LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 19


Tukio la kisiasa la kwanza ninalolikumbuka ni shughuli za kuandaa mkutano aliohutubia Mwalimu Nyerere ambao ulifanyika kwenye uwanja wa mpira wa shule ya Iringa Middle School, uwanja ambao kwa sasa ni Uwanja wa Samora. Sikumbuki kumuona Mwalimu Nyerere kwa karibu wakati huo, lakini Mzee mmoja amenitaarifu kuwa baada ya mkutano Mwalimu alilala kwenye nyumba ya Mzee Abbas Maxi kule Makorongoni (Makorongoni Oyee)., mkutano huo ulikuwa katika kampeni za kukitangaza chama cha TANU. Tukio la pili la kisiasa ninalolikumbuka lilikuwa lakutisha kidogo. Siku chache baada ya Uhuru mwaka 1961, vijana wa TANU Youth League wengi walikuja nyumbani kwetu na kuanza kuzunguka nyumba yetu huku wakiimba ‘Bendera Bendera Bendera yapepea sasa tumekuwa huru’ wakati huohuo wakitupa changarawe juu ya bati la nyumba yetu, nakumbuka kujificha uvunguni mwa kitanda. Baadae sana mtu mmoja aliwahi kunambia inawezekana kwa kuwa baba yangu alikuwa katika chama kingine cha siasa wakati ule, aidha UTP au ANC, kwani ndivyo vyama vilipingana na TANU katika uchaguzi wa kwanza nchini ambapo TANU ilipata ushindi mkubwa sana.
Mwanzoni mwa Januari 1964 yalitokea mambo makubwa mawili japo kwa sie watoto tuliokuwa Iringa hayakubadili chochote katika taratibu zetu za kawaida. Tarehe 12 ya mwezi huo ndipo yalipotokea mapinduzi Zanzibar, tukawa tunasikia wakubwa wakimtaja John Okello, Babu na baadae Karume. Nakumbuka kukaweko na hadithi ya kitoto kuwa Adulrahmani Babu alitumia mtumbwi toka Zanzibar mpaka Dar es Salaam kumwambia Mwalimu Nyerere kuwa kumetokea mapinduzi Zanzibar!! Kama wiki moja baada ya Mapinduzi Zanzibar, yakatokea maasi ya wanajeshi wa Tanganyika Rifles, jeshi lililokuwa la Tanganyika. Tukaona magari yakiwa yamejaza familia na kubeba mizigo mingi yakiingia Iringa, watu wakawa wanasema, ‘Daresalamu kuna vita’. Tarehe 26 mwezi huohuo tukasikia kuwa Tanganyika na Zanzibar zimeungana, sikumbuki kama kulikuwa na shamra shamra zozote siku hiyo,nadhani kwa kuwa jambo hili lilitokea ghafla, hakukuwa na matayarisho ya sherehe.
Nilianza kuwa kujua na kushiriki shughuli za kisiasa kupitia matukio mbalimbali, kwanza kwenye somo la maarifa ukiwa darasa la nne, ilikuwa lazima uwajue wakuu wote wa wilaya nchini, wakuu wa mikoa, mawaziri wadogo na mawaziri wengine wote na kuwataja kwa kichwa, na uwe unaweza kuchora ramani ya mkoa wako na wilaya zake na ramani ya nchi na mikoa yake na kisha ramani ya Afrika na nchi zake. Siku Waziri yoyote alipotembelea mji, shule zilifungwa na wanafunzi tulienda kujipanga barabarani kumsubiri, hivyo heka heka zilikuwa za kutosha, siku nyingi za shule zilipotea na mapema serikali ikaagiza kuwa ni viongozi wa juu tu tu ndio ambao watasababisha wanafunzi waache masomo na kwenda kuwapokea.

Halafu kulikuwa na siku kuu za Kitaifa, Sabasaba, Uhuru, May Day na kadhalika, siku hiyo wanafunzi tulikusanyika shuleni na kuanza maandamamo kuelekea uwanja wa Bomani (Garden) ambako kulikuwa hasa ndio mahala pa mikutano na maonyesho mbalimbali ya siku hizo za sikukuu. Kama nilivyosema awali kila shule ilikuwa na bendi yake ambayo iliongoza masafara wa shule. Bendi hizi zilipishana kwa ubora na vimbwanga. Shule yetu ya Consolata ilikuwa na bendi nzuri sana, watu waliokuwa maarufu katika bendi walikuwa mshika fimbo na mpiga ngoma kubwa. Mpaka leo wenzangu wengi wanamkumbuka Karama Masudi, mpiga ngoma kubwa na pia golikipa wetu, Kigahe nae alikuwa mpiga ngoma kubwa maarufu, nadhani ilikuwa ni wakati wake shule ikapata ngoma kubwa ya kisasa na si zile zilizotengenezwa kwa ngozi ya ng’ombe. Ratiba ya siku ya maandamano pale Consolata ilianza asubuhi kwa ukaguzi wa usafi, wachafu walikuwa wakiondolewa na kuachwa shuleni wafanye usafi wa shule. Baada ya pale tulianza kutembea kwa ukakamavu tukiongozwa na bendi ya shule tukiteremka na barabara kuu kuelekea uwanja wa Bomani, wakati huo hata shule nyingine zilikuwa na ratiba kama hiyo , kwa hiyo si mara moja tulikutana barabarana na hapo ndipo wapiga ngoma waliongeza sauti kukawa na mashindano ya aina fulani kila bendi ikipiga wimbo wake na kutaka uwe ndio unasikika. Sisi na ngoma yetu kubwa ya kisasa tulishinda mara nyingi sana mpambano huu ambao ulikuwa unatupa hadithi za kusimuliana baadae. Mshika fimbo nae katika mpambano huo aliongeza vimbwanga kwa kuzungusha na kurusha fimbo juu na kuidaka kwa madaha, sie huku tukitembea kikakamavu zaidi na kutupa mikono kama askari wa ukweli kuwashinda wapinzani. Hatimae tulifika uwanjani, kila shule na mahala pake. VIongozi wakaanza mikutano yao. Enzi hizo kauli mbiu zilikuwa hivi, kiongozi alisema ‘Uhuru na TANU’ na wananchi walijibu ‘ Uhuru na TANU’, au ‘Uhuru na Kazi’ au ‘Uhuru na umoja’ jibu likawa kurudia kauli, baadae ikabadilishwa ikawa wananchi wanajibu ‘Kazi ya TANU’ baada ya kila neno la kiongozi, na baada ya salamu hizo mikutano iliendelea kwa kukaribishwa Waheshimiwa. Kila kiongozi akaitwa Mheshimiwa, ilipoingia siasa ya Ujamaa, neno Mheshimiwa likaachwa, ikawa sasa ukaribisho ukaanza kwa kusema tunamkaribisha Ndugu Mkuu wa Mkoa, au Ndugu Waziri na kadhalika. Katika upande wa bendi, nisisahau kuwa Wahindi walikuwa na bendi yao ya Jamatini iliyokuwa na vifaa vya kisasa ilikuwa nayo nzuri sana ikipendeza kutokana pia na mavazi yao rasmi ya Brass Band.
Kama nilivyosema awali tulihamia Mbeya nikawa nasoma shule ya Aga Khan, siku moja tukapata mwanafunzi mpya, tukaambiwa katoka Zanzibar, ilikuwa mara yangu ya kwanza kuona mtu kutoka Zanzibar. Nakumbuka ilisemekana baba yake alikuwa polisi, kwa vyovyote kama alikuwa polisi basi alikuwa na cheo kikubwa kwani watoto wake walikuwa wanaletwa shuleni na gari na pia kurudishwa kwa gari……………ITAENDELEAAAAA

Categories: Iringa, Uncategorized

1 reply

  1. BAADA YA KUSOMA MAKALA HII MZEE MAPUNDI KAANDIKA HIVI….Wasomi wa wawakati ule wengi walikuwa chama cha Gavana United Tanganyika Party …U.T.P…kwa hofu ya kufukuzwa kazi……ata Chief Adam Maomba Sapi,Francis Kitime,Amran Mayagila D.E.O…Dr Varty Mwanjisi ambaye 1958 alikuwa na private hospital kwene makutano ya barabara itokayo mwembe togwa inapita kwa mzee Yasin mhabeshi vuka korongo nakukatisha barabara kuu kwenda kintazini yenye vitanda 30 na wengine wengi….ata babu angu Charles Nindi bwana afyia wa wilaya nae pia

    Like

Leave a comment