LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 14


Watoto wa Barabara Mbili tulikuwa tunafahamiana maana mtaa wenyewe haukuwa mrefu sana, pia tuliwafahamu wazee wa mtaa ule. Kati ya ninao wakumbuka walikuwa Mzee Kasingo, Mzee George Masasi, huyu alikuwa dereva wa Relwe na pia alikuwa mjomba wangu, Mzee Malangalila aliyekuwa mganga maarufu. Simsahau Mwarabu aliyekuwa akitupa pilau kila sikukuu ya Iddi. Alikuweko Baba Moshi yeyey alikuwa polisi, wakati huo alikuwa na watoto wawili Moshi na dada yake. Pembeni ya nyumba ya babu alikuwa akiishi Bibi Mahenge. Baadhi ya watoto ninao wakumbuka ni Shukuru, Jelasi huyu nae baba yake alikuwa dereva wa relwe, Rose, Anitha na Henry watoto wa Mzee Masasi, Lestermtoto wa mchungaji, Peter mtoto wa mzee Malangalila, watoto wa Mzee Kisingo walikuwa wakubwa, Athumani alikuwa mwonezi kweli akikukuta anakupiga konzi ilikuwa tukimuona tunakimbia mbio.
Siku za Jumamosi kulikuwa hakuna shule japo Jumamosi nyingine kulikuwa na zamu ya darasa kufanya usafi. Hivyo Jumamosi tulikuwa tunapitiliza kidogo kulala, si sana maana mama alikuwa hakubali mtu awe kitandani mpaka saa tatu hata iwe siku kuu gani, utafukuzwa utoke nje uoge ukacheze, ukichelewa utakuta uji au chai imekwisha. Jumamosi pia ilikuwa na vituko vyake kati ya kimoja ambacho kilikuwa kikidhalilisha sana, ilikuwa unaweza ghafla ukasikia watoto wanaimba, ‘Kikojozi kakojoa na nguo kaitia moto, kindumbwe ndumbwe chalia’. Hapo tulikimbia nje kujiunga na waimbaji kwani ilikuwa na maana kuna mtoto kikojozi anapitishwa mtaani kuelekea kisimani. Ulikuwa utamaduni kuwa mtoto akiwa anakojoa kitandani, na adhabu zote zimeshindikana basi siku ya Jumamosi, anaamshwa anafunikwa virago alivyokojolea, wengi tulikuwa tunalala kwenye vitanda vya kamba vilivyotandikwa kirago, baada ya kufunikwa anatolewa nje na wwenzie wanaitwa kumuimbia na kumsindikiza mpaka kisimani ambako adhabu inaisha kwa kutumbukizwa kisimani Sina uhakika kama aibu hiyo ilikuwa ikisaidia kumfanya mtoto aache kukojoa, lakini hakika ilikuwa inadhalilisha kwani habari hizo zikifika shuleni, mtoto atataniwa siku zote pale shuleni.

Kitanda cha kamba kikiwa na kirago juu

Lakini nadhani mwisho watu walikuwa sugu maana adhabu za kudhalilisha zilikuwa nyingi tu. Kwa mfano mwisho wa mwaka wanafunzi wote mlikusanywa pamoja na yakawa yanatajwa majina ya wanaoingia darasa linalofuata. Wale wanaoitwa walikuwa wakitoka kwenye kundi kubwa na kuanzisha kundi lao, hatimae waliofeli na kubakia darasa lilelile walibaki peke yao, na baada ya hapo ilitolewa amri ya kuwazomea ‘waliobunda’. Kwa mwaka mzima unaofuata unajulikana kuwa ulibunda, na unakumbushwa hilo kila mara na wanafunzi wenzio waalimu na wazazi. Kati ya amri kubwa tulizotakiwa kufuata ni marufuku kula kwa ‘watu’. Nadhani wazazi walikuwa wakifumba macho tu pale tulipokuwa tukila kwa Mwarabu siku ya Iddi, lakini ole wako ijulikane ulikula nyumba nyingine adhabu yake utadhani ulienda kuiba. Ila nakumbuka jambo moja ambalo nikijaribu kufikiria sipati jibu. Nyumbani kwetu hatukuwa na tatizo la chakula, lakini nilikuwa na rafiki yangu aliitwa Hassani alikuwa akiishi katika moja ya nyumba za tofari mahala ambapo saa hizi ni eneo la biashara ya ‘kitimoto’ jirani na CCM Mkoa. Hassani alikuwa akiishi na kaka yake ambaye sikumbuki kuwahi kumuona. Alikuwa akipata taabu ya chakula na kuna siku alikuwa anakuja kula kwetu, lakini kuna siku nilikuwa nakwenda kwao tunapika ugali, na kuanza kusaka mboga za majani zilizojiotea hovyo kando ya barabra na kuzichuma kisha tukapika tukala. Kuna siku tulikosa mboga hizo tukawa tunakula ugali kwa maji ya chumvi. sijui yu wapi rafiki yangu yule……ITAENDELEAAA

Categories: Iringa, Uncategorized

1 reply

  1. John Kitime, kwa kweli wewe unagus maisha ya watu wengi kwani hizi njia ni wengi sana tumezipitia na nadhani kwa watoto wa siku hizi sidhani kama wanayajua haya yote, mimi ningekushauri to compile all these documented facts uziite au utafutie Common Title kama vile VITUKO VYA UTOTONI ENZI ZETU, ili ijitofautishe na muda wa sasa. Thanks very much!!!

    Like

Leave a reply to David Nderimo Cancel reply