LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 22


Moja ya jambo lililokuwa likinipa shida sana ilikuwa kuamka asubuhi na kwenda kumnunulia sigara baba yangu. Baba alikuwa mvuta sigara karibu maisha yote niliyomfahamu. Kwenye miaka ya 60 na 61 alikuwa akivuta sigara iliyoitwa Crown, na mara nyingine alitumia mtemba kuvuta tumbako yenye jina hilohilo. Baadae akahamia Sportsman, na hatimae kuvuta Portsman. Sigara ndizo zilizosababisha kifo chake. Baba alikuwa akiamuka asubuhi lazima aanze siku na sigara, kama akiamka asubuhi hana sigara, ilikuwa nitumwe kwenda kununua sigara jambo ambalo sikulipenda kabisa.
Wakati tukiishi maeneo ya Lugalo mwaka 1966 na kuendelea, kulikuwa hakuna maduka karibu. Hivyo ukitumwa dukani ilikuwa lazima uende aidha Relwe, pale karibu na National Milling, hapo ndipo kilikuwa kituo cha mabasi ya relwe na kulikuwa na duka ndani ya kituo ambapo ungeweza kununua sigara au uende Kihesa. Pale karibu na soko la Kihesa kulikuwa na maduka ya kuuza sigara. Kwenda Kihesa ilihitajika uchukue njia nyembamba iliyoanzia mwisho wa uwanja wa mpira wa shule ya Lugalo, pale kulikuwa na kimteremko fulani kutoka uwanjani, kimteremko hiki tulikuwa tukikitumia kwa mchezo wa kutereza, kilisaidia sana kuchakaza kaptura. Ukimaliza sehemu ya kutereza ndipo unakutana na tuta ambalo lilitengenezwa kwa ajili ya kulenga shabaha, baaada ya hapo ni njia nyembamba ambayo asubuhi ilikuwa inajaa umande, na msimu mwingine nyasi ni ndefu sana hivyo unalowa umande mwili wote. Katikati ya Lugalo na Kihesa ilikuwa pori,nyumba za Kihesa zilianza baada ya kupita hosteli za Padri Balbanti, ambayo pia jirani yake kulikuwa na shule ya chekechea.
Kuanzia kona ya Lugalo kwa upande wa kushoto kulikuwa hakuna jengo lolote mpaka pale ilipo gereji ya Sagamiko. Hapo kulikuwa na nyumba zilikuwa zikikaliwa na Wahindi, kisha ikafuata gereji iliyoitwa Kingsway Garage baadae ilikuja kuwa KJ Motors miaka michache baadae. Kampuni ya KJ Motors ilikuwa ikishughulika na kuuza aina mbalimbali za usafiri kuanzia pikipiki za Honda mpaka mabasi na malori ya Isuzu. Kifupi iliuza magari na vipuri vya magari kutoka Japan. Baada ya KJ Motors lilifuata jengo la TANESCO kisha ile nyumba ya ghorofa moja iliyopo mpaka sasa. Pale ilipo Hoteli ya Isimila kulikuwa na jengo la makazi ya kawaida. Waliokaa pale wote walikuwa Wabaniani. Kulikuweko na ndugu wawili Suriyakant na Chandrakant Patel, hawa ndio walikuwa wakiendesha kituo cha mafuta cha Caltex kilichopo jirani na kanisa na msikiti wa Mshindo. Pia alikuweko Baniani mwingine aliyeitwa Joshi, mwanae tulikuwa darasa moja na kila mara tulikuwa tukimtania kwa kutumia methali ile isemayo ‘Dau la Mnyonge haliendi joshi’. Baada ya hapo yalianza majengo ya National Milling ambayo yalikuja kupakana na TFA.


Tukirudi tena mpaka kile kibanda cha basi cha Sabasaba, upande wa kulia, nyumba ya kwanza kama nilivyosema awali ilikuwa ya mwalimu wetu Mrs Saleh, baada ya hapo zilifuata nyumba mbili mpaka ile iliyoandikwa Villa Oscar mlangoni, hapakuwa na nyumba nyingine mpaka Idara ya maji. Pale kuna barabara inayopanda juu kuelekea shule ya Wilolesi. Shule hii miaka hiyo ilikuwa inaitwa High Ridge Primary School, wakati Aga Khan ilikuwa mali ya Waismailia, High Ridge ilikuwa mali ya Wabaniani zote mbili zilikuwa English medium. Ukitoka Idara ya majo na kuvuka barabara kulikuwa na nyumba ya relwe, halafu likafuata duka la magari kutoka Uingereza, lililoitwa Ridoch Motors, hili liliuza Magari ya Ford, na matrekta ya Ford yaliyotengenezwa Uingereza. Baada ya hapo zilifuata nyumba mbili tatu za matofari nyingine zikiwa mali ya Relwe. Kisha ikafuata station na gereji za relwe eneo lililoishia upande wa pili wa benki NMB. Wakati huo benki hiyo ilikuwa ni Barclays Bank…..ITAENDELEAAA

Categories: Iringa, Uncategorized

4 replies

Leave a reply to Anonymous Cancel reply