
Mji wa Iringa ni mji ambao ni wa watu mchanganyiko kihistoria. Tofauti na historia za miji mingi Tanzania, mji wa Iringa kwanza haukuanzishwa na kabila moja, ni mji wenye historia ya kuchangamsha ambayo ingeweza kutengeneza filamu yenye mvuto mkubwa. Jina la kwanza la mji huu lilikuwa Neu Iringa, likimananisha Iringa mpya, kwa kuwa ilipo Kalenga sasa ndio ilikuwa Alt Iringa yaani Iringa ya zamani. Jina Iringa lilitokana na neno Lilinga ikiwa na maana Boma. Kwa kuwa Mkwawa alijenga Boma la kwanza kule Kalenga, basi baada ya jeshi la Wajerumani kuvunja ngome ile na Mkwawa kuingia msituni, ilianza vita ya msituni, Mkwawa akiendelea na mapigano japo hakuwa na makazi ya kudumu. Ili kumdhibiti utawala wa Ujerumani ukampa kazi hiyo, Luteni Tom Von Prince aliyefahamika pia kwa jina Bwana Sakarani, yeye ndie aliyeanzisha ngome mpya ya askari hapa ulipo mji wa Iringa sasa. Ngome ilikuwa na askari wengi Waafrika kutoka sehemu mbalimbali za nchi yetu sasa, kulikuwa na Wamanyema, Wasukuma, Wanyamwezi na hata Wanubi kutoka Sudani. Askari hawa walikuwa wakisafiri na familia zao hivyo walikuweko wanaume na wanawake wa makabila hayo, na hao ndio walikuwa wakazi wa kwanza wa mji huu. Kwa hakika hapakuwa mahala salama kwa Wahehe hivyo walikuwa wageni katika ngome hii mpya. Wafanya biashara wa Kihindi walihamia hapa kuanzia zama hizo za Von Prince. Luteni Von Prince aliwahi kurudi kwao akaoa mke wa Kijerumani aliyeitwa Magdalene ambaye hadithi zinatusimulia kuwa alikuwa mtu wa karibu sana wa Mpangile aliyekuwa mdogo wake Mkwawa, hata hatimae akamfundisha kusoma Kijerumani kidogo. Lakini kuna askari wa Kijerumani ambao walioa wanawake Waafrika na hivyo kuanzisha koo mpya kabisa katika mji huu zama hizo. Wakati huo huo wa enzi za Wajerumani kukaweko na wageni wengine toka Ulaya hawa walikuwa Wagiriki, mmoja wa Wagiriki wa kwanza kuingia Iringa aliitwa Christos Tsavalos, walipowasili nchini wengine wakaanzisha maduka madogo madogo wengine wakaingia katika kilimo. Kilimo maarufu cha Wagiriki kilikuwa kilimo cha tumbaku, Wagiriki walipendelea zaidi kuajiri watu wa kabila la Wakinga katika mashamba yao, kwani watu wa kabila hili husifika kwa uhodari wa kazi za shambani. Wagiriki wengi wakapata wake wenyeji hivyo tena Iringa ikajiongezea mchanganyiko mwingine wa wakazi wake. Waarabu wa kutoka pande mbalimbali za Uarabuni wakahamia mji huu kama nilivyoandika katika makala moja kabla kulikuwa na Waarabu waliokuwa wakifanya biashara ya kuzunguka na nguo, maarufu kama Guoguo, na kuna waliokuja kufungua maduka na kadhalika. Wahindi walikuwa wa makabila mbalimbali pia, kulikuwa na Khoja, Wahindu, Magoa, Singasinga wote walikuweko kuchangamsha mji wa Iringa. Wakazi wa zamani wa Iringa watakumbuka Goa aliyekuwa anaitwa Fernandes alikuwa na Taxi kadhaa zilizokuwa chini ya jina la Fernandes Cabs. Kulikuweko na Singasinga wengi wakiwa wanafanya kazi hasa za ufundi, kuanzia ufundi seremala, ufundi wa magari na hata ujenzi, nao pia wanaume walioa wanawake wa Kiafrika na kuchangia katika kuleta uzuri wa Iringa. Katika mlolongo huu huwezi kuwasahau Wataliani ambao wengi walikuja kwa ajili ya umishionari baada ya shirika la Consolata kuweka nguzo zake hapa Iringa.






KAMA UNA HADITHI AU PICHA ZA ENZI NINAYOZUNGUMZIA NA AMBAZO UNGEPENDA WATU WAKUMBUKE NITUMIE jkitime@gmail.com au utoe maoni yako katika eneo la comment chini ya habari hii.
Categories: Iringa