LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 38


Muziki wa soul ulianza kuingia Iringa mwaka 1968 hivi. Nilianza kusikia santuri za muziki wa soul nyumbani kwa rafiki yangu John Silva. Baba yake John Silva ndie aliyekuwa Fundi Mkuu kwenye garage ya kampuni ya Tanzania Motor Mart. Kwa sasa gereji hiyo inamilikiwa na TEMESA, ni gereji inayoangaliana na Chuo Kikuu cha RUCU. Familia ya akina John Ilikuwa ikiishi katika nyumba ya matofari iliyo ubavuni mwa gereji hiyo. John alikuwa na gitaa zuri na pia kulikuwa na record player nyumbani kwao hivyo nikamsikia kwa mara ya kwanza muimbaji Otis Redding na nyimbo kama I have got dreams, Amen, These arms of mine, nyimbo ambazo mpaka leo sichoki kusikiliza. Pamoja na kuwa na gitaa pia alikuwa na kitabu cha kujifunzia gitaa, hivyo basi nilikuwa nakopi maelekezo ya kile kitabu na kwenda kufanyia mazoezi nyumbani. Muziki wa soul ambao asili yake ni Wamarekani weusi ulikuja na tamaduni zake nyingine kama uchanaji wa nywele kwa mtindo wa Afro, ambapo nywele zilichanwa kwa ustadi na kujaza kichwa, muziki huo uliambatana na uvaaji, suruali za bell bottom, mashati ya slimfit na viatu vya platform. Kiujumla pia usafi wa mtu binafsi. Wanamuziki maarufu wakati huo walikuwa akina James Brown, ambae pamoja na muziki wake alikuwa mchezaji mzuri wa muziki wa soul. Pia wanamuziki wengine wa mtindo huo walikuwa akina Wilson Picket, Clarence Carter, Sam and Dave na wengine wengi sana. Lakini kuna huyu mwanamuziki aliyeitwa Buddy Guy, huyu hasa ndie aliyekuja kuwasha swichi ya upenzi wa muziki wa soul. Buddy Guy alikuwa mpiga gitaa mashuhuri Mmarekani mweusi, Ubalozi wa Marekani ukamleta huyu bwana na akapiga onyesho la bure katika viwanja vya Mnazi Mmoja, kuanzia hapo vijana wanamuziki waliosoma kidogo hasa wanafunzi wa sekondari, shughuli ilikuwa kujaribu kuwa Mmarekani mweusi kadri itakavyowezekana. Katika kuongea kila baada ya sentensi ungesikia ‘Yea man”, na pia kuitana ‘Hey Brotherman’ basi vijana wa namna hiyo waliitwa Ma yea man au Mabrotherman. Mwanafunzi mmoja wa Lugalo ambaye alidai alihudhuria onyesho la Buddy Guy wakati wa likizo alikuwa na mengi ya kutufundisha sie wenzie wa Iringa. Wakati huu fursa za mtoto wa Iringa kufika Dar es salaam zilikuwa ndogo sana, hivyo kama ukimjua mtu aliyekwenda Dar es Salaam basi huyo ndie alikuwa ndie chanzo chako kikuu cha habari za mjini. Rafiki yetu Steven Lunyungu ndie alikuja kutuhabarisha swala la Buddy Guy, akatuambia jinsi Buddy alivyokuwa akipiga gitaa kwa kutumia leso yake, na jinsi watu walivyokuwa wakimshangilia, sisi wenyewe tukajiongeza alimoacha ikawa na sisi tukihadithia ni kama vile na sisi tulimuona Buddy Guy.
Mazoezi nyumbani kwa John Silva yakiendelea pia tukiwa na rafiki yake mkubwa Mohamed Issa pembeni. Kulikuwa na magazeti kutoka Marekani yaliyokuwa yakiitwa True Detective, katika magazeti haya kulikuwa kunatolewa matangazo kuwa nyimbo zinahitajika. Kulikuwa na kampuni zinanunua nyimbo na maneno ya nyimbo , nasi tukawa na ndoto kuwa nyimbo zetu tukipeleka ‘tutatoka’. Nilipeleka mashahiri kadhaa kwenye anwani zilizotajwa, lakini majibu hayakurudi hata siku moja. Nakumbuka siku moja niliwakuta John Silva na Mohamed Issa wakiwa na daftari la nyimbo alizotunga John Silva, walinambia walikuwa wametunga wimbo ambao walikuwa na uhakika utawatoa ulikuwa unaitwa Double V. Maneno machache ya wimbo ule bado nayakumbuka ulikuwa unasema,
Who can it be
Look and try to see
The lady in double V
Double v on her blouse

Sijui uliishia wapi wimbo huo ntawauliza.
Suruali yangu ya kwanza ya Bell Bottom au pecos niliishona mwaka 1969. Ilikuwa siku chache kabla ya siku yangu ya kuzaliwa, mama , ambaye wakati huo alikuwa kozi moja huko Masasi, sehemu inaitwa Ndwika, akanitumia fedha ninunue ninachotaka, mimi nikaona ninunue kitambaa cha suruali nishone Bell bottom. Kulikuwa na mzee mmoja fundi cherehani maarufu alikuwa akishona nguo pale ilipo stendi ndogo ya daladala iliyoko Miyomboni. Eneo hili daima lilikuwa wazi na katikati ya eneo kulikuwa na bomba ya maji ya umma. Jirani ya fundi huyu kulikuwa na kinyozi maarufu ambaye alikuja kupata kashfa kama ile ya fundi Maumba miaka mingi baadae. Fundi alinipima vizuri baada ya siku chache nikapita kuchukua suruali yangu. Suruali hiyo niliivaa kwa mara ya kwanza kwenye party ya birthday ya msichana tuliekuwa tukisoma aliyekuwa na asili ya Kisingasinga aliitwa Inderjit, nae alikuwa akiishi maeneo hayohayo ya Miyomboni. Pamoja na kuvaa suruali mpya nilikuwa sina raha maana niliona hainikai sawasawa, nilikuja gundua baadae kuwa fundi alishona mguu mmoja mwembamba kuliko mwingine.

Michael Jackson enzi za Afro hair


Kuchana Afro ndio ilikuwa staili ya wajanja, lakini asili ya nywele zetu Wabantu ni kipilipi, hivyo ili uchane Afro ilihitajika kwanza uzinyooshe nywele hivyo basi ukaingia utamaduni wa kuchoma nywele. Wasichaa kwa wavulana walijitahidi kuchoma nywele ziwe ndefu ili wachane Afro. Kulikuwa na watu Afro zao zilijulikana mji mzima kwa mfano kwa upande wa wanafunzi, kule Iringa girls kulikuweko na binti mmoja huyo alikuwa ndie mwenye Afro kubwa shule nzima. Mkwawa kulikuwa na mwanafunzi anaitwa Deo yeye ndie alikuwa bingwa wa suruali za bell bottom. Suruali hizi ziliambatana na shati iliyobana sana iliyoiywa slimfit. Kwa vile tulikuwa hatuna vitambi basi tuliweza kubana sana mashati vifungo karibu vinaachia. Miaka hiyohiyo vikaingia viatu vyenye kisigino kimepanda juu hivyo kuitwa platform shoes kwetu vikajulikana kwa jina la raizon. Nilichelewa kidogo kuvaa Raizon, lakini nilipopata mshahara wangu wa kwanza mwaka 1974 nikanunua jozi yangu ya kwanza ya raizon zilizokuwa zikitengenezwa na kiwanda kimoja Moshi, zilikuwa maarufu kwa jina la ‘Mchaga kajitahidi’.


Duka lililokuwa likiuza sahani ya santuri lilikuwa duka ambalo lilikuwa linaangaliana na Jamati na hoteli ya Green Hotel ya Mzee Kamrudin. Duka hili pia lilikuwa linauza baiskeli. Hapokaribu kila wiki alikuwa analeta santuri mpya za muziki wa aina mbalimbali. Hivyo kilikuwa kituo kingine muhimu kwa wapenda muziki, kazi hii ilikuja kuchukuliwa na RTC katikati ya miaka ya 70.
Mwaka huo 1969 nami nikapata nafasi ya kutembelea Dar es Salaam, lakini nilifikia Kibaha kwa mjomba wangu ambaye alikuwa Headmaster wa KIbaha Secondary, Mr George Mkwawa. Nilikaa Kibaha siku chache kisha nikaenda Dar es Salaam kuwatembelea rafiki zangu ambao baba yao Mr Michongwe alikuwa mwalimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akina MIchongwe walikuwa Wamalawi na baba yao alikuwa balozi Marekani akakorofishana na Rais wake Kamuzu Banda hivyo akakimbilia Tanzania na kuwa mwalimu pale chuo kikuu. Rafiki zangu hao walikuwa mtu na kaka yake, Mbuto na Dazika. Dazika alikuwa mpiga gitaa hivyo urafiki ukawa mkubwa zaidi. Pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kulikuwa kuna bendi mbili, moja ya watoto wa waalimu ambamo Daziki alikuwa mmojawapo. Bendi hii ilikuwa inajiita The Frozen Soul, pia alikuwemo mwanamuziki Dave Marama ambaye mpaka leo ni mwanamuziki huko Australia. Bendi ya pili ilikuwa ya wanachuo, ninaemkumbuka zaidi ni Mwabulambo ambaye alikuja kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni. Siku za Jumamosi tulienda ukumbi wa White house Ubungo na kupiga na bendi iliyokuwa ikiutumia ukumbi huo, bendi hiyo iliitwa Super Bocca. Hatimae nilirudi Iringa nami nikiwa na hadithi nyingi kwa waliokuwa na muda wa kunisikiliza.
Bendi yetu ya shule ya Lugalo haikwenda popote nadhani kwa sababu tulikuwa na mawazo yaliyopishana kimuziki, huku Iddi Mwanahewa anataka kupiga rumba, huku John Silva anataka kupiga soul. Iringa mjini wakati huo ilikuwa ikitamba kwa bendi iliyoitwa Highland Stars, kwa kuwa nilikuwa shule ilikuwa marufuku kukutwa kwenye madansi usiku, sikupata kuiona bendi hiyo ikiwa jukwaani. Lakini niliwaona mara kadhaa wakitangaza dansi, bendi nzima ilikuwa ikijazana kwenye pickup na magitaa yao kisha kuunganisha kwenye amlifaya na kupita mitaani wakipiga nyimbo zao ‘live’ na kutangaza kuwa bendi hiyo ingekuwa jukwaani siku ile.
KAMA UNA HADITHI AU PICHA ZA ENZI NINAYOZUNGUMZIA NA AMBAZO UNGEPENDA WATU WAKUMBUKE NITUMIE jkitime@gmail.com au utoe maoni yako katika eneo la comment chini ya habari hii.

Categories: Iringa, Uncategorized

3 replies

Leave a comment