LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 6


Ukipita miji mingi siku hizi unaweza kudhani hakuna watoto. Jamii haiwekezi kwenye sehemu za watoto katika miji yao, utamaduni huu unabebwa na wazazi pia, mzazi anakuwa na kiwanja kikubwa na ana watoto kadhaa lakini akijenga nyumba yake nzuri, sehemu iliyobaki hawazii sehemu ya kucheza watoto wake, bali anaijaza sehemu hiyo na shughuli mbali mbali za biashara, watoto wake mwenyewe wanalazimika kucheza mitaani mahala pasipo salama. Jambo la ajabu ni kuwa wakati wa ukoloni ni miaka ya mwanzo wa Uhuru wa nchi yetu, miji ilitenga sehemu maalumu kwa ajili ya watoto. Watoto tulikuwa wachache kuliko siku hizi lakini tulikuwa na sehemu nyingi na salama za kucheza. Katika mji wa Iringa nakumbuka sehemu tatu ambazo zilitengwa na kuhudumiwa na serikali kwa ajili ya watoto. Sehemu ya nne ilikuwa ikimilikiwa na Relwe.

Uwanja ambao sasa unaitwa Garden, ulikuwa ndio kiwanja kikubwa cha umma tokea zama za Mjerumani. Mechi za soka, mikutano na sherehe mbalimbali zilifanyika hapa. Uwanja huu ulioitwa uwanja wa Bomani, ndipo zilipofanyika sherehe za Uhuru mwaka 1961, na kulijengwa mnara wa Uhuru ambao zamani ulikuwa ukitoa maji juu kabisa na kuwa na vibomba vidogo pembeni, ambavyo tulitumia kunywea maji hayo, ulikuwa ni alama ya tukio hili muhimu kwa wakazi wa Iringa. Katika uwanja huu palijengwa mabembea na michezo mingine ya watoto hivyo kutufanya tuwe muda mwingi katika eneo hilo wakati wa utoto wetu, Wengine wakibembea wengine wakipanda mabomba maalumu kwa watoto, wakitereza katika mabati yaliyotengenezwa kwa ajili hiyo basi watoto tulikuwa na raha kwa gharama ya kodi za wazazi wetu. Maeneo ya michezo ya watoto yalikuwa pia katikati ya kota za Mlandege na sehemu ya tatu ilikuwa uwanja mkabala na ukumbi wa Community Center au Welfare Center maarufu kama Olofea. Hapa Olofea pamoja na kuwa na uwanja nje wenye mabembea (Uwanja huo sasa umegeuzwa soko la mitumba) ndani ya ukumbi wa Olofea kulikuwa na shughuli nyingi za watoto. Kulikuwa na kituo cha Maendeleo ya kina mama kikiongozwa na aliyeitwa Mama Maendeleo, hapa walifundishwa yale ambayo siku hizi yanaitwa ujasilia mali. Walijifunza kushona kufuma, kupika na kadhalika na walikuwa wakifanya maonyesho na kuuza bidhaa zao. Nawakumbuka mama maendeleo Mama Kitime na rafiki yake Biti Yusufu. Wakati akina mama wanaendelea na elimu yao watoto wadogo walikuwa wakifundishwa kusoma na kuandika na Mwalimu Mwambola. Watoto wakubwa kidogo waliendelea na michezo mingine ikiwemo table tennis, boxing, bao , drafti na kadhalika. Mchana kulikuwa na vikundi vya sanaa kama kwaya na michezo ya kuigiza. Siku nyingine nyakati za usiku kulikuwa na dansi katika ukumbi huu. Ilikuwa Community Center kwa maana yake halisi. Huu uwanja nje ya Olofea ulikuwa pia ndio uwanja wa kuonyeshea sinema za bure. Kulikuwa na kampuni kutoka Kenya ilikuwa inapita kila tarehe 13 ya mwezi kutanganza biashara na kuonyesha sinema. Bidhaa zilizotangazwa zilikuwa sigara Sportsman, kuna mpiga trombone mmoja aliyeitwa Bwana Msafiri ndie aliyekuwa akipuliza trombone lake na kuimba wimbo wa Bwana Msafiri, Maneno ya wimbo huo yalikuwa hivi; Bwana Msafiri mi nasema, Hakuna sigara inayokufaa, Ila Sportsman King size, Ile yenye kichungiii. Kulikuwa na matangazo ya Blue Band, sabuni ya kufulia Surf, Cocacola na kadhalika. Sinema zilizokuwa zikionyeshwa zilikuwa ni za Cowboys na mara nyingine sinema za kuchekesha za Charlie Chaplin , na mara nyingine wachekeshaji wenzie Lawrence na Hardy, ambao tuliwafahamu zaidi kwa majina ya Chale Ndute na Chale Mbwambwambwa, mmoja alikuwa mwembamba na mwingine mnene. Wale wapenzi wa sinema za Macowboy tuliwafahamu kwa majina, kati ya waliokuwa maarufu walikuwa akina Tex Ritter, Roy Rodger, John Wayne na Gene Autry. Nyakati hizohizo kuliingizwa ‘chewing gum ambazo ndani yake kulikuwa na picha za wacheza sinema maarufu wakati huo. tulinunua sana pipi hizo ili kupata picha za mastaa wetu. Uwanja maarufu wa mikutano wa Mwembetogwa ulikuwa mali ya Relwe na hapo pia palitengwa maalumu kwa ajili ya watoto. Kulikuwa na mabembea na michezo mingine kwa ajili ya watoto wa wafanyakazi wa Relwe…………

Categories: Iringa

2 replies

Leave a reply to Anonymous Cancel reply