LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 36


Baba akiwa na baiskeli yake 1953

NILIPOKUWA na umri wa miaka mitano hivi tulisindikizana na baba kwenye duka la Mhindi mmoja alikuwa akiitwa Fateharis, katika duka lake pia kulikuwa kukiuzwa vitu vya kuchezea watoto, lakini kilichonikaa kichwani mpaka leo ni zile baiskeli za miguu mitatu zilizokuwa na rangi rangi za kumvutia mtoto. Nilitaka sana kuwa na moja ya baiskeli zile, nakumbuka siku moja nikaota usiku kuwa nimenunuliwa baiskeli zile zimejaa chumba chote, nililia nilipoamka kukuta hakuna kitu kama hicho. Wakati nikiwa mdogo sana baba alikuwa na baiskeli ambayo mama naye alijua kuiendesha. Nilipofika darasa la tatu mama akapata kazi ya ‘mama maendeleo’ – Welfare officer, hivyo serikali ikampa baiskeli zile za ‘kike zisizo na mwamba katikati. Mjomba wangu alipata kazi ya kuuza magazeti kwenye duka la Iringa Printers akapewa baiskeli yenye tenga mbele na hapo ndipo alipoweka magazeti yake. Baadae mjomba alipata kazi shirika la posta akawa na rafiki yake mfanyakazi mwenzie aliyeitwa Mwakasuga, huyu jamaa alikuwa smart sana, nae alikuwa na baiskeli iliyopambwa vivuri na ulikuwa usafiri wa mtu mwenye kipato.
Wakati wa mkoloni na miaka kadhaa baada ya hapo baiskeli zilikuwa zikilipiwa leseni, kama ilivyokuwa kwa redio. Nadhani leseni ya baiskeli ilikuwa shilingi tatu, kisha unapata kibati cha rangi kilichoandikwa mwaka na ni lazima ubandike kibati hicho kwenye baiskeli au utakamatwa na makarani wa kodi, na baiskeli yako kuzuiwa. Baiskeli ilikuwa lazima iwe na taa na kengele.Baiskeli maarufu zilikuwa Raleigh, Humber, Gazelle, BSA. Kulikuwa na posters na matangazo ya redio yakitangaza baiskeli hizi. Wimbo wa kutangaza baiskeli ya Raleigh ulikuwa na maneno yafuatayo;
Rale Rale
Baiskeli ya chuma
Weka akiba weka akiba ya kununua Rale

Nembo ya Raleigh


Sikuwahi kupata bahati ya kumiliki baiskeli, lakini nilipofika sekondari rafiki zangu wengi walikuwa na baiskeli. Kulikuwa na watu wanaishi mbali sana na shule, hivyo baiskeli hazikuwa anasa bali usafiri muhimu. Uhusiano wa Tanzania na China ulisababisha bidhaa nyingi zilizokuwa zikitoka nchi za magharibi kuachwa na kukaingia bidhaa sasa kutoka Uchina, baiskeli ilikuwa moja ya bidhaa hizo. Baiskeli za Phoenix. Hizi baiskeli zilikuwa bei nafuu kuliko zile za kutoka UIngereza na India, na hakika zilikuwa imara, hatimae kulikuwa hakuna aina nyingine ya baiskeli zilizoweza kupatikana madukani. Pale Lugalo miaka ya 68 mpaka 71, palitengenezwa maegesho ya baiskeli za wanafunzi, kila mtu na baiskeli yake. Nyingi zilikuwa kubwa nyeusi na kijani, nyingine zilikuwa Phoenix sports ambazo zilikuwa ndogo kidogo na zilipatikana kwa rangi ya kijani, bluu na nyeusi. Nakumbuka baiskeli moja tu nyekundu ndogondogo ya kike ya bi Dellilah, sikumbuki msichana mwingine aliyekuwa akija shule na baiskeli zaidi yake. Baiskeli hizi zilianza kuwekewa de railer maarufu kwa jina la ‘gia’, na kuanza kuwa na ufanisi zaidi, kutoka Lugalo kuja mjini barabara ilikuwa na mwinuko si kama ilivyo sasa, hivyo kwa baiskeli kubwa njia rahisi ya kupanda mlima ilikuwa kwa kusukuma hizo baiskeli na kupanda baada ya kufika eneo la TANESCO. Baada ya baiskeli kuwa za gia kazi ikawa nyepesi zaidi.

Phoenix sports

Waalimu kadhaa nao walikuwa na baiskeli, akiwemo mwalimu Kikudo, nadhani alikuwa akiishi Mkwawa, mwalimu Maulaga nae alikuwa na baiskeli phoenix sports ya kijani.
Moja ya burudani za kuwa na baiskeli ilikuwa ni kutembelea sehemu mbalimbali nje ya mji, kwenda uwanja wa ndege wa Nduli, kwenda Tosamaganga, kwenda Isimila au Itamba na hizo zilikuwa outing za mara kwa mara watu walizifanya wakiwa kwa kikundi.
Burudani nyingine ilikuwa mashindano ya baiskeli, wakati wa sikukuu za Kitaifa huo ulikuwa mchezo mmoja muhimu sana, aidha kwa kuzunguka uwanja wa michezo mara kadhaa au kwa kufanya mashindano ya kwenda Nduli na kurudi.
Wapanda baiskeli maarufu ninao wakumbuka ambao walikuwa wakishiriki hata mbio za baiskeli ni John Silva, Gulam, Mohamed Issa, Ismail Thakore. Baiskeli ya John Silva ilikuwa Phoenix sports ya kawaida baadae akaweka usukani wa kupinda wa baiskeli za mashindano. Vituko vya baiskeli vilikuwa vingi lakini sitasahau siku moja kulikuwa na maandamano na wanafunzi walikuwa wamejipanga nje ya ukuta wa viwanja vya Bomani, mwanafunzi mmoja akaja spidi kali na baiskeli, nadhani ilikuwa ni kuwaonyesha mbwembwe wasichana wengi waliokuwa pale, alikuwa akitokea kwenye mnara wa saa na akakunja kona pale posta kuelekea sokoni, bahati mbaya akala mueleka mzuri tu sasa kosa lake lilikuwa ni kujaribu kufuta kosa kwa kuokota baiskeli haraka kuipanda na kuondoka pale, bahati mbaya alipopanda kabla ya hatua mbili akadondoka tena huku akishangiliwa na wasichana aliotegemea kuwa ‘impress’. Ikalazimika awe mpole na kuondoka na baiskeli polepole kinyonge.
Pale sokoni mbele ya duka la Omari store kulikuwa na watu kazi yao kukodisha baiskeli. Nusu saa, senti hamsini na saa moja shilingi. Kwa kweli ni biashara ambayo ukiifanya kwa namna ile siku hizi baiskeli zote zitaibiwa siku hiyohiyo. Ilikuwa unaenda kwa jamaa, unamwambia unataka baiskeli ya aina gani na kwa muda gani, unalipa, anakuandika jina unaondoka na baiskeli.
Baiskeli pia zilitumiwa na ‘guoguo’. Guoguo walikuwa Waarabu ambao walikuwa wakipita mtaa kwa mtaa kwa staili hii ambayo Wamachinga hudai wameigundua, na Waarabu hao walikuwa wakiuza nguo, hivyo walipokuwa wakipita mitaani walikuwa wakitangaza, ‘Guo guo’ yaani ‘Nguo nguo’. Awali walikuwa wakitembea kwa miguu kama machinga sasa, baadae wakaanza kutumia baiskeli, baadae walikuwa wakitumia pikipiki, hasa Honda 125. Guoguo walikuwa wakikopesha kiasi utakacho, walikuwa wakiuza vitambaa , na hata mazuria.

Si mara moja niliona bibi harusi akisafirishwa kwa baiskeli baada ya kutoka kanisani pale Mshindo. Harusi zilikuwa zikifanyika mapema kama saa tano au sita mchana. Kwa wale wakazi wa Mlandege harusi ingetoka pale kanisani Mshindo na kuanza kuelekea Mlandege kwa miguu wapambe wakiimba’ Swee swe twiwonaga swee’, kwa wale wenye uwezo bibi harusi alipanda kwenye keria ya baiskeli na kulikuweko mtu anasukuma hiyo baiskeli mpaka mwisho wa safari. Baiskeli zilikuwa na nafasi kubwa sana katika maisha ya kila siku.

Tangazo la Raleigh


Baiskeli ya muuza magazeti

KAMA UNA HADITHI AU PICHA ZA ENZI NINAYOZUNGUMZIA NA AMBAZO UNGEPENDA WATU WAKUMBUKE NITUMIE jkitime@gmail.com au utoe maoni yako katika eneo la comment chini ya habari hii.

Categories: Iringa

Leave a comment