LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 13


Mjomba wangu Thadei alikuwa mdogo wa mwisho wa mama, baada ya mama kuolewa, mjomba wangu alianza kuishi na wazazi wangu, nimezaliwa na mpaka napata akili mjomba wangu alikuwa pembeni yangu. Kuna watu walikuwa wakidhani alikuwa kaka yangu. Mwaka 1961 alipata kazi ya kuuza magazeti katika duka la Iringa Printers, duka maarufu wakati huo kwa kuuza vitabu na magazeti, duka hili mpaka sasa linauza vitabu, na vifaa vya shule na maofisi. Duka likampa baiskeli ambayo ilikuwa na kapu mbele na hivyo akawa anazunguka mjini akiuza magazeti. Alipopata hiyo kazi mama akamwambia lazima ahame akajitegemee. Wakati huo tunaishi nyumba ya Headmaster wa Middle School ambayo nilisema ilikuwa katika eneo ambalo sasa ni uwanja wa Samora. Mjomba alipata nyumba jirani na nyumba ya mzee muhimu sana katika historia ya Iringa mzee Juma Kayugwa. Kwa vile haikuwa mbali na nyumbani nilikuwa naenda kumtembelea. Chumba chake kilikuwa na kitanda cha chuma maarufu kwa jina la Banco, stovu ya Primus na visufuria viwili vitatu. Siku hizi pamekuwa ni mahala pa kuuza frame za milango na madirisha ya alminium.

Stovu ya Primus


Nilikuwa napenda sana kumtembelea kwani nilikuwa naona anafaidi sana alipokuwa akichemsha viazi mviringo (viazi Ulaya) na mboga zake kachumbari. Utengenezaji wa kachumbari siku hizo ulikuwa tofauti na siku hizi. Vitunguu vilikatwakatwa na nyanya zikakatwa zikachanganywa halafu zikachanganywa na pilipili ya unga, kisha kuanikwa juani. Sijui ni kule kuanikwa juani lakini kachumbari ile ilikuwa tamu sana kuliko siku hizi. Au pengine kwa sababu nyanya za siku hizi zinatumia madawa mengi shambani labda. Nilikuwa nawaza kuwa kuwa na mimi nikiwa mkubwa ntakuwa napika viazi namna ileile na kachumbari yangu pembeni, hakika nilikuwa nikiona yale ndio maisha.
Mjomba alijiendeleza kupitia kozi zilizokuwa zikitolewa kwa njia ya posta kupitia shule iliyokuwa ikiitwa British Tutorial Course, akaweza kupata vyeti vilivyomuwezesha kujiunga na Shirika la Posta. Enzi hizo likiitwa East Africa Posts and Telecommunications, makao yake makuu yalikuwa Nairobi. Muda si mrefu akaenda Nairobi kwa ajili ya mafunzo ya kazi yake, aliporudi akawa anafanya kazi posta pale Iringa, nikaweza kupata bahati ya kuingia mle posta nikaona wanavyoweka barua kwenye masanduku na hasa kubwa niliona maopereta wa simu walivyokuwa wakifanya kazi. Labda nieleze hapa kuwa zamani ilikuwa lazima kila simu iwe na waya unayoiunganisha na posta. Ukitaka kumpigia mtu simu lazima upige kwa opereta na kumueleza namba unayoitaka, yeye ndie anakuunganisha na namba ile, kama umepiga kwenye kibanda cha simu unaelezwa fedha ya kulipa, unatumbukiza kwenye tundu maalumu fedha unayotakiwa kulipa kisha unaunganishwa uongee.
Mjomba ndie aliyekuwa akifuatilia nyendo zangu kuhakikisha nakwenda kanisani, maana wakati nasoma Consolata Primary, tulikuwa na sheria kuwa wanafunzi wa shule ile lazima tuhudhurie Misa ya 3. Sasa misa ya 3 ilikuwa ndefu toka saa nne mpaka saa sita au saba kutegemea na urefu wa mafundisho, hatukuwa tunapenda kukaa kanisani muda wote ule, na kubwa zaidi, baada ya misa ilikuwa lazima keenda shule kuandika jina daftari la mahudhurio ya misa hiyo. Jumatatu kulikuwa na viboko kwa wakatoliki ambao hawakuhudhuria misa ya 3. Hivyo basi tulikuwa tunashinda porini mpaka dakika za mwisho mwisho ndio tunajitokeza viwanja vya kanisa ili kuandika majina. Sasa mjomba alikuwa akihakikisha naingia kanisani mapema, na nilikuwa sina ujanja wa mkwepa alikuwa ananijua vizuri mno. Urafiki wangu na yeye ulikuja siku za kwenda sinema za bure kwani nisingeweza kwenda bila yeye. Kila tarehe 13 kulikuwa na sinema ya bure katika viwanja vya Olofea. Kwa hiyo ikikaribia siku hiyo ninakuwa mtoto mpole na mnyenyekevu nisimuudhi. Baadae mjomba alihamia Morogoro alipokuwa akirudi likizo alikuwa akituhadithia kuhusu rafiki yake aliyeitwa Juma Kilaza ambaye alikuwa mwanamuziki. kwa kweli nilikuwa namwona mjomba ni mtu mkubwa sana kwani anajuana na mtu anayeimba kwenye redio.
Nilikuwa na miaka 9 nilipowasha swichi ya umeme kwa mara ya kwanza. Siku hiyo nilikuwa nimemtembelea rafiki yangu David Mwaibula ambaye alikuwa akiishi uzunguni. Mwaibula huyuhuy ambaye alikuja leta mabadiliko kwenye Daladala mjini Dar es Salaam. Nyumba ilimokuwa ikiishi familia yao ni kati ya nyumba zinazoangaliana na kanisa la Anglikana lililopo karibu na ‘makaburi ya wazungu’. Wakati huo ilikuwa ngumu kuwakuta watoto wa uswahilini maeneo hayo, familia ya Mwaibula walikuwa na hali nzuri baba yake alikuwa na mabasi kadhaa. Siku hiyo baada ya michezo kadhaa ya hapa na pale, ndipo akanionyesha namna ya kuwasha swichi ya taa ya umeme, jambo ambalo lilinipa mshangao mkubwa wakati huo, nikawa nawasha na kuzima mpaka akanikataza kuwa ntaunguza taa, nilijua anaringa tu kwani inawezekanaje ukaunguza taa kwa kuzima na kuwasha? Nyumbani kwetu kwa babu kulikuwa hakuna umeme, tulikuwa na aina vyanzo vitatu vya mwanga. Jikoni kulikuwa na koroboi, vyumbani tulitumia taa za chemli na babu alikuwa na karabai chumbani mwake.

Kutoka kushoto ni taa ya chemli, karabai na koroboi

Tulikuwa na redio ambayo ilikuwa ikitumia betri. Betri za redio ukubwa wake ulikuwa karibu sawa na ukubwa wa betri ya gari dogo la siku hizi. Na ililazikika kuwa na antena ya nje juu ya paa au mti ili kuweza kushika matangazo. Labda niongeze kitu hapa redio zilikuwa zikilipiwa leseni, baiskeli pia zilikuwa zikilipiwa leseni.
Betri za redio zikiisha zilikuwa zikitupwa nasi tulikuwa tunapata kitu kingine cha kuchezea. Tulikuwa tukizivunja na ndani kulikuwa na vidubwasha vya mkaa ambavyo tulivitumia kucheza michezo mbalimbali, kama eksi, kiboleni na kadhalika. Redio ilikuwa moja ya vitu ambavyo ilikuwa marufuku kugusa. Radio ilifunikwa kitambaa na ilikuwa ikipanguswa vumbi mara kwa mara. Na kwa vile kulikuwa na tabia ya mende kuhamia ndani ya radio, kulikuweko na taratibu ya kuweka dawa ya kuuwa mende ndani ya redio

Kushoto betri ya radio na kulia ni redio Philips……ITAENDELEEEEEEA

Categories: Iringa, Uncategorized

1 reply

  1. KUTOKA KWA MWANASHERIA SHUKURU WA TANGA……Hapo makorongoni barabara mbili ndipo nilipofundishwa kiingereza nikasoma kuanzia Oxford English Course kuanzia Book two hadi Book five. Nikifika shuleni nilikuwa nazungumza na kusoma kiingereza nikistajaabisha watu sana. siku moja niliitwa kusoma kitabu darasa la tano pale Shule ya Consolata Roman catholic primary school humo Darasani alikuwepo marehemu Esteriunus Mahingira baadae ndiye aliyekuwa Msajili wa Makampuni BRELA. Je unajua aliyekuwa mwalimu wangu wa tution hiyo? alikuwa ni babu yako Mr. Kitime wakati huo alikuwa amekwisha retire ambaye na mimi ni babu yangu kiumri na Mwalimu wangu mkuu wa kiingereza.

    Like

Leave a comment