Ungepita nyumbani kwetu kuanzia saa kumi mpaka saa kumi na mbili jioni mwaka 1967 mpaka 1969 ungekuta watoto Zaidi ya 20 wakicheza michezo mbalimbali kwenye uwanja wa nyumba yetu. Ungekuta watoto wa Kiswahili, Kihindi, Kishelisheli, Kisingasinga na hata Kichina. Palikuwa na watoto wawili wa Kichina waliokuwa wakisoma Aga Khan Primary wakati imesha anza kuitwa Shabaha Primary School, mmoja Ving Kit na mwingine Ving Chang.
Sisi tulizaliwa watoto 6, wavulama wanne na wasichana wawili, na wakati huo mdogo wetu wa mwisho aliyezaliwa mwaka 1965 ndie pekee hakuwa na marafiki wa kumfuata nyumbani, sisi wengine kila mmoja wetu alikuwa na kundi la rafiki zake, na wote walikaribishwa nyumbani baada ya saa za shule, hivyo nyumbani palikuwa mahala pa furaha kwa watoto wa kila aina. Mama ambaye alikuwa mwalimu nae alikuwa na wanafunzi wanaofanya twisheni wakati huohuo nao waliongeza idadi ya watoto katika eneo lile. Kama nilivyosema awali tulikuwa waswahili peke yetu eneo lile wakati ule , hivyo kwetu tu ndipo watoto waliweza kucheza na kupiga kelele bila kusumbuliwa, haikuwa rahisi kwenda kucheza namna ile mbele ya nyumba za majirani zetu, wazazi wao hawakuwa na simile kubwa na hasa kama ni waswahili mnaojazana pale.
Michezo ilikuwa mingi, wengine wakicheza gololi, wengine kiboleni, wengine kuruka kamba, au michezo ya kihindi kama iti danti, au tikri, wavulana kwa wasichana ni furaha tu, pia kulikuwa na mti wa zambarau, hivyo wakati wa msimu hiyo ilikuwa shughuli nyingine. Kuna wakati huwa nawaza na kuona wazazi wetu walikuwa wavumilivu sana, Je mimi ningeweza kuvumilia vurugu zile? Sidhani, lazima ningewatimua tu wakacheze kwengine. Na pia haikuwa kucheza tu, kulikuwa na utamaduni wa chai ya saa kumi, kila siku sufuria kubwa la chai lililtengwa maana yoyote aliyekuweko aliruhusiwa kunywa chai.


Shughuli nyingine kubwa ililkuwa usomaji wa comics. Hivi vilikuwa vijigazeti vya vibonzo ambavyo vilikuwa vikitoka Uingereza, vilikuwa ni vya kila wiki, Jumanne na Alhamisi ungetukuta Iringa BookShop tukinunua magazeti hayo, ikikosekana pesa hata kuiba tuliiba maana duka lilikuwa kubwa limejaa vitabu na magazeti mbalimbali. Siku moja mwenye duka alinikamata nimeiba comic, akaahidi atamueleza baba yangu, nilidhani anatania kwa kuwa nilirudisha gazeti na kumwambia ‘Nilichukua kibahati mbaya’. Na yeye akamwambia baba yangu kibahati mbaya, Baaba alikuwa hana tatizo kutumia kiboko, sikuweza kukaa vizuri kwa wiki nzima. Jirani ya Iringa Bookshop kulikuwa na duka jingine la kuuza magazeti na vitabu lililokuwa likiitwa Iringa Printers hili hasa liliuza vifaa vya shule na stationary.
Katikati ya maduka haya kulikuwa na grocery iliyomilikiwa na Goa flani aliyeitwa Lorandos.

Comics maarufu zilikuwa Beano, Dandy, Topper na Beezer, halafu yakaja magazeti ya picha zenye hadithi za Kiafrika, Kulikuweko na gazeti la Film, mbabe alikuwa Lance Spearman na adui wake namba moja alikuwa Rabon Zollo. Hadithi zilisisimua mpaka tukawa tunaona ni kweli. Pia kukawa na gazeti la Boom ambalo kulikuwa na Tarzan wa Kiafrika aliyeitwa Fearless Fang na kukawa na gazeti la hadithi za mapenzi lilioitwa Sadness and Joy, haya nayo yalikuwa ya kila wiki bei yake shilingi moja. Kulikosa ilikuwa unajiona hufai. Jambo la ajabu ni kuwa magazeti haya yalitoka Afrika ya Kusini na enzi zile kulikuwa na mahusiano mabaya sana kati ya Tanzania na Afrika ya Kusini kutokana na siasa za kibaguzi. Muda si mrefu baada ya hapo muandishi maarufu wa Tanzania Faraji Katalambula akaanzisha gazeti la poicha la Kiswahili lililoitwa Film Tanzania.








Hatukuwa na TV lakini hakika magazeti haya, mengine yalikuwa matamu kuliko kuangalia TV, na yalitulazimisha pia kujifunza Kiingereza.
Kama nilivyosema nyumbani kwetu kulikuwa na mkusanyiko wa rafiki wengi sana. Rafiki yangu mmoja ambaye kwa kweli siwezi kumtaja labda akisoma hadithi hii na kukumbuka mkasa huu ataruhusu nimtaje, maana kwa sasa ni mwanajeshi mstaafu ambaye bado ni jina kubwa katika jamii. Siku moja alikuja na mchele, ambao nina hakika aliuchukua kwao bila ruksa, nami nikachukua sufuria kwetu tukaenda porini milimani,nyuma ya shule ya Lugalo ‘kujipikisha’. Bahati mbaya tulizidisha mno chumvi wali ukawa hauliki, ikabaki tufanye mchezo wa kusiliba ule wali kwenye miti, maana hata mbwa tuliokuwa nao hawakutaka kula ule wali kabisa. Wakati tukiwa kule porini tukakuta gofu moja la nyumba ya udongo, ndani ya nyumba hiyo tukasikia sauti ya mtu kama analia, mbwa wetu ndio walikuwa wa kwanza kukimbia, nasi tulifuata kila mtu kwa uwezo wa hatua zake tukasahau hata ile sufuria na hatukurudi tena upande ule. Mpaka leo sijui ni nini kilichowatia uwoga mbwa kiasi kile………….. ITAENDELEEEEEEA
Categories: Iringa, Uncategorized
Ukweli umeweza kuihifadhi historia ya Iringa aka Ku Boma. Hongera sana
LikeLike
Sande na inaendeleeeeeea
LikeLike
Well I wondered when you were coming to those wonderful shop’s Nakumbuka Gerald Emmanuel (RIP) Nami tulipita sana pale kununua hizi comics Niliweka copies zangu muds mrefu. Siku moja nilipokuwa Uingereza niliona copy ya Beano 1965 ikiuzwa kwa £4000 Nilipokuja likizo nikauliza nyumbani box la vitu vyangu nikaambiwa magazeti yaliuzwa kwa menye duka jirani kufungia bidhaa😩😩😩😩😩
LikeLike
LOHH KWETU HUWA HATUNA UTAMADUNI WA KUWEKA KUMBUKUMBU, TUNAONA NI TAKATAKA TU
LikeLike