LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 18


Wolf Cubs wa Aga Khan Mbeya

Nilipojiunga na shule ya Aga khan Mbeya nikakuta kitu kinaitwa Wolf Cubs, hii ni hatua ya chini kabla hujajiunga na kuwa Skauti. Pale shule ya Consolata kulikuwa na kundi zuri la skauti lakini sikuweza kujiunga, wenzetu wakubwa waliokuwa darasa la tano ndio waliweza kujiunga, tukawa tunawatazama wanavyopendeza na nyimbo zao na magongo yao wanapotembea ilikuwa safi sana. Kwa hiyo nikajiunga na kundi la Wolf Cubs ili baadae niwe skauti kamili, kati ya mambo tuliyofanya ni kujaribu kupanda ule mlima mrefu wa Mbeya, maarufu Mbeya peak, wazazi wa wenzetu Wahindi wakaja na magari kuwasaidia watoto wao kuwarudisha nyumbani wakiwa hoi. Kulikuwa na wahindi wengine ngangari sana, namkumbuka Azad puandefu, huyu alikuwa mwembamba na alikuwa na pua ndefu hilo likawa jina lake rasmi muda wote niliokuwepo. Alikuwa na vituko kila siku, kwanza alikuwa akijifanya mmoja wa watemi wa sinema za kihindi, miondoko yake vaa yake na hata jinsi alivyochana nywele, kuonyesha utemi wake mara asilale kwao analala juu ya miti, mara kaiba gari la mjomba wake mara atoroke darasani kupitia dirishani basi alikuwa mjanjamjanja flani. Mwingine alikuwa chotara wa Kihindi na Kinyakyusa anaitwa Nazir Barma huyu alikuwa anaweza kuwakong’ota wenzie wote, na muda mwingi utamkuta uswahilini mara Ghana, mara Mabatini.Jambo moja nililolikuta kila mara wahindi watemi walikuwa wanaongea Kiswahili kimenyooka kuliko wenzao. Kati ya shughuli tulizopeda kufanya ni kwenda picnic.Tulikuwa tunapenda kwenda picnic Nzovwe ambako kulikuwa na chemchem ya maji ya moto, huko tulishinda tunaoga na kula vyakula vya kihindi, wenzangu walikuwa wakifungiwa vyakula vingi kuja navyo picnic, mimi nadandia tu, nani akupe chakula cha kwenda nacho popote? Pia tulikuwa tukienda picnic jirani na shule ya serikali iliyokuwa inaitwa NA Goverment School kulikuwa na vichaka vizuri kwa kufanyia picnic.
Gari jipya liliingia mjini wakati huo lilikuwa muundo wa Consul Corsair, nilikuwa nina uhakika nikiwa mkubwa lazima ninunue Corsair, nilikata mapicha kwenye magazeti, nikawa naenda kuiangalia nyumba ya jirani kuna jamaa alinunua moja mpyaa kabisa. Nilikuwa namuona anafaidi sana. Halafu wakati huo nilikuwa na ndoto za kuja kushiriki East African Safari, haya yalikuwa mashindano ya magari ya Afrika ya Mashariki yaliyotoa majina mengi yaliyopata sifa. Bert Shankland, Joginder Singh na ndugu yake Jaswant Singh, Pat Moss (huyu alikuwa mwanamke) na wengine, Nikiangalia consul corsair siku hizi sielewi nini kilinifanya niipende vile.

Kushoto Consul Cortina ikiwa kwenye mashindano ya East African Safari, kulia Consul Corsair iliyokuwa ndoto yangu

Mchezo mwingine mkubwa ulikuwa kurusha tiara/ vishada kwenye uwanja wa shule. Nyuma ya shule kulikuwa hakuna majengo yoyote wala waya za umeme hivyo tulishinda muda mrefu tukirusha tiara. Kufikia muda huu nilikuwa nazungumza Kiingereza kama muhindi, athari niliyonayo mpaka leo. Na hata Kihindi (Kikhoja) nilikuwa sitetwi.
Ilikuwa katika kipindi hikihiki niliporushwa na umeme kwa mara ya kwanza maishani, na nina uheshimu umeme mpaka leo. Kituo cha mafuta kilicho karibu na shule yetu kilikuwa ni kituo cha kampuni ya CALTEX, nyuma yake kulikuwa na rafiki zangu akina Fred, waswahili wenzangu, siku hiyo tukaamua kucheza mchezo wa kujificha. Mimi nikajificha chini ya uvungu wa kitanda, nikatafutwa muda mrefu, sionekani. Wakati niko chini ya kile kitanda macho yakazoea kiza nikaanza kuona vitu mbalimbali, kimojawapo ilikuwa swichi ya umeme iliyovunjika. Kwa utundu nikaigusa, nilipiga ukelele na kurusha kitanda godoro na kila kitu juu yangu, nilisikia tu griiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii mwili mzima. Mkasa kama huu ulikuja nitokea tena miaka mingi baadae kwenye guest house moja Arusha, lakini hiyo ni hadithi ya siku nyingine………..ITAENDELEEA

Categories: Iringa, Uncategorized

1 reply

  1. one again thanks for this narative, nayakumbuka sana mashindano ya East African Safari na shabiki kama vile Yanga na Simba/Sunderland na mimi nikawa mshabiki wa Datsun 240-Z series, na baaday kuhamia Cortina (Ford Cortina),……hayo mambo ya umeme ndio yaliyonifanya nianze utundu wa kupigwa short mapema mno na kama unakumbuka kwenye Gari kuna kifaa tikiita Choke, ni coil ambayo ukiweka umeme wa 12 Volts inatoa umeme mkubwa, tukiwategeshea wenzetu wkipigwa shoti, mpaka siku moja mwenzetu akizimia wote tukakimbia bila kutoa taarifa, habari zikaenea David kaua mtoto kwa umeme, kumbe aliamka baadaye naye kutimulia mbio kwao,…lakini nakumbuka huo ndio ulikuwa mwanza wa kupata ajira ndogo ndogo za kutegesha watu wapate shoiti, kama tulivyoita wakati ule,…kutega kwenye mababda ya kuku , magari mabovu nakadhalika,……..

    thanks very much again for this flashback!!!

    Liked by 1 person

Leave a comment