HISTORIA FUPI YA TANCUT ALMASI ORCHESTRA


BAADA ya bendi kongwe ya Highland Stars kusambaratika mwishoni mwa miaka ya 60, Iringa haikuwa tena na bendi yoyote ya maana, mpaka ilipokuja kuzaliwa bendi ya shule ya Mkwawa, bendi hii na mtindo wake wa Ligija ilikuwa ndio bendi maalumu kwa ajili ya mwisho wa wiki, ilikuwa ikipiga muziki wa mchana uliojulikana kama Buggy, hivyo ulikuwa zaidi muziki wa watoto na vijana. Ilikuwa bendi nzuri sana kwa wakati huo, wanamuziki wake wakiwemo, Sewando aliyekuwa akipiga solo, kwa sasa ni mwalimu wa Chuo Kikuu mstaafu, Manji alikuwa akipiga rythm na second solo, sasa ni engineer mstaafu anaeendesha shule ya muziki Tabata Dar es Salaam, Kakobe alikuwa mpiga tumba kwa sasa nia Askofu anaeendesha makanisa kadhaa, Danford Mpumilwa, mwanzilishi wa Serengeti Band ya Arusha na mwandishi mstaafu, na kutokana na miaka mingi ilimepita wengi wamekwisha fariki.
Bendi nyingine iliyoanzishwa miaka ya sabini ni bendi ya chuo cha ualimu cha Klerruu. Chuo kilikuwa na magitaa hivyo wanachuo waliokuwa wakijua kupiga magitaa walianzisha bendi ndogo. Chuo pia kilifanya mpango wa kutafuta wanamuziki ambao wakapewa ajira hapo chuoni, kulikuweko na Mzee Mahmoud Bezi, huyu historia yake ya kupiga gitaa ilianzia Highland Stars, alipokuja Klerruu akawa anashughulika na usafi huku anapiga kwenye bendi ya chuo, kwa sasa ni Shehe anaeheshimika Iringa. Walikuweko wazee wengine watatu ambao wote walikuwa wakifanya kazi za upishi jikoni lakini walipata ajira kwa kuwa walikuwa wanamuziki. Wanachuo wanamuziki waliowahi kupitia pale ni Kassim El Siaggy, huyu yupo Tanga akiendelea na kufundisha watalii Kiswahili na kuendelea na utengenezaji wa filamu, kulikuwa na mwanachuo mmoja aliyewahi kuwa mwanamuziki wa Mara Jazz na alitufundisha nyimbo nyingi za Mara Jazz bahati mbaya simkumbuki jina lake. Nilikuweko mimi John Kitime, rafiki yangu marehemu Yusufu Mdee, Maika, huyu Maika bahati mbaya alirukwa na akili wakati bado tuko chuoni, nadhani tatizo lake lilikuwa la muda mrefu hatukulijua , ila nikikumbuka mambo yake nadhani alikuwa anaumwa kwa kipindi kirefu, kwa mfano kulikuwa na siku haendi darasasni anaenda moja kwa moja kwenye chumba chenye vyombo vya muziki, huko ataanza kupiga nyimbo akawa anaimba kwa hisia mpaka anatoa machozi. Nilikutana na Maika mara ya mwisho pale Chalinze nikiwa na bendi ya Vijana Jazz, alikuwa katika hali mbaya sana japo alinikumbuka na hata tukaanza kukumbushana kuhusu wenzetu tuliokuwa nao Kleruu, ilisikitisha sana kwangu, ikawashangaza wakazi wa Chalinze kumsikia mtu wanaemdharau kuwa kichaa akiongea Kiingereza kizuri na tukiwa na mazungumzo ya kina kabisa.

Spika tulizokuwa tukitumia

Hakukuwa na bendi yoyote iliyoibuka na kufanya chochotekwa muda mrefu. Vijana wachache wa Iringa, kati yao walikuweko Juma Msosi,Hashim Kasanga , Nico , Mamado Kanjanika, Saidi Kananji, John Kitime, walijaribu kuanzisha kundi lililojulikana kama Chikwalachikwala mwaka 1975, kundi hili lilikuja kukusanya vijana wengi wa Iringa waliotaka kupiga muziki lakini halikufika popote kutokana na ukosefu wa vyombo. Chikwalachikwala ilikuwa na magitaa matatu, japo gitaa la bezi daima lilikuwa halina nyuzi, hivyo ni kama bendi ilikuwa na magitaa mawili tu. Ilikuwa shida sana kupata nyuzi za magitaa hivyo zilitimika ‘cable’ za breki za baiskeli za sports, tulinunua waya za breki na kuzichuna kisha kuzichambua na hizo ndizo zilikuwa nyuzi zetu za magitaa. Bendi hiyo pia ilikuwa na ngoma moja kubwa lakini haikuwa na pedali ya kuwezesha kupiga kwa miguu, hivyo ililazimika ‘drums’ ziwe zinapigwa na watu wawili, mmoja akiwa kakalia kitofali anadunda ngoma kubwa na mwingine akiwa anapiga ngoma ndogo. Vyombo hivi awali ilisemekana ndivyo vilivyokuwa vikitumika na Highland Stars wakati wa uhai wake, baadae ikawa inasemwa vilikuwa vyombo vya TANU Youth League ambavyo vilikuwa vikitumika na bendi ya shule ya Mkwawa, hatimae ndipo vikaangukia kwenye mikono yetu. Tulitambulika rasmi kama Iringa Jazz Band,jina lililosajiliwa kwa Afisa Utamaduni, lakini siku moja Mamadow Kanjanika akaja na wazo kuwa mtindo wetu uwe Chikwala chikwala, sijui alilitoa wapi hilo jina. Lakini wakati ule kufuatia wimbi la bendi za Kongo kuwa majina yanayojirudia kama vile LipuaLipua, Belabela, Shamashama na kadhalika bendi za Tanzania nazo zikaanza kuwa na mitindo au majina ya bendi yenye jina la kujirudia rudia, kama vile Vangavanga, kokakoka, Dundadunda na kadhalika, nasi tukaja na Chikwalachikwala, jina ambalo kwa maajabu sana bado nalisikia wazee wa Iringa wakilitaja mpaka leo japo bendi yenyewe haikuwahi kurekodi wala kutoka nje ya mkoa. Lakini kutoka hiyo Chikwalachikwala, walitoka wanamuziki kama Ally Makunguru aliyekuja kufanya mambo makubwa JKT Kimbunga, Tanzania Stars, Sikinde na Ndekule, akiwa mpigaji wa magitaa yote, solo, rythm na second solo. William Maselenge ambaye baba yake mdogo alikuwa refa mashuhuri Iringa, tulijiunga wote Orchestra Mambo Bado na baadae akawa Maquis, guitar lake la rythm linasikika katika nyimbo kama Ngalula, kisha akarudi TANCUT Almasi kama mpiga rythm na second solo. Hashi Kasanga aliyekuwa muimbaji wa sauti ya tatu katika asilimia kubwa ya nyimbo za TANCUT, Amani Ngenzi mpiga bezi katika nyimbo nyingi maarufu za TANCUT, Said Kananji aliyekuwa mpiga tumba wa kwanza wa TANCUT, Mamadow Kanjanika alikuja kuwa kiongozi wa kwanza wa TANCUT, hivyo Chikwalachikwala iliacha alama yake katika muziki wa Tanzania.
Awali mazoezi ya Chikwalachikwala yalikuwa yakifanyika kwenye chumba alichopanga Mamadow, pale Barabara mbili kwenye nyumba ya Mzee Swedi Kasingo, tulihama sehemu kadhaa ikiwemo kuhamia kwa mganga wa kienyeji aliyekuwa mfadhili wetu kwa kutupatia chumba cha kufanya mazoezi kwenye nyumba moja wapo inayopakana na hoteli ya Babanusa kwa sasa. Tuliachana na mfadhili yule baada ya kuzua balaa kwenye ukumbi wa disco wa Soweto, ambapo siku moja alimtaka msichana mmoja na msichana yule alipomkataa jamaa akatoa nyoka mfukoni, lilikuwa timbwili la kutosha mganga akaishia kulala kituio cha polisi na sisi kesho yake tukahamisha vyombo.
Chikwala chikwala ilikuwa inapiga katika kumbi mbili kuu, Community Center Kitanzini na Weekend Bar ya Kihesa. Ni muhimu kumkumbuka Mzee Mwashitete aliyekuwa meneja wa Community Center kwani bila yeye kulikuwa hakuna bendi, alituazima amplifaya na maik ya community, kwani tulikuwa tunaimbia maik moja tu na kutumia amplifaya hiyo moja kwa vyombo vyote. Na vyote hivyo vikiwa vinatoa sauti kwenye spika moja, tuliokuwa tukiitundika juu kabisa ya ukumbi wa Community.
Mwaka 1987 wafanyakazi wa kiwanda cha kuchonga almasi pale Iringa, TANCUT, walifanya kazi ya ziada hivyo wakawa walipwe fedha ya ziada na mzungu mmoja toka Ubelgiji. Chini ya tawi lao la Jumuia ya Wafanyakazi (JUWATA) wakakubaliana kuwa badala ya kugawana fedha hiyo na kila mtu kupata kiasi kidogo tu, wakaona wanunue vyombo vya muziki wawe wanapata burudani baada ya saa za kazi, na hivyo ndivyo vyombo vya bendi ya TANCUT Almasi Orchestra vilivyopatikana. Wanamuziki wenyeji waliokuwa wakiendeleza Chikwala chikwala, akina Mamadow, Said Kananji, Juma Msosi na wengi wengine wakawa ndio wanamuziki wa kwanza wa kundi hili. Kampuni ikamuita Ndala Kasheba kuzindua vyombo na ikiwezekana kujiunga na bendi hiyo, Kasheba alifanya mazoezi na wanamuziki waliokuweko wakiwemo Shaaban Yohana ambae alikuwa mpigaji mzuri sana wa gitaa la solo, kuhusu kubaki katika bendi ilishindikana hawakukubaliana masharti, lakini ndie aliwataarifu akina Kasaloo kuhusu bendi hiyo. Wakati huo mimi nilikuwa katika bendi moja ambayo ilianzia Chikwalachikwala lakini ikahamia Dar es Salaam, huku tukabadilika jina na kujiita Seleleka. Mwenye vyombo tulivyokuwa tukitumia aliitwa Kick van de Heuvel, huyu alikuwa Mholanzi aliyeingia nchini hasa kwa ajili ya kufanya kazi kwenye mradi ulioitwa Mianzi Miti, nae alikuwa mpiga piano mzuri, alianza kuwa na ndoto kuwa tupige muziki wa kiasili zaidi, hivyo tukawa hatukubaliani ikaonekana tuvunje bendi. Kwa kuwa bendi ilianzia Iringa tulienda Iringa na kupiga dansi la mwisho kwenye ukumbi uliokuwa unaitwa Bank Club, kwa sasa ni eneo la Chuo Kikuu cha RUCU. Baada ya dansi tukasambaratika nikaenda kuungana na wenzangu waliokuwa wameanzisha TANCUT. Bado haikuwa bendi nzuri sana, wanamuziki wa bendi ya Dodoma International wakapata taarifas kuwa kuna vyombo vipya, hivyo wakaja Iringa na kwenda kujitambulisha kwa uongozi wa TANCUT, hakika walikuwa wazuri kuliko tulivyokuwa tatizo lao walikuwa wakitaka kuchukua vyombo na bendi ihamie Dodoma, hapo ndipo hawakuelewana na menejmenti ya TANCUT. Hivyo wakachaguliwa wachache ndio wakabaki kwenye bendi. Mohamedi Ikunji, Athumani Saburi, na wengine wawili. Muda mfupi baada ya hapo ndipo wakajiunga mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa na Mafumu Bilali na muda mfupi baadae akajiunga Kawelee Mutimwana, bendi ya TANCUT ikaanza safari yake ya umaarufu.

John Kitime nikiseti mixer ya TANCUT Band 1986

Album ya kwanza ilikuwa na nyimbo zifuatazo
Nimemkaribisha nyoka– mtunzi Kasaloo Kyanga, waimbaji Kasaloo, Kyanga Songa, Mohamed Shaweji na Hashim Kasanga. Solo Shabaani Wanted, second solo Mohamed Ikunji , rythm John Kitime, bass Amani Ngenzi
Kashasha– mtunzi Kyanga Songa, waimbaji Kyanga , Kasaloo, Shaweji, na Hashimu, Solo Shaabani Wanted, rythm John Kitime, second solo Mohamed Ikunji, Bass Amani Ngenzi
Tutasele, mtunzi Kasaloo, Big Four mtunzi Mamadow Kanjanika, Kuwajibika mtunzi Zacharia Daniel, Kiwele mtunzi Kawelee Mutimwana, na Mtaulage utunzi wa John Kitime. Nyimbo hizi zilirekodiwa mwaka 1987 na bado zinarushwa hewani mpaka hii 2020.

Categories: Muziki Muziki

1 reply

  1. Kuna nyimbo za album ya mwisho ya Tancut, album iliitwa MBUGUSWA ndani yake kulikuwa na nyimbo kama Sista K nk.

    Naomba kama nyimbo hizi za album ya Mbuguswa zipo naomba nitumiwe.

    Like

Leave a comment