LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 3


Maandamano yakipita ukumbi wa Highlands kuelekea garden

LEO  nirudi nyuma tena mwaka 1961, mwaka ambao nchi yetu ilipata Uhuru, na ndio mwaka nilianza darasa la kwanza pale Government Primary School (Shule ya Msingi Mlandege). Hii ndio shule kongwe kuliko zote pale Iringa. Mpaka mwaka huo ilikuwa inaishia darasa la nne tu. Shule hii ilijengwa 1947 baada ya kuweko shule iliyoitwa shule ya tembe iliyokuwa pale ambapo yapo Makaburi ya Mlandege. Mkesha wa siku ya Uhuru kulikuwa na matayarisho ya sherehe Uhuru pale ulipo uwanja maarufu wa Garden au uwanja wa Boma, pembeni mwa hospitali ya mkoa. Uwanja huu miaka yote ulikuwa uwanja muhimu kwani kabla ya kuweko uwanja unaojulikana sasa kama uwanja wa Samora, huu ndio ulikuwa ndio uwanja wa mpira ambao timu zote kubwa zilicheza. Hata mashindano ya shule mbalimbali yalikuwa yanafanyika hapa. Sasa siku kabla hiyo kabla ya Uhuru spika zilifungwa na muziki ulikuwa ukipigwa, taa za karabai ziliwekwa sehemu mbalimbali za uwanja, sehemu nyingine watu walikoka moto wakisubiri Uhuru, wengi tulikuwa hatuujui umeme siku hizo. Niliwacha swichi ya umeme kwa mara ya kwanza nyumbani kwa David Mwaibula 1964, familia yake ilikuwa ikiishi nyumba zilizoangaliana na kanisa la Anglican Uzunguni, lakini hiyo ni hadithi ya siku nyingine. Maspika yalikuwa yakipiga nyimbo mbalimbali, nakumbuka maneno machache ya wimbo mmoja tu wa Salum Abdallah ukiimba, ‘ Tutie jembe mpini twendeni tukalime’. Siku ya Uhuru ilikuwa shamra shamra sana pamoja na kuwa nchi ilikuwa na vyama vingi na vingie vilishindwa kwenye uchaguzi, kwa ujumla watu wote walishangilia kwa ngoma na kukesha pale Uwanja wa uhuru.

Huu uwanja wa Samora una historia ndefu sana pia. Uwanja huu awali ulikuwa ukiitwa Gymkhana, ulikuwa uwanja wa michezo wa Wahindi. Labda niwaeleze jinsi eneo hilo la kiwanja lilivyokuwa enzi hizo, pale ulipo mlango mkuu wa kuingilia Samora ndipo pia ulikuwa mlango wa kuingilia eneo la klabu. Jengo lililo kushoto ndio jengo asili la klabu hiyo. Ndani kulikuwa na ukumbi ambao waliutumia kwa maonyesho na michezo mbalimbali ya ndani. Lilipo jukwaa kuu la uwanja wa Samotra kulikuwa na viwanja vya mchezo wa tenisi, na kulikuwa ni mikalitusi (miti ulaya) mingi kuzungukia eneo hilo. Katika mipaka ya uwanja kulipandwa miti ya minyaa ikiwa imefuatia mulemule ambamo kumejengwa ukuta wa kuzunguka uwanja siku hizi. Baadae eneo hili lilichukuliwa na serikali na kujengwa shule ya kwanza ya Middle School. Katika zama hizo ilikuwa wanafunzi wa Iringa mjini walikuwa wanasoma Goverment Native School (Mlandege) kuanzania darasa la kwanza mpaka la nne, kisha wanaochaguliwa kuendelea ililazimika waende kuijiunga darasa la tano na kuendelea kwenye shule ya serikali ya Kalenga Middle School, ambayo ilikuwa na darasa la tano mpaka la nane. Hivyo wakati huohuo wa ukoloni wa Waingereza ikaamuliwa kujenga shule ya darasa la tano mpaka la nane pale mjini, ambayo ndiyo ilijengwa ulipo sasa uwanja wa Samora. Ilikuwa ukiingia getini tu kushoto palikuwa  na kajumba kadogo kalikokuwa ofisi ya kwanza ya Headmaster, baba mzazi wa Mama Anna Abdallah alikuwa Headmaster wa kwanza wa shule ile, na nyumba ya mwalimu mkuu ya kwanza ilikuwa upande wa pili wa barabara ikiangaliana na makaburi ya Mlandege, kwa sasa kuna mashine za kusaga unga. Kama nilivyosema mwanzo jengo lililo kushoto mwa lango la kuingilia uwanja wa Samora mpaka mwanzoni lilipokabidhiwa shule lilikuwa ukumbi wa shule na kutumika na wanafunzi wa shule ya Goverment na shule hiyo ya Iringa MIddle School. Goverment School ilikuja kuitwa Mlandege Primary na Iringa Middle School ilikuja kuitwa Mshindo Primary School enzi za uhai wake. Ukumbi huu pamoja ya kuwa ukumbi wa kuonyesha vipaji vya wanafunzi pia ulikuwa ukumbi wa wasanii mbalimbali kuja kuonyesha sanaa zao, enzi hizo wasanii wa mazingaombwe walikuwa wakipendwa sana na wanafunzi. Pia ukumbi huo ukawa sehemu ya kujifunzia ufundi seremala kwa wanafunzi wa ile Middle School, na sehemu ile iliitwa jina la ‘ workshop’. shule ilikuwa pia na jiko  kubwa lilijengwa hapo kwani wanafunzi walikuwa wakipata chakula cha mchana hapohapo shuleni, kila Alhamisi walipewa kikombe cha karanga mbichi. Awali shule ilikuwa ya wavulana tu, lakini baadae wakajiunga wasichana si zaidi ya wanne, akiwemo mmoja aliyeitwa Lidya, simkumbuki hata sura lakini nakumbuka nilimpenda sana na wakati huo nilikuwa naamini kuwa nikiwa mkubwa ningekuja kumuoa!!!.  Nyuma ya shule kulikuwa na pori lakini kulikuwa na njia nyembamba ambayo ilikuwa ikielekea kilabu cha Kijiweni, mahala pekee ambapo serikali ya mkoloni ilikuwa ikiruhusu wenyeji kunywa pombe zao za kienyeji. Ni wakati huohuo ambapo mmoja wa wasichana hawa waliojiunga na hii shule aliamua kujinyonga nyuma kidogo ya shule, ilisemekana alijigundua ana mimba, miaka hiyo msichana kupata mimba shuleni ilikuwa aibu kubwa sana, akaona heri afe. Ni kati ya vitu vilivyonishtua sana utotoni kumuona mtu akining’inia kwenye mti, na ni utundu wa kwenda porini nyuma ya shule kulikosababisha nimuone huyo msichana na ndio nikakimbilia nyumbani kueleza.Middle School ilikuwa na timu nzuri sana ya mpira wa miguu na ilikuwa ikichuana na timu nyingine zilizokuweko Iringa mjini bila matatizo, na ilikuwa na vikombe kadhaa vilivyokuwa vikikaa ofisini kwa mwalimu mkuu, ambae kama mnakumbuka nilisema alikuwa baba yangu. Kati ya timu ninazozikumbuka ni Boni na Relwe. Hii Boni ilikuwa ni kifupi cha Born Town, ilikuwa timu ya watemi wa Iringa wakati huo. Jezi zao zilikuwa mashati meusi, wakifungwa walikuwa wanaweza kukatisha mchezo wakati wowote kwa mtemi mmoja kuweka mpira kwapani na kuondoka nao uwanjani. Kulikuwa na ndugu wa ukoo wa Kibasila ndio walikuwa kati ya watemi wa wakati huo. Timu ya Relwe ilikuwa ya shirika la usafirishaji la East African Railways and Harbours. Majirani ninao wakumbuka ni kina Duma waliokuwa na nyumba jirani na lango kuu la Samora, hawa nawakumbuka zaidi kwa kuwa walikuwa na ndugu yao anajua kupiga gitaa kwa hiyo kuna siku walikuwa wakikusanyika na kuimba nyimbo za jive za Afrika ya Kusini wakati ndugu yao akipiga gitaa, mimi nilikuwa nabaki kuduwaa na ninakumbuka sana mpaka leo. Jirani sana na kwetu alikuwa anaishi Mwalim Lea Lupembe na mumewe Joseph Lupembe. Mama Lea baadae alikuja kuwa Katibu Mkuu wa UWT. Pia kulikuweko Mkikuyu mmoja Joseph Karuli ambaye alikuwa na duka jirani na shule. Maduka mengi pale Mshindo yalikuwa ni ya Waarabu. Kati ya wazee maarufu alikuweko Mzee Pangras Mkwawa huyu alikuwa mtoto wa Chifu Mkwawa alikuwa na nyumba yake palepale Mshindo, yeye alikuwa na punda kadhaa na gari lilikuwa likivutwa na punda, siku akiamua kulitembeza ilikuwa ni siku ya kushangilia. Mzee Pangras pia alikuwa akiuza matunda kama mifudu na misasati, nilikuwa naenda kwakwe na kumsikiliza akipiga ligombo lake na mwisho kupewa matunda yale bure,  Jirani yake walikuwa wakiishi akina Nindi. Hapo kulikuwa na rafiki yangu anaitwa Dokta, hilo lilikuwa ndio jina lake. Kwa ujumla kipindi hicho nilikuwa nakiona ni kitulivu pengine kwa sababu akili zilikuwa bado za kitoto nilikuwa nafurahi tu maisha.Baada ya kuisoma hii mzee aliyekuweko ameongezea haya…..ITAENDELEA

Categories: Iringa, Uncategorized

4 replies

  1. Home sweet home ….Ninejifunza mengi ya mkoani kwangu …ubarikiwe mzee Kitime….Salma Omary Sosovele

    Like

  2. Umenikumbusha sana historia hii. Napata kurejesha kumbukumbu na picha halisi za mji wa Iringa. Mimi nilikuwa mwenyeji wa Tosamaganga mwanafunzi wa primary baadaye Sekondari, tulikuwa tukija mjini kwa miguu siku za weekend. Tukirudi jioni tulikuwa tukibeba bagia, sukari-gulu na matunda ya mjini.
    Baadhi ya walimu uliowataja niliwafahamu kama: Mama Kalinga{Marehemu mama mdogo}, Mwalimu Kalinga(mme), Mwalimu Luhanga, alikuwepo pia Mwl. Pancras{Mtelefu}nk

    Like

Leave a reply to rhumbatz Cancel reply