binti na wenzie wakabaki wananiambia, ‘Sorry John Sorry’ machozi yakiwa yananilengalenga kwa aibu. Sikuwahi kupigana tena maishani.
Pale ulipo ukumbi wa sasa wa shule ya Lugalo kulikuwa na muembe mkubwa. Siku moja jioni baada ya masomo kundi la wasichan wakawa wamepanda juu ya ule mti wanaangua maembe. Rafiki yangu mmoja akaona ni fursa ya kwenda kuwachungulia wasichana, wasichana wakakasirika na kuanza kumpigia kelel aondoke mwenyewe kang’ang’ania kuangalia ‘sinema ya bure’. Hakuwa kajitayarisha kwa kilichomtokea, walitokea wasichana wengine wakamkamata na kumuangusha, waliokuwa juu ya mti wakashuka, jamaa akajikuta anashambuliwa na wasichana sita, wakawa wamemzidi nguvu wakamvua kaptura na kukimbia nayo. Ilichukua wiki kadhaa kabla jamaa hajarudi shule tena.
Baada ya kuanza masomo ya sekondari, nilianza sasa kuwaona wasichan kwa jicho jipya. Pale sekondari kulikuwa na wasichana wengi. Nakumbuka madada wakuu Rukia Masasi, Asha, kulikuwa na binti wa kihindi simkumbuki jina. Wasichana wengine walikuwa Patricia na mdogo wake Emma C, Zainabu K, Lucy, huyu aliwahi kutoroshwa na mwanaume halafu baba yake akaja na bunduki shuleni, kutishia atampiga mtu risasi. Alikuwepo Lucy, kisha katikati ya muhula akajiunga msichana mmoja mzuri sana,mwanafunzi mmoja aliyeonekana kupendwa na huyu msichana akaja kuanguka na baiskeli, zikaanza tetesi kuwa yule msichana ana mkosi. Mwenzetu mmoja wakati tuko sekondari ilisemekana alimjaza mimba mwanafunzi mwenzie msichana wa Kihindi, msichana yule alihama shule ghafla sasa sijui ni kweli au la. Itakuwa vigumu kumsahau Gulam na mwenzie ambao walikuwa kila mmoja na baiskeli yake, walikuja shuleni wameongozana na kurudi kwao wameongozana. Gulam alikuwa pia mcheza mpira hodari sana.
KAMA UNA HADITHI AU PICHA ZA ENZI NINAYOZUNGUMZIA NA AMBAZO UNGEPENDA WATU WAKUMBUKE NITUMIE jkitime@gmail.com au utoe maoni yako katika eneo la comment chini ya habari hii.
l
Categories: Iringa