LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 15


Barabara Mbili

Leo nimepata faraja sana maana nimeanza kupata michango ya kumbukumbu kutoka kwa wazee wengine waliokuweko zama hizo. Kwanza nirudi Barabara Mbili, awali nilitaja majina ya wazee waliokuweko enzi hizo, nimekumbushwa majina mengine ambayo itakuwa vizuri nikiyataja hapa tena. Pamoja na majina niliyokwisha yataja, Mzee George Masasi, Mzee Kasingo, Bibi Mahenge, Mzee Malangalila, nimeongezewa majina muhimu mengine.
Mzee mwatebela, Mzee James Mulwa Mkamba huyu alikuwa na Shirikisho Bar. Jina Shirikisho lilikuwa maarufu siku hizo kwani viongozi wa mwanzo wa nchi za Afrika walikuwa na ndoto ya kutengeneza Shirikisho la Afrika, japo Afrika Mashariki tuliweza kufikia Shirikisho la Afrika Mashariki. Mama Zelea, huyu alikuwa na nyumba kubwa jirani na nyumba ya Mzee Masasi, kulikuweko hata wimbo tulikuwa tukiimba unaitwa Mama Zelea, mama huyu alikuwa mpole sana mwenye kuongea taratibu na muda mwingi alikuwa kwenye baibui, kwa mama Zelea ilikuwa nyumba nyingine tuliyokuwa tukikusanyika siku ya Iddi kula wali awamu ya pili baada ya kutoka kwa Mwarabu.
Kulikuwa na Mzee Musa Kibalabala, Athumani Liundi, Mzee Daudi Sapi alikuwa na nyumba nzuri mtaa mzima, nyumba hiyo ilikuwa na chipping ya kijani na madirisha makubwa ya kioo, na ngazi nje na kuifanya ya kipekee mtaani. Nyumba ya babu yangu ilikuwa na madirisha ya mbao, na ndivyo zilivyokuwa nyumba katibu zote mtaani. Nyumba ya mwisho karibu na kota za Relwe ilikuwa ya Ibrahimu Makongwa ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya enzi hizo.
Nyumba nzuri zilikuwa chache, nakumbuka nyumba ya mwisho kwenye kona ukiwa unashuka kutoka stendi, tulikuwa tukijua ni nyumba ya Mhabeshi, ndio ilikuwa nyumba nzuri zaidi katika sehemu ile ya Makorongoni.

Categories: Iringa

2 replies

  1. Mtaa wa Barabara Mbili au Kwa sasa Tandamti pia ulikuwa na Baa iitwayo Matamba Bar ya Mzee Mwaikambo,pia nyumba kubwa ingawa ndiyo zile za Udongo ambao ni imara sababu ipo hivyohivyo ya Mzee Abdala Mgohamwende.Hawa nyumba zao zipo mstari wa chini msitari ambao ndiyo huo huo wa Mzee Makongwa.

    Like

Leave a reply to Hafsa Kufakunoga Cancel reply