
Mwishoni mwa mwaka 1964 baba alipata kazi ya Sales manager katika kampuni ya mafuta ya CALTEX. Nyakati hizo kulikuwa na kampuni chache sana za kuingiza na kuuza mafuta nchini. Ilikuweko Caltex(California-Texas) ya Wamarekani, Shell BP(British Petrol) ya Waingereza, ESSO ya Wafaransa na Agip ya Wataliani, pia campuni iliyoitwa Mobiloil. Kazi ya baba ilikuwa kuzungukia vituo vyote vya CALTEX kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuhakikisha wananunua na kuuza mafuta ya CALTEX. Alikuwa akizunguka Iringa, Mbeya Tunduma, Sumbawanga, Kyela , Ipinda, Njombe na miji midogo ya karibu kufanya kazi hiyo. Kampuni ikampa gari, Hillman Minx, na akaona heri awe anaishi Mbeya ili awe katikati ya eneo lake la kazi. Muda mwingi alikuwa safarini.

Tulipoingia Mbeya niliingia maisha tofauti kabisa na Barabara Mbili. Nyumba tuliyokuwa tukiishi ilikuwa sehemu ambayo karibu majirani wote walikuwa wakiishi Wahindi. Nyumba yetu ilikuwa jirani kabisa na Stendi kuu ya mjini Mbeya. Katika kona moja ya Ilipoanzia stendi hiyo kulikuwa na nyumba ya Mzee mmoja Chotara aliyejulikana kwa jina la Baba Shukuku, huyu Shukuku alikuwa rafiki yangu wa kwanza pale Mbeya. Baba Shukuku alikuwa fundi wa magari na alikuwa na taxi kadhaa. Nyuma ya nyumba ya baba Shukuku kulikuwa na mzee mwingine chotara ambaye binyi yake aliyeitwa Salama tulikuwa tukisoma nae na kucheza nae. Nyumba iliyokuwa nyuma yetu waliishi wakimbizi wa kutoka Zimbabwe, mmoja wao aliitwa Kamjuji, alikuwa akijitomasa shingoni kwa vidole inatoka sauti kama kaweka pesa, nilijitahidi kujifunza kufanya vile zikuweza kamwe, nilikuwa napenda kwenda kwao kusoma magazeti ya kutoka kusini. Majirani wengine wote walikuwa Wahindi. Nikaingizwa shule ya Aga Khan Primary School, baadae ilikuja kuitwa Shule ya Msingi Azimio. Ngoma ikaanzia hapa, kwanza masomo yote ni ya Kiingereza, pili kukaa na watoto na waalimu wa Kihindi, maisha yote wenzangu wote walikuwa waswahili wa Barabara Mbili, ilikuwa mtihani mkubwa. Shule ilikuwa safi kulikuwa na wafanyakazi wa kufanya usafi mpaka chooni, kumbuka kuwa nilitoka shule ya Consolata ambapo kuosha vyoo ilikuwa kazi ya wanafunzi, na vyoo vyenyewe vilikuwa hata maji mnaenda kuchota kisimani ili kufanya usafi. Kiingereza changu ilikuwa nimeanzia darasa la tatu na kujua maneno machache kama Ziz iz a boy, hapa nikaingia darasa la tano na kukuta wanasoma Oxford English Book 5, kitabu chenye hadithi ya yule mjanjamjanja Abdul, aliyemshonea mfalme nguo isiyoonekana na wenye dhambi. Kila kitu kilikuwa tofauti, wanafunzi walikuwa hawaogopi sana waalimu, lugha waliokuwa wakiongea nilikuwa siijui, kwanza nilikuwa nawaonakama wazunguwazungu flani hivi wanaoongea Kihindi muda wote. Lakini darasani kulikuweko na waswahili wawili watatu, Gwakisa, Cosmas na binti wa Kinyasa alikuwa akiitwa Gloria Nyirenda, pia kulikuwa na waalimu wachache Waafrika akiwemo mama yangu mzazi, hii ilisaidia sana nisinyanyasike. Siku zikaenda nami nikawa moja wapo wa wanafunzi. Nilianza kupata marafiki Wahindi mmoja wao alikuwa akiitwa Nagib, baba yake alikuwa na duka la mikate na pia alitengeneza pipi, hakika nilikula sana pipi. Rafiki mwingine alikuwa akiitwa Imtiaz, huyu aliendelea kuishi hapo Mbeya mpaka karibuni, wao walikuwa na duka supermarket, mara ya mwisho nilimkuta na duka kubwa la dawa pale Mbeya. Sehemu ilipo Stadium ya Mbeya ulikuwa uwanja wa Gofu, na ilikuwa jirani kidogo na duka la akina Imtiaz.
Mambo mawili makubwa naweza kusema kuhusu kipindi hicho Mbeya. Pale shuleni sanaa ilikuwa inatiliwa msisitizo sana na kulikuwa na mashindano ya kuonyesha vipaji mara kwa mara. Na nilishiriki kuimba wimbo uitwao Jamaican Farewel na kushinda zawadi ndogo na hapo ndipo ndoto yangu ya kuwa mwanamuziki ilipoanza. Kulikuweko na mwalimu wa Kimarekani bibi mmoja mzee aliyeitwa Miss Maire alikuwa anaweza kupiga gitaa, harmonica na filimbi huyu nikawa namtembelea kila Jumamosi nikapige hivyo vyombo vyake. Jumapili baada ya kutoka kanisani na wazazi tulipita soko Matola kununua vitu vya wiki, sokoni nguo iliyokuwa ikitawala ilikuwa ni ya rangi ya bluu, kama vile wanawake wa Kihehe zamani walivyokuwa wakivaa kaniki, basi akina mama wa Kisafwa walikuwakivaa kitambaa cha bluu. Bei za vyakula zikuwa chini sana wakati huo kwa sababu kila kitu kilikuwa kingi na kiliishia Mbeya tu. Siku moja baba akamkuta mkimbizi mmoja anauza gitaa, basi akalinunua gitaa na ndio hasa lilikuja kuwa gitaa nililojifunzia. Kitu cha pili ni kuwa hapa ndipo nilipompenda msichana kwa mara ya kwanza. Kulikuwa na binti wa Kihindi darasani kwetu aliyeitwa Noor, mama yake alikuwa mwalimu wa shule ya chekechekea. Alikuwa akiishi mitaa karibu na shule, kiukweli Wahindi karibu wote waliishi maeneo hayo. Huyu nilimpenda sana, nikawa nimemwambia hata rafiki yangu Shukuku kuwa Noor ni mchumba wangu. Kuna mahala nikasoma namna namna ya kutengeneza dawa ya mapenzi, nilitakiwa kutafuta mpapai dume nchimbe mizizi yake kisha nikaushe halafu nitwange iwe unga, kisha nachanganya na mafuta ya kujipaka. Ilitakiwa kila ninapotaka kumuona mpenzi wangu nipake mafuta hayo. Tulihangaika sana na Shukuku kupata mpapai ‘dume’. Kosa kubwa nililofanya ni kuandika maelezo haya kwenye karatasi, bahati mbaya nikaipoteza ile recipe na mama akaikoto na kumpa baba. Sinema likawa tamu zaidi pale nilipotafutwa sikuonekana, kumbe nimeenda kusimama kwenye mti uliokuwa ukiangalia mlango wa nyumba ya kina Noor, ilikuwa ratiba yangu ya kudumu hasa siku za week end. Nilikuwa nimemuaga Shukuru kuwa naenda kwa mchumba wangu, wakati natafutwa Shukuru akaulizwa nae bila ukakasi akawaambia, ‘Joni kaenda kumuona mchumba wake’. Alitumwa kuniita, nikakuta viboko vimeshatayarishwa..dahh. Uchumba ukaisha siku hiyo kabla hata muhusika hajajua kuwa nampenda….Headmaster alikuwa Mzee Mmoja aliyeitwa Mr Lohar, alikuwa mkali sana huyo tulikuwa darasa moja na mwanae Rafiq ambaye nashukuru bado tunawasiliana. Mzee Lohar nae alikuwa hacheleweshi kutembeza kiboko. Mwaka mmoja pale Mbeya palinijenga mambo mengi sana hadi leo. Mwanzoni mwa mwaka 1966 tukarudi ‘home ground’ Iringa…….ITAENDELEAA
Categories: Iringa, Uncategorized
David ngoja na wewe nikuchekeshe kama nilivyocheka mimi. Kwenye comment yangu ya mwanzo nilieleza jinsi umombo ulivyokua unapanda toka niko Std II pale Consolata Roman Catholic Primary school Iringa ung’eng’e niliopata kwa Babu yake mwenye Blog hii Mwalimu Kitime na hivyo Baba yangu akaamua kunihamishia shule nyingine ya English medium Wakati huo inaitwa HIGH RIDGE PRIMARY SCHOOL. Hapo waalimu wote kasoro 2 walikuwa wahindi , wanafunzi wote Wahindi, Magoa na Shelisheli au Seychelles. Hapo nikamkuta binti mmoja wa kishelisheli (Seychelles ) kwa jina akiitwa Lorna Silva. huyu alikuwa ni dada yake na rafiki mpenzi wa John Kitime akiitwa John Silva wakicharaza magitaa pamoja hata siku ya Graduation day ya Form IV walipomaliza secondary school. nikampenda kweli binti huyo bila yeye kujua bali ni kuzungumza kiingereza tu na yeye mambo ya kawaida. Sasa kwa upande wangu mimi wewe ulikuwa mjanja zaidi ukatafuta njia ya kufikisha ujumbe ambao ukagonga ukuta na kukusababishia madhara ya viboko. mimi upande wangu ilikuwa kinyume kwani nilikuwa bwege kweli maana nilishidwa kabisa kusema chochote nikabaki nameza mate tu hadi leo hii na sasa zimebaki memories tu kama hizo zako kasoro viboko. hakika siku hizo kweli zilikuwa tamu.
LikeLike
John, hii nimecheka sana kwa vile na mimi yalinikuta lakini tofauti kidogo, sehemu tunayoishi ilikuw wahindi wengi sana nami nikampenda msichana bila hata yeyey kujijua, yeye alikuwa Goa, hawa ni wahindi Wakristo/Roman,…ilibidi nijifunze Kiingereza ili niweze kumwandikia barua, basi nilivyompa barua akampa Mama yake ambayo aliichukua na kumpelekea mama yangu,..sitasahau vile viboko…na tangu siku hiyo tukanyimwa kupewa COMICS, yale magazeti ya cartoon watoto, waliyokuwa wanapenda kuyasoma,………
Asante sana, nimeipenda.
Tena wakati huo 60″s tulikuwa tunacheza mpira pamoja na Wasichana,..kweli maisha yalikuwa tofauti kidogo na kule PASEE Uswahilini!!!!
LikeLiked by 1 person
Hahahaha
LikeLike