
KUMBUKUMBU za waalimu wa sekondari nyingi, nianze na Mr Jiran, huyu alikuwa mwalimu Mhindi, aliyekuwa na tabia ya kikohozi na kutema mate hata katikati ya kipindi, alikuwa mwalimu mzuri sana wa Chemistry na ndie alituanzisha kujua mgawanyiko wa atom, kutafuta valency na kadhalika. Pia alikuwa mcheza Cricket na hockey. Nimekumbushwa na rafiki yangu tuliyekuwa pamoja kuhusu mwalimu wa kike Mrs Hoja, siku moja katika hadithi zake akatuahidi kuwa angetufanyia social evening na wanafunzi wa Iringa Girls, na baadae alikwenda kuwa Headmistress wa shule ya jirani ya Iringa Girls Secondary, lakini ile ahadi yake hakuwahi kuitimiza, tulikuwa tukimkumbuka kwa kosa hilo. Social Evening ilikuwa ni shughuli iliyofanyika mida ya jioni saa moja mpaka saa tatu au nne, japo shule nyingine shughuli zilianza saa nane hadi saa kumi na mbili, na mara nyingi social evening ilikuwa siku za mwisho za wiki ambapo shule moja ya wavulana iliwaalika wasichana kutoka shule nyingine au vice versa. Mara nyingine mialiko hiyo ilihusu hata kula chakula cha mchana kwanza, kisha watu kutawanyika madarasani au kwenye viunga vya maua vya shule na kwa kawaida ilikuwa ikiishia kwa dansi. Matayarisho ya social evening yalihusisha kutafuta record player, kutafuta santuri, kuchangisha pesa kwa ajili ya kununua betri za player, na hata kutafuta pipa kwa ajili ya kuifunika spika muziki uwe na bass zaidi. Kama kulikuwa na mpango wa kuwapa wageni vinywaji au chakula basi kamati husika ilichangisha fedha, waliochanga tu ndio walioruhusiwa kushiriki. Shule ya Iringa Girls Secondary tuliita zoo, kwani kulikuwa na utamaduni wa kuruhusu wageni kuwatembelea wasichana hawa siku za Jumapili mchana, hivyo ilikuwa kama kuja kuwaangalia wanyama walio katika Zoo, jina hilo ndilo likawa kitambulisho cha shule ile.Watu tulikuwa tukiwahi sana kuwa karibu na geti la Zoo, na saa nane kengele ikilia basi tuliingia kwenye eneo la shule kwa wingi utadhani tunaenda kuangalia wagonjwa hospitali, kuna wavulana wengine walianza kufika katika gate lile toka saa sita na nusu. Kila mtu alimtafuta mtu wake na wakakaa pembeni wawili wawili, wengine darasani wengine chini ya miti na kadhalika, na saa kumi kengele ililia muda wa kuangalia wasichana ulikwisha, basi wenye kulia walilia wenye kucheka walicheka. Kama kulikuwa na mpango wa social evening basi hapo ndipo pakuagana na kutegemea kukutana social evening. Siku ya ‘sosho’ wavulana walikaa upande mmoja wa hall wasichan upande wa pili, wimbo ukianza wavulana walisimama na kukimbilia msichana wako au unaempenda na kuomba ucheze nae. Aibu kubwa ilikuwa ukikataliwa, unarudi mnyonge na hasa akija mwenzio akakubaliwa kucheza masichana uliyekataliwa. Katika madansi haya ambayo kwa kawaida hayakuwa na kelele sana kutokana na spika kuwa ni za nguvu ndogo, watu walikuwa wakinong’onezana maswali kama, ‘Syllabus ya hesabu mmefikia wapi?’ ‘ Je mmeshaanza kujitayarisha kwa Moke?’ na maswali namna ile.

aliyokuwa akituazima kwa ajili ya ‘sosho’
Tuendelee na waalimu wangu, aliokuweko Mr Mvungi huyu alifundisha Kiswahili na Geography nina hamu sana kumuona huyu bwana maana alikuwa karibu sana na wanafunzi. Ilikuwa kawaida kumkuta akicheza basket ball na wanafunzi, akina Emmanuel Mkusa, Mshindo Msolla, Kipate, Ephraim Mhekwah aka Chuma, John Silva, hawa walikuwa wazuri sana kwenye basketball. Alikuweko Mr Magelewanya huyu alikuwa mkiya sana na alikuwa akifundisha physics na hesabu, naambiwa miaka ya baadae naada ya sisi kuondoka alijulikana kama “Magelewanya Fomular”. Mwalimu KIkudo hatimae alikuja kufundisha Magogoni , na hata wachache katika familia yake bado wanaishi Kigamboni. Mwalimu Sandhu alifundisha biology wakisaidiana na Mr Maulaga aka Mackean, Maulaga nae alikuwa nae mchezaji mzuri wa hockey. Namkumbuka Mr Dhanani, huy mwalimu wa KIhindi alikuwa akitufundisha book keeping. Tulipokuwa Form 1 na 2 kipindi chake kilikuwa mara moja tu kwa wiki, Alikuwa na Kiingereza chake cha kihindi na bado kama namuona alivyokuwa akikosea kutaja majina ya wanafunzi wakati wa roll call ‘Naboth Mabemabati, John Kitaim, sasa kulikuwa na majina ya Kibena magumu zaidi, Eberhard Likiliwike, Ludaliko Nganyange hapo ndio ulikuwa mtihani zaidi kwake. Na alikuwa anajua sana kusimanga. Tarehe ya safari ya Apollo 11 kwenda kwenye mwezi huwa haitoki kichwani mwangu kwa kuwa ilianza Jumatano 16 July, 1969 na wanaanga hao walirudi ardhini July 24, sasa Mr Dhanani aliingia darasani July 15 akatoa homework, kwa bahati mbaya hakuweza kuja darasani July 22, hivyo tulionana nae tena July 29, miamba wengine tukawa hatukufanya ile homework. Nakumbuka tulisimamishwa wote na kashfa yake ambayo sitaisahau ni, ‘Pipal go to the moon and come back in 8 days, you piple have not done your homework in 14 days, God vil not help you, God is busy helping piple go to the moon’
Ilikuwa ni wakati huu huu tukapata mwanafunzi mpya darasani, kijana smart sana alikuwa anaitwa Charles Roman, alikuwa na nywele ndefu kazichana kwa staili yake na hata kaptura aliyokuja nayo ilikuwa ya staili yake. Katikati ya somo, Charles ambaye alitoka shule ambayo hakukuwa na book keeping alinyoosha mkono na kumwambia Mr Dhanani ‘Sir I don’t know book keeping’, jibu alilopata lilimfanya asiingie tena kwenye somo la bookkeeping. Mr Dhanani ambaye wakati huo kajaza ubao kwa notes za book keeping alimuuliza Charles ‘Vea is book keeping, this is Inglis only’
Mr Dhanani alihamia Zambia, siku anatuaga shule nzima tulikutana kwenye ukumbi wa shule akatoa hotuba yake ya kutuaga, sentensi yake maarufu katika hotuba ile ilikuwa ‘Piple come piple go but the school remains the same’ Alitumia neno and mara nyingi kiasi cha wanafunzi kuanza kumtania katikati ya mkutano, na wote tulifurahi aliposema, ‘I am leaving Aringa I am going to Jambia’

KAMA UNA HADITHI AU PICHA ZA ENZI NINAYOZUNGUMZIA NA AMBAZO UNGEPENDA WATU WAKUMBUKE NITUMIE jkitime@gmail.com au utoe maoni yako katika eneo la comment chini ya habari hii.
Categories: Iringa, Uncategorized
Yes Nawakumbuka hao waalimu wote nilijua kuwa Mr Jiran ( jina ambalo linnandikwa Geeran) alikuwa anakula tumbaku ya kihindi iitwayo Paan Hii tumbaku hufungwa kwenye majani ya mgomba na mlaji hutafuna kwa kuweka pembeni mwa shavu Kutema ni lazima
Mwalimu Mvungi alinishawishi nichukue EGM Tosamaganga I hope they enjoy life wherever the are I am one of the boys who never went to the zoo I thought we had enough girls at Lugalo 😂😂😂
LikeLike
Na kweli tulikuwa na warembo tosha Lugalo. Waendaji wa zoo wakubwa walikuwa wanafunzi wa Mkwawa
LikeLike
Mimi nilikuwa na Raleigh nyeupe na nyekundu sports…machozi yananitoka
LikeLike