LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 25


Nilizaliwa siku ya Jumamosi muda wa saa moja hivi, baba yangu alikuwa mwalimu Middle School Njombe, wakati huo alikuwa ba pikipiki moja kubwa aina ya BSA, huo ndio ulikuwa usafiri wangu wa kwanza duniani kutoka hospitali ya Kipengele nilipozaliwa mpaka Njombe nyumbani kwa wazazi wangu. Labda ndio maana nilikuja fanya mengi na pikipiki baadae katika ujana wangu, ntaelezea baadae. Mama alisafiri na kurudi Tosamaganga kwa mama yake eneo linaloitwa Mabanda na baada ya siku chache akavuka makorongo kuingia sehemu inayoitwa Ilangi ambako ndiko baba alikulia, huku alikuwa akiishi bibi yake baba na mama yake mzazi, nikatambulishwa kwao.

Bibi Kongo- Adelaide Se Mkombe

Nilibahatika sana kumuona bibi wa baba yangu nikiwa na akili zangu. Bibi alikuwa na historia ya kusisimua sana, ambayo nayo naendelea kuifuatia ili kujua ndugu zangu wengine. Bibi aliitwa Adelaide Semkombe, lakini alijulikana kwa jina la Bibi Kongo. Inasemekana jina hilo alilipata kutokana na dhana kuwa alitoka Kongo, japo maelezo yake ni tofauti kidogo kwani alisema yeye alikuwa mtoto wa Chifu wa Unyamwezi. Ntaeleza hadithi hiyo baadae. Tulikuwa tukimtembelea bibi karibu kila mwezi, alikuwa akiishi sehemu inaitwa Ilangi jirani na kiwanda cha sukari guru cha Buruda Fabian, wenyewe tulizoea kumuita Fyabian. Bibi Kongo alikuwa mcheshi sana, mwanae Elizabeth ndie alikuwa mama mzazi wa baba yangu. Bibi Elizabeth nae alikuwa mwalimu akifundisha shule moja na babu huko Mpwapwa. Siku moja wakati baba akiwa darasa la nne, bibi alipokuwa akitoka kwenye kwaya nyakati za jioni, kuna kitu kilimtokea kuanzia siku hiyo hakuwa yeye tena, alikuwa mkimya aliyependa kukaa sehemu moja kwa muda mrefu, na alikuwa akiongea mara chache sana tena kwa sauti ya upole ya chini. Alipata tatizo katika ubongo na hivyo ndivyo alivyokuwa mpaka alipofariki. Bibi Kongo alikuwa akituhadithia kuwa alikuwa mtoto wa Chifu wa Unyamwezi. Alituambia kuwa wakati akiwa bado mdogo sana, baba yake alimtoa kwa Wajerumani kama rehani kuwa hatafanya nao vita tena. Wajerumani walimchukua mpaka Bagamoyo kupitia Kilimatinde. Alipofika Bagamoyo akakabidhiwa kwa mama aliyekuwa akipika vitumbua, alipoona anateseka sana akatoroka na kukimbilia nyumba ya mapadri wa Kitaliano ambao muda si mrefu waliondoka na kuelekea Iringa kuja kuanzisha kanisa la kwanza Katoliki pale Tosamaganga. Alipofika Tosamaganga alijifunza kusoma na kuandika na baadae akaolewa na Mzee Benedict Saula aliyekuwa moja ya wajenzi wa kanisa la Tosamaganga. Ubora wa ujenzi wa mzee Saula,unaonekana katika nyumba waliyokuwa wakiishi ambayo ilijengwa kwa uthabiti na ufundi mkubwa kutumia mawe. Vilembwekeze wa mzee huyu wameanza kuibomoa nyumba hiyo na kuuza mawe hayo. Kaburi la Mzee Saula linaonyesha hata tarehe aliyozaliwa na kubatizwa.

Msalaba juu ya kaburi la Benedict Saula, linaonyesha alizaliwa mwaka 1891 na kubatizwa mwaka 1898 na alifariki 31 Agosti 1946
Gofu la nyumba ya Mzee Saula

Categories: Iringa, Uncategorized

6 replies

Leave a comment