LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 7


mwandiko iringa
kitabu cha mwandiko

Naikumbuka vyema sana siku ya kwanza baba aliponipeleka shule kwenda kuanza darasa la kwanza. Wakati huo baba alikuwa Headmaster wa Iringa Middle School, shule ambayo ilikuwa ulipo sasa uwanja wa Samora, tulitembea kwa miguu tuu mpaka Goverment Primary School, shule ambayo sasa inaitwa Shule ya Msingi Mlandege. Hapakuwa na nyumba nyingi jirani na shule hizi, eneo kati ya shule hizi lilikuwa wazi kabisa, japo eneo lote ambalo sasa ni uwanja wa Samora lilikuwa limezungushiwa wigo wa miti ya minyaa. Miti hii hutoa utomvu mweupe ambao ulikuwa ukitumika kama gundi, lakini ilikuwa ni miti ya kujichunga sana kwani tone likudondokea jichoni tuliambiwa unaweza kuwa kipofu na dawa yake ilikuwa lazima udondoshewe matone ya ziwa ya mama jichoni!! 
Tulipofika shuleni baba akanipeleka moja kwa moja kwa Headteacher Mwalimu George Nyakunga. Siku hizo mwalimu mkuu wa shule iliyoanzia darasa la kwanza mpaka la nne aliitwa Headteacher na yule aliyekuwa mwalimu mkuu wa shule ya darasa la tano mpaka la nane aliitwa Headmaster, Baba na mwalimu mwenzie walikuwa marafiki hivyo waliendelea kuzungumza yao wakati mimi nikishangaa mazingira mapya. Mwalimu George alikuwa muwindaji na mara nyingi akitoka kuwinda alikuwa akituletea nyama nyumbani. Baba aliondoka na Mwalimu George akanipeleka darasani, darasa la 1B. Mwalimu wa darasa alikuwa mwalimu Chitigo, kama kumbukumbu zangu si mbaya alikuwa akiitwa Michael. Nilipoingia darasani, mwalimu alinitambulisha kwa wenzangu, kisha akafungua kabati lililojaa vitabu na daftari na kunikabidhi daftari mbili mpya, daftari la hesabu na daftari la mwandiko.    Madaftari hayo ukubwa wake yalikuwa ni nusu ya ukubwa wa daftari za siku hizi. Pamoja na daftari hizo nikapewa na kitabu cha kujifunza kusoma kiliitwa “Someni kwa furaha 1B”, nikawa mwanafunzi rasmi. Shule ilianza mambo yalikuwa mengi. 1+1, 1+2, aeiou, ba be bi bo bu, taa na saa, kaka ana saa na mengine mengi, pole pole vikaingia kichwani. Viboko vilikuweko kama kawaida. Furaha ilikuwa aidha wakati Mwalimu Chitigo alipotuambia, ni saa ya kuimba sasa na kuanza kutufundisha nyimbo kama Baba Paka, au Ngo ngo twaingilia, nyimbo ambazo sitazisahau, au aliposema “Sasa namihadithieni hadithi, hadithi hadithi” kwa lafudhi yake ya Ki Tanga..tukishajibu “Nam taim hadithi njoo”. Anaanza kutupeleka mbali, siku nyingine hadithi za sungura mjanja mara hadithi za mazimwi, ilikuwa kama kuangalia sinema vile. Mwenzetu moja bingwa wa kukojoa darasani alikuwa akitumia muda huu kukatiza hadithi kwa sauti ya kojo likitiririka. Hapo atasimamishwa na kutolewa nje ya darasa huku analia.  Kulikuwa na sababu watoto walikuwa wanakojoa darasani, nje kulikuwa kuna tisha. Kulikuwa na hadithi kuwa kwenye choo kimoja cha wasichana kuna jini, sasa ili ufike choo cha wavulana ililazimu upite choo kilichosemekana kina jini, hiyo ilikuwa inatisha mno, ikawa heri ukojoe hapo hapo darasani. Siku moja Mwalimu George alituita wanafunzi wote na kututangazia kuwa kuna mganga kaja kuchinja mbuzi kwenye choo cha wasichana na jini limekimbia. Naona alitumia saikolojia kutuondoa woga. Maisha yakaendelea. Shule yetu ilikuwa na madarasa manne yote yana A na B. Darasa la kwanza na la pili tulikuwa tunabadilisha vipindi kwa mlio wa pipa moja lilokuwa limetengenezwa kwa mbao. Wakubwa, yaani darasa la tatu na la nne walikuwa wanatumia kengele. Tulikuwa tunaanza vipindi saa nne mpaka saa nane. Pipa likigonga saa nane….kelele za nyumbaniiiii zilisikika tukiwa tunatimua mbio kuelekea makwetu na kaptura zetu za kaki stakapoti….unajua stakapoti ni nini? INAENDELEAAAA

Categories: Iringa, Uncategorized

1 reply

Leave a comment