LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 24


Sleti na kalamu yake

Katika mfumo wa elimu wakati wa ukoloni na miaka kadhaa baada ya Uhuru, mwanafunzi alianza na sub standard (supu), darasa hili siku hizi linaitwa Nursery au chekechea. Ukiwa supu, muda mwingi ni kucheza na kuimba. Lilikuwa pia darasa la kijifunza kuandika kwa kutumia sleti, hizi zilikuwa mbao za kuandika zilizotengenezwa kwa madini ya sleti, kutumia sleti tulianza kujifunza kuandika na kusoma. Tofauti kubvwa kati ya supu na nursery ilikuwa waalimu na wazazi walijua kuwa sisi bado watoto na kazi yetu kubwa ni kucheza. Siku hizi si ajabu kabisa kusikia mtoto wa nursery eti ana homework, kwangu mimi huu ni unyanyasaji kwani mtoto ananyimwa haki yake ya msingi ya kucheza.
Baada ya kusoma supu standard, wengine walichaguliwa kuingia Lower Primary School, hii mara nyingi ilitegemea umri, ili kuingia darasa la kwanza umri uliokubaliwa ulikuwa miaka sita au saba, hivyo mtoto chini ya hapo aliendelea tena kubaki supu. Shule zilizoitwa ‘Lower Primary School zilikuwa na darasa la kwanza mpaka la nne. Mwanafunzi alipofika darasa la nne, kulikuwa na mtihani mgumu sana ambao ulichuja wanafunzi wengi, na wale wachache walifaulu waliingia hatua ya shule zilizoitwa Upper Primary Schools au Middle Schools.

Njombe Middle School 1956

Upper Primary au Middle Schools zilikuwa darasa la tano hadi la nane. Shule za serikali ziliitwa NA schools, yaani Native Authority Schools, ziliheshimika sana kwa kutoa elimu bora. Mtihani wa kumalizia shule ya msingi uliitwa Territorial Examinationa, kwani ulikuwa ni wa territory yote ya Tanganyika, nchi nzima mtihani ulikuwa wa aina moja tu. Miaka ya 70 mfumo huu ulibadilishwa na kila mkoa ukawa na mtihani wake wa darasa la saba. Kati ya mwaka 1966 na 67 kulianzishwa taratibu ya kulifuta darasa la nane, ili shule za msingi ziishie darasa la saba. Mwaka 1967 mambo yalikuwa tofauti kwani darasa la nane lilifutwa na mtihani wa darasa la nne haukuwa wa kuchuja wanafunzi tena. Mwaka 1967 nilikuwa darasa la saba, hivyo sisi wa darasa la saba na wale wa darasa la nane tulifanya mtihani pamoja na wote kuingia ‘Form One’ pamoja. Darasa letu lilikuwa na Wahindi (Makhoja), Wabaniani, Waarabu wawili, Saleh Abri, Saleh Ahmed, na tulikuwa waswahili kama wanane hivi. Darasa la nane pia kulikuwa na mchanganyiko uliofanana na huo. Kulikuwa na baadhi ya wanafunzi waliokuwa wanaishi hosteli ambayo wote walikuwa wahindi kasoro wanafunzi wawili ndugu, Chacha na mdogo wake Kisyeri, hawa walitoka Tarime. Hosteli ilikuwa pia kwa ajili ya wanafunzi wa Kihindi waliokuwa wanasoma sekondari, hosteli ilikuwa mwisho wa majengo ya sekondari ya Aga Khan. Pembeni ya hosteli kulikuwa na ukumbi mkubwa uliotumika kwa chakula cha wanafunzi walio hosteli na pia ndio ulikuwa ukumbi wa shule ya sekondari ya Aga Khan, matumizi yake ntasimulia baadae.

Hosteli ya shule ya Aga Khan Iringa


Baada ya kuingia darasa la saba mambo yalibadilika nyumbani, baba akanipiga marufuku kugusa gitaa ambalo nilianza kuligusagusa toka alipolinunua Mbeya sokoni mwaka 1965. Gitaa lile lilisababishwa nipate kipigo mara nyingi kutokana na kukata nyuzi, lakini hiyo haikunizuia kuendelea kuligusa gusa, kuna siku nyingine baba wenyewe alikuwa ananiita na kunikabidhi nikalipige. Lakini ndio hivyo amri mpya ikatoka, hakuna kugusa gitaa mpaka nipasi kwenda form one. Kilikuwa kivutio kikubwa cha kusababisha nisome japo kwa bidii kidogo. Kama nilivyosema huko nyuma mama yangu alikuwa mwalimu katika shule niliyokuwa nasoma toka nilipokuwa Mbeya, na ikwa hivyohivyo nilipojiunga na Aga Khana Iringa, sasa kuwa na mzazi mwalimu wa shule unayosoma ni gereza fulani, huwezi kutoroka vipindi, fujo zako zote za darasani zinafika kwa mzazi mapema, walimu waliruhusiwa kukuadhibu bila woga, na piasi mara moja nilijikuta nikipewa adhabu na mama mbele ya darasa. Ila nikirudi nyuma na kuanza kufikiria je hali isingekuwa ile mimi ningekuwaje, maana hakika nilikuwa mtundu sana. Hatimae tulifanya Territorial Examinations, shule zikafungwa baada ya sherehe za kawaida za kuaga shule, kwa vile shule ilikuwa ya Wahindi hakukuwa na shughuli kama muziki ila kulikuwa na kula sana vyakula vilivyoletwa kwa ajili ya kuagana. Wakati nipo darasa la sita na la saba mwalimu wangu wa darasa alikuwa Mrs Saleh, baadae alikuja julikana sana Iringa mjini kutokana na mgahawa wake wa Hasty Tasty, alikuwa ndie mwalimu wetu wa Kiingereza, kuimba, kulikuwa pia kuna kipindi cha mashahiri ya Kiingereza. Unapewa shahiri halafu unapewa wiki moja ulikaririr,

Nikiwa na ticha wangu Mrs Saleh kwenye mgahawa wa Hasty Tasty

Humpty Dumpty sat on the wall
Humpty Dumpty had a agreat fall
Of all the king’s horses and all the King’s men,
None could put Humpty Dumpty together again

Tulijifunza nyimbo za Kihindi, pia kwa mfano;
Tame sutracho, tame sutracho
Bhai John, Bhai John
Sava nagra vakeche, sava nagra vakeche
ding dong ding

tafsiri yake ni wimbo ambao kila shule ulikuwa ukiimbwa
Unalala, Unalala

Kaka John, Kaka John
Kengele inalia, Kengele inalia
Ding dong ding


Mwaka 1967 ulikuwa na majonzi yake, bibi yake Baba ambaye nilipata bahati ya kumuona na akanihadithia mengi kuhusu maisha yake, maisha ambayo nayo nitahadithia humu kwani ni ‘adventure’ ya ajabu sana kwani yeye hakuwa Mhehe alikuwa mtoto wa Chifu wa Wanyamwezi!! Tulikuwa tukimuita Bibi Kongo, kwani ilidhaniwa alitokea Kongo, alifariki usingizini tarehe 10 March 1967. Tarehe 17 mwezi September mwaka huohuo siku chache kabla ya mtihani wa darasa la saba, babu yangu na rafiki yangu, Mzee, Mwalimu Raphael Mwagutangu Kitime alifariki katika hospitali ya Gavamenti……….ITAENDELEEAAAAA

Categories: Iringa

4 replies

  1. LOOOOOOOO, NIMEFURAHI SAAANA, NIMEREJELEA MAMBO MENGI SAAANA NA NIMEJIFUNZA KUWA KUMBE HUWA TUNAPOTEZA HISTORIA ZETU KWA KUTOKUANDIKA SIMULIZI KAMA HIZI
    ASANTE SAAANA

    Like

Leave a reply to Ernesto Mwonge Cancel reply