LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 10


St Michael &St George School mwaka 1959

Miaka ya 1963 na 1964 wakati naishi Barabara Mbili pale Makorongoni, eneo linaloitwa Mkwawa siku hizi halikuwa na jina hilo. Ukitoka Makorongoni uliingia eneo la Mwembetogwa, kisha Ilala A halafu Ilala B, baada ya hapo ndipo likaja eneo la shule ya wazungu ya St George and St Michael. Kihistoria shule hii ilianzia Kongwa mwaka 1951, ilikuwa shule maalum kwa watoto wa wazungu waliokuja kufanya kazi Tanganyika, mwaka 1958 shule hiyo ikahamia Iringa na kuitwa jina hilo.January 1961 ndipo ilipoingiza wanafunzi wa kwanza mchanganyiko, Waafrika 21 na wahindi 20.
Eneo la St George na St Michael lilikuwa na umuhimu wake kwetu sie watoto wa Iringa, kwanza nje ya uwanja wa shule walikuwa na jalala ambalo tulikuwa tukienda kufukua fukua kila tulipopata nafasi ili kupata vitu vya kizungu. Vitabu, madaftari, vitu vya kuchezea, japokuwa vilikuwa vibovu vimeshatupwa kwetu ilikuwa mali sana. Hatukuwa na tabia ya kuingia eneo la shule maana tulikuwa na uwoga fulani wa kukamatwa na wazungu. Kuna wenzetu tulisoma nao ambao wazazi wao walikuwa wakifanya kazi pale shuleni lakini hata wao kota zao zilikuwa nje ya eneo la shule. Mmoja wa watoto hao kwa sasa ni Profesa mstaafu, kweli tumetoka mbali. Barabara ya kutoka jengo la Hans Poppe mpaka mwisho wa Ilala ilikuwa ya vumbi. Kuanzia hapo unashuka kuelekea yalipo makaburi ya Makanyagio mpaka kwenye lango la kuingia shule ya St George kulikuwa na kipande kifupi cha lami. Kipande hicho kilikuwa muhimu sana kwani hapo ndipo tulitumia masaa mengi Jumamosi na Jumapili tukiendesha magari yetu ya magurudumu ya beringi, enzi hizo magari yalikuwa machache sana hakukuweko na tatizo kucheza katikati ya barabara ya lami. Tulicheza sana na magari hayo hapo, tukichoka tuliyabeba magari yetu kichwani na kurudi makwetu, ila wengine walivuka eneo la shule na kuelekea Itamba ambako kulikuwa na miembe mingi.

Gari la beringi

Inawezekana kuwa miembe hii ilipandwa na Wanyamwezi wa kwanza kuishi eneo hili, kwani katika historia ya kuanzishwa kwa mji wa Iringa, inasemekana wageni Wanyamwezi walienda kuishi sehemu za Itamba. Sisi kazi yetu kubwa Itamba ilikuwa kwenda kuiba embe na zambarau. Wenyeji walijaribu sana kutukamata watutie adabu, walitengeneza mitego ya kamba ambapo ukijikwaa makopo yanalia na kuwashtua mbwa waliotufukuza. Tulifukuzwa na mbwa mara nyingi lakini tulirudia tena na tena kuiba embe, hatukujali kama zimeiva au mbichi zote kwetu zililiwa tu. Sikumbuki hadithi ya mtu yoyote kuwahi kuumwa na mbwa wale, ingawaje tena mara kwa mara watoto wengine walikutwa juu ya miti na kuzingirwa na mbwa, kwani kwa kawaida tulienda kwa jozi, mwingine anapanda mti kuangua mwingine anakuwa chini kuokota, huyu wa chini ilikuwa rahisi kukimbia mara atakaposikia sauti za mbwa, lakini aliyoko mtini kazi kwake,lakini hadithi za uhodari wa kuruka toka juu ya mti na kutimua mbio kukwepa mbwa zilikuwa za kawaida sana.

Kama kawaida kila mtaa una mlevi wake, pale Barabara Mbili mlevi wetu aliitwa Baba Beni, Sikuwahi kumuona huyo Beni wala sikumbuki kama nilikufahamu alikoishi Baba Beni, lakini kila akipita mtaani kwetu alikuwa kisha lewa chakali hata kutembea kwake ni shida. Watoto tulimzingira na kuanza kumuita, ‘Baba Benii’, sijui kwanini hakulipenda jina hilo alikuwa nakasirika na kututukana matusi mazito na kujaribu kutufukuza lakini ulevi kila mara ulikuwa unamzidi.
Pombe za kienyeji zilikuwa zinaruhusiwa kuuzwa Kijiweni tu. Kijiweni ilikuwa sehemu maalum ambayo serikali ya mkoloni ilijenga kwa ajili ya kuuza pombe hizo. Lakini kama ilivyokawaida akina mama wengine walikuwa wakipika na kuuza kwa wizi katika nyumba zao. Polisi mmoja ambaye alikuwa anajiita special constable Msungu sasa sijui ni cheo au sifa alikuwa maarufu sana wa kukamata akina mama waliokuwa wakiuza pombe majumbani mwao, ilidaiwa siku moja aliingia nyumba moja kukamata pombe, wateja wakamkamata na kumfunga kamba kichwa chini miguu juu kuelekea kwenye shimo la choo, baada ya hapo ukali wote ukaisha. Tulikuwa tukimuogopa kwa kuwa hatukuwahi kumuona anacheka, na tuliambiwa akikukamata Mwamsungu lazima ufungwe. Wakati huu polisi walikuwa wakivaa shati za kijivu na suruali ya kaki.
Makorongoni nilikuwa naishi na Babu yangu, alikuwa ananipenda sana kwani alikuwa akishiriki vitu vyangu kwa upendo hata vile ambavyo nikikumbuka leo naona ulikuwa utoto wa kupindukia. Kwa mfano pale mtaani watoto wote tulikuwa tukihadithiana kuwa tajiri mmoja wa zamani Mzee Salehe Masasi alitajirika baada ya kuokota kipande cha almasi. Sasa siku moja nilikuwa nacheza nje na wenzangu nikaona kipande cha jiwe kinang’aa, nilikiokota na kwaambia wenzangu nimeokota almasi, nikakimbilia kwa babu na kumwambia kuwa nimeokota almasi. Alikiangalia kile kipande kisha akanambia kwa sauti ya kisirisiri, ‘Ee bwana twende tukafiche kwenye kabati nyuma ya vitabu’, babu alikuwa na vitabu vingi maana alikuwa mwalimu. Baada ya kuficha ile ‘almasi’ kwa kweli nilikuwa nina kuwa sasa umasikini baibai na mimi ningenunua magari mengi kama ya Masasi. Baada ya kama wiki babu akaniita chumbani kwake akanionyesha jiwe kubwa lililokuwa kama kioo hivi, akanambia kwa sauti kama vile na yeye ndio kapata habari muda ule ule, ‘E bwana e kumbe bwana lile jiwe sio almasi ni mica’, mica ni madini fulani hayana thamani kubwa na kakipande kangu nilikookota kalikuwa na ukubwa wa kucha tu, basi ndoto yangu ya utajiri ikapotea kwa muda.
Nyumba za zamani zilikuwa zinaezekwa kwa vipande vya madebe. Debe lilichukuliwa na kukatwa kisha kunyooshwa na kuwa kama kipande cha bati, hivyo yakiwa mengi yaliweza kuezeka vizuri nyumba nzima, nyumba ya babu ilikuwa imeezekwa kwa madebe. Shangazi yangu alivyopata uwezo akanunua bati na nyumba ikaezekwa bati na yale madebe yaliyotolewa juu yakakusanywa na kuwekwa pembeni. Siku moja nikapata wazo la kutengeneza ndege. Bati zilikuweko za kutosha, hivyo nikamuomba babu zile bati nitengeneze ndege. Bila kuniangusha nae akachangamkia sana mradi wa kutengeneza ndege, akaniuliza nilichokuwa nataka, nikamwambia nahitaji nyundo na misumari, hakika bila uvivu babu alienda kununua nyundo na misumari akanikabidhi. Nakumbuka mama yangu alicheka sana siku hiyo na kesho yake wakati nikigonga mabati najitahidi kutengeneza ndege. Babu alikuwa akipita mara kwa mara yuko ‘serious’ ananipa pole kwa kazi, bahati mbaya misumari ile ilikuwa haishiki vizuri nikashindwa kutengeneza ndege yangu mwenyewe mwaka 1963………ITAENDELEA

Categories: Iringa, Uncategorized

4 replies

  1. Vya kale ni dhahabu, hata debe zamani zilikuwa imara sana, kuna bwana mmoja injinia pale Iringa alinunua nyumba ya zamani akaivunja na kujenga mpya ilipofika wakati wa kuezeka alizitathmini zile bati za debe akaona ni imara akazirudishia zilezile kwenye nyumba mpya ya kisasa akapiga na rangi ikapendeza sana.

    Like

  2. Asante sana kwa kumbukumbu historia ya Iringa LEO NIMEKUMBUKA…Nilisoma Iringa Govt Primary School kuanzia mwaka 1959 mpaka 1963. Nilikuwa darasa B. Walimu wote uliowataja na wanafuzi nawakumbuka sana. Tumetoka mbali tunamshukuru Mungu.

    Like

Leave a reply to Michael Myinga Cancel reply