
Nilikuwa na miaka minne nilipokwenda kuishi kwa bibi kwa muda. Wazazi wangu walikuwa wameenda Dar es Salaam kwa ajili ya likizo wakaenda na mdogo wetu Eva ambaye alikuwa na umri wa miezi kadhaa. Kumbukumbu za wakati huo zipo nyingi kwa kuwa baba yangu aliyekuwa mpiga gitaa mzuri alichukua nafasi hii kwenda TBC (Tanganyika Broadcasting Corp) na kurekodi nyimbo kadhaa, mama nae alirekodi kipindi akielezea taratibu za ndoa za Kihehe. Hivyo basi mimi nilipelekwa kwa Bibi mzaa mama aliyekuwa akiishi kijiji cha Msombwe, kijiji kilicho kilomita chache kutoka Tosamaganga. Kuna mambo machache nakumbuka kuhusu muda niliokuwa na bibi. Kwanza ilikuwa ratiba ya kila siku, Bibi alikuwa akiamka kwa mlio wa jogoo. Akiamka hapo alikuwa anawasha moto na kupasha moto chakula alichokuwa kapika jana yake, kisha niliamshwa alfajiri hiyohiyo. Kulikuwa na kitanda kimoja cha kamba ambacho kilikuwa cha bibi, mimi nililala chini kwenye ngozi, kulikuwa hakuna kudeka kiasi hicho kwa bibi, na baada ya kunawa uso tulielekea shambani, kukiwa kwa kweli bado giza. Shamba halikuwa mbali na nyumba ya bibi. Mimi nilikaa pembeni ya shamba na bibi alianza kulima. Jua lilipoanza kutoka bibi alikuja na kufungua vile vyakula, siku nyingine ilikuwa viazi vitamu vilivyocheshwa au kuokwa, mara nyingine ugali na maharage au mboga za majani na ndivyo kilikuwa kifungua kinywa. Bibi aliendelea tena kulima mpaka kama saa nne au tano kisha tulirudi nyumbani, lakini njiani tulikota kuni nami nikabebeshwa kamzigo kangu. Baada ya kufika nyumbani zilianza shughuli za kutayarisha chakula, maji tulifuata kwenye kisima kilichokuwa kwenye makorongo yalikuwa jirani na nyumbani kwa bibi, maji safi matamu na ya baridi. Baada ya hapo ndipo nikawa huru kucheza aua kuwafuata watoto wa nyumba za jirani ambao nao kimsingi ratiba yao ilikuwa kama yangu.
Siku moja nikaamua kutoroka kurudi Iringa mjini. Mtoto wa miaka minne nataka kuanza safari ya kutoka Tosamaganga hadi Iringa mjini.

Kwa wenyeji wa Msombwe wanakufahamu kwa Buruda Fabian wenyewe tulikuwa tunamuita Buluda Fyabian, hapa kilikuwa kituo cha mambo mengi lakini hasa kulikuwa na shamba la miwa na kiwanda cha kutengeneza sukari guru, kwenye miaka ya 80 kilikuwa kituo kikubwa cha biashara ya mitumba. Haya mie mtoro nilitoroka kwa bibi mpaka nikaweza kufika hapa, baada ya hapo nikaanza kufwata barabara kuelekea Iringa. Sikufika hata kilomita 2 nikakutana na Padri Yorda akiwa katika gari lake mwenyewe alikuwa analiita simba. Padri Yolda alikuwa ananifahamu mimi na familia yangu yote, akaniuliza naenda wapi nikamjibu naenda kwa baba Iringa, akaniambia nipande gari twende, safari yetu ikaishia kwa bibi. Bibi hakuwa mtu wa mchezo mchezo, alinichapa na fimbo sikutoroka tena. Juzijuzi nilikutana na padri Yolda nikamkumbusha habari hiyo hakumbuki, akanikumbusha kuwa sasa ana miaka 93 ameona mengi sana. Gari ya Padri Yolda aliyoiita simba ilikuwa Peugot 203 ambayo ilikuwa na sanamu ya kichwa cha simba mbele kabisa.
Bibi yangu mzaa mama alikuwa anaitwa Costanzia Sebilahimu, jina lake maarufu alikuwa akiitwa Mbeve. Baba yake alikuwa Myao, na kwa kadri ya hadithi alizokuwa akituhadithia baba yake alikuwa akiishi Iringa mjini enzi hizo za Mjerumani. Jina la baba yake lilikuwa Ibrahim, na kwa kuwa hakuwa na jina jingine, hilo likageuka jina la ukoo wa bibi. Kama ilivyo kawaida ya Wahehe, jina la ukoo kwa wanaume linaanza na Mwa na kwa wanawake jina hilohilo linaanza na Se. Sasa jina Ibrahimu gumu kwa Wahehe hivyo akaitwa maisha yake yote Sebilahimu. Alikuwa na kaka yake ambaye tulimfahamu kwa jina la Chuma cha moto, alikuwa na hadithi zake tata nyingi sana pia. Bibi aliwahi kutuhadithia mambo yalivyokuwa siku ambapo Wajerumani walikuwa wakiwanyonga wenye makosa pale eneo linaloitwa sasa Kitanzini. Siku za kunyonga zilikuwa zikitangazwa na ili watu wengi wahudhurie, nadhani nia ilikuwa kutisha watu waogope kumpinga Mjerumani. Kitu cha ajabu ni kuwa siku hiyo ilikuwa kama sherehe fulani, kwa maelezo ya bibi yangu ambaye asikio yake yalikuwa yametobolewa matundu makubwa, siku za kinyongo wao walivaa makaratazi ya kung’aa masikioni ili wapendeze. Bibi alikuja kuolewa na Ananias Kaberege aliyekuwa Mbena kutoka Lupembe Njombe ambaye alihamia Tosamaganga. Wakapata watoto sita, wasichana watatu na wavulana watatu, mama yangu alikuwa watatu kuzaliwa. Mtoto wa kwanza alifariki wakati hata mama bado ni msichana, ila wengine wote niliwaona na walihusika katika maisha yangu kwa namna moja au nyingine.
Kwa maelezo ya mama, mara ya kwanza wao kwenda Lupembe ilikuwa wakati yeye bado mdogo, walitembea kwa miguu kutoka Tosamaganga mpaka Lupembe, safari ya wiki mbili, lazima ilikuwa kabla ya mwaka 1947, kwani ndio mwaka Babu Anania alipofariki kutokana na kidonda kikubwa mguuni. Bibi alikuwa katika sehemu kubwa ya maisha yetu, alikuwa akishikilia sana sala na ulipokuwa nae ilikuwa uelewe utalazimika kushiriki sala zote za siku nzima. Asubuhi, saa sita mchana, saa kumi na mbili jioni na sala ya jioni kabla ya kulala.

Bado huwa nashangazwa na upendo aliokuwa nao Bibi, sisi tuliishi mjini, siku akitoka kijijini kuja kututembelea alikuwa lazima aje na kapu kubwa lilisheni, mahindi ya kuchemsha viazi vitamu vilivyochemshwa, kuku, matunda ya porini, mzigo mzito haswa, na anakuwa katembea nao mbali sana kichwani, kwani magari yalikuwa machache hivyo kuna siku alikuwa anatembea na huo mzigo kutoka Tosamaganga hadi Iringa mjini kupitia Mapogolo.
Bibi alikuwa akipenda sana tumhadithie hadithi za picha zilizokuwa zikiendelea kwenye magazeti yaliyotamba sana ya Film na Boom. Nyota wa gazeti la Film alikuwa Lance Spearman na nyota wa gazeti la Boom alikuwa Fearless Fang.Haya yalikuwa magazeti ya picha ambayo wakati huo tuliyapata kila wiki. Raha ya bibi, aliyekuwa akitamka Fearless Fang kuwa Fyalesi Fwengi ilikuwa ni kusimuliwa kilichokuwa kikiendelea kwenye hadithi hizi. Na wajukuu hatukumtupa kwa hilo. Bibi alikuja fariki 1987 akazikwa Tosamaganga eneo jirani na alipozikwa mumewe 1947…..ITAENDELEEEEA TU
Categories: Iringa, Uncategorized
asante sana kwa kumbukumbu mzeee
LikeLike