
Tulifanya mtihani wa darasa la saba tukaanza likizo ya kusubiri majibu. Siku moja wakati niko porini mlimani nyuma ya shule ya Lugalo kwenye mizunguko ya klutafuta matunda ya porini nikasikia dada yangu ananiita, nikarudi nyumbani, kufika akanambia ‘Umepasi’. Nikajua matokeo ya mtihani yametoka, mama nae akanambia umechaguliwa kwenda sekondari, unaenda kusoma Aga Khan Secondary, ilikuwa habari nzuri ya furaha, nikaambiwa majibu yamebandikwa kwenye ubao wa matangazo shuleni. Kwa kuwa palikuwa jirani nikakimbilia kusoma nani mwingine kachaguliwa. Kama nilivyosema mwaka ule tulikuwa madarasa mawili tuliofanya mtihani ule sisi darasa la saba na wenzetu wa darasa la nane jumla ya wanafunzi 90 hivi. Nilipoangalia ubao nikakuta tumechaguliwa watu wanane tu katika madarasa yote mawili. Nawakumbuka wasichana Aisha Thakore, binti wa Headmaster, alikuwa na akili sana binti yule , na rafiki yake Jeet Hathibhai, huyu naye alikuwa binti ya mwalimu wa shule ya Mkwawa, Inderjit Sohal, huyu alikuwa binti wa Kisingasinga wakati huo familia ya Sohal ilikuwa ikiishi katika nyumba ambazo ni magofu zilizo jirani na kituo cha mabasi cha Ipogolo, sikumbuki kama kulikuwa na msichan mwingine. Wavulana tulikuwa mimi, Kisyeri Chambiri, Saleh Ahmed na wengine wawili siwakumbuki majina kwa sasa. Muda si mrefu tukapata barua za kueleza masharti ya kujiunga na shule. Kaptura za khaki na shati linen nyeupe, viatu na soksi na vitu kama hivyo. Nyumbani ilikuwa furaha tupu, nikaruhusiwa rasmi kupiga gitaa na baba akanipa zawadi kamera aina ya Kodak instamatic.
Siku ya kwanza sekondari nikakutana na sura nyingi ngeni na nyingi tulikuwa wote darasa la tatu na la nne Consolata Primary. Naboth Mbembati, Chesus Lutego, Emmanuel Mkusa hawa tulikuwa wote Consolata, pia nikawakuta wakubwa zetu waliokuwa mbele yetu pale Consolata, akina Gerald Mkusa, John ‘Mzungu’ Komba, Abbas Kandoro, Ibrahim Sareva, basi ikawa ni kuangalia sura mpya tu siku ile ambayo tulikaribishwa shuleni kwa kuanza kufanya usafi.
Headmaster alikuwa Mr Sheikh, mwalimu mmoja Mpakistani mrefu ambaye hakusita kukutwanga teke ukikosea karibu yake, miaka miwili baadae walishirikiana na Mwalimu Thakore kuanzisha sekondari ya kwanza ya kulipia iliyokuja kuitwa Highlands Secondary School.


Shule yetu ilikuwa na wanafunzi wengi kwani ‘form one na two’ zilikuwa na A na B, kisha ‘form 3 na 4’ zilikuwa na Science na Arts, sheria wakati ule ililazimisha kila darasa lisizidi wanafunzi 35. Mwaka mmoja kabla kuliletwa wanafunzi wengi kutoka Kanda ya Ziwa, mpango uliofanyika enzi za Nyerere wa kuchanganya wanafunzi kutoka sehemu tofauti za nchi, jambo ambalo hakika lilifanya Watanzania kujiona nyumbani popote waendapo na kuvunja sana ukabila. Hawa wanafunzi waliotoka nje ya mji wa Iringa, wengine walipata nafasi ya kuishi katika hosteli zilizokuwa karibu na shule, ambazo nilizitaja awali kuwa zilikuwa kwa ajili ya wanafunzi zaidi wa Kihindi, na wengine waliishi katika majengo ambayo niliyataja kabla kuwa yalikuwa majengo yaliyoitwa SILAB, ambayo yalikuwa yakupokea ‘Manamba’ waliokuwa wakienda kufanya kazi kwenye mashamba ya mkonge. Majengo haya yakageuzwa kuwa hosteli za wanafunzi wa sekondari. Majengo haya yalifahamika baadae kama vigaeni kwani yaliezekwa kwa vigae na yalikuwa mbele ya ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Wanafunzi wapya tulipangwa kwa kufuatia tulikotoka, wale waliomaliza darasa la nane wakapangwa Form 1A, sisi wa darasa la saba tukapangwa Form 1B. kama ilivyokuwa kawaida miaka ile kila mwalimu wa somo alikuja kutuigawia vitabu. Masomo yalikuwa Arithmetic, Algebra, Geometry, Biology, Physics, Chemistry, Civics, Kiswahili na English, na kila somo lilikuwa na kitabu chake. Masomo yakaanza, si Primary tena, wanafunzi wengine walikuwa watu wazima sana, kuna walioamua kuacha shule mapema sana. Darasani kwetu nawakumbuka wawili, Abasi na Mponzi hao walikatisha masomo kuenda kuanza maisha.
Waalimu walikuwa wengi, mwalimu wetu wa darasa alikuwa Mmarekani aliyeitwa Mr Hert, kulikuwa na tatizo kidogo kuelewana, mwalimu ana Kiingereza cha Kimarekani na sisi tuna mchanganyiko, kuna waliosoma Iringa mjini, kuna waliotoka vijijini na kulikuweko na wenzetu wengine wamtoka Njombe, tukaweko wengine ambao Kiingereza tulifunsdishwa na waalimu wa Kihindi, basi kuna wakati Mr Hert alikuwa akiongea peke yake hakuna aliyekuwa akimuelewa. Mr Hert na mkewe ambaye nae alikuwa mwalimu palepale walikuwa Wamarekani walioingia nchini chini ya mpango ulioitwa Peace Corps, hawa walikuja nchini baada ya mwalimu Nyerere na rafiki yake rais wa Marekani John F Kennedy kuafikiana kuhusu kuleta wataalamu wa kilimo na elimu kuja kufanya kazi sehemu mbalimbali nchini. Waalimu wengine walikuwa Mrs Rodrigues huyu alikuwa Mgoa, Mr Dhanani mwalimu wa Book Keeping na ndie alikuwa mwangalizi wa hostel iliyokuwa jirani na shule. Darasa letu lilikuwa na wanafunzi wa aina mbalimbali kama kawaida, wanafunzi walikuwa ‘serious’ kuwa wamkuja kusoma, wengine akina sisi tupo tu kufurahia kuwa sekondari, wengine wenye vituko kama bwana mmoja alikuwa mfupi lakini mwenye vituko vingi aliyekuwa akijiita ‘Kojo’ baadae ‘The artful Dodger’ kutokana na ubingwa wake wa kutoroka vipindi. Huyu bwana alikuwa mpiga ngoma mzuri wa ngoma aliyeaminika na kabila lake wakati wa kupiga ngoma ya Mganda.
Shule ilikuwa na viunga vingi vya maua, na kulizungushwa spika kwenye miti na tulikuwa tukitegemewa kusikiliza taarifa ya habari kupitia spika hizi. Pia uliweza kuitwa na Headmaster kwa kutumia spika hizihizi jambo ambalo liliashiria kuna tatizo zito.



Ratiba ya ujumla ilianza saa moja na nusu asubuhi kwa usafi kisha kuingia darasani mpaka saa nne ambapo kulikuwa na mapumziko. Masomo yaliendelea mpaka saa sita na robo hivi, kisha kulifuatia mapumziko ya chakula cha machana. Wale waliokuwa wakiishi ‘hostel’ walikuwa wakirudi kula na kisha kuwahi shuleni kwa masomo ya mchana. Mlo week days ulikuwa ugali wa unga wa njano maarufu kwa jina la Yanga. Masomo ya mchana yaliendelea mpaka saa tisa na nusu na baada ya hapo kuliendelea shughuli za nje zikiwemo michezo, kilimo, na fani nyingine.
Shamba la shule lilikuwa chini katika eneo kati ya uwanja wa mpira na eneo la FFU. Mwaka 1968 kulikuwa na mpango wa kutengeneza bwawa la samaki, Wanafunzi wakishirikiana na Mr Hert walichimba sana pale sikumbuki kama mradi ule ulifanikiwa. Kwa kuwa wamo wasomaji waliokuwa nami shuleni wakati huo hakika watanikumbusha. Huku shamba nako kuliwahi kuwa na vituko ntaelezea baadaeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee
Categories: Iringa, Uncategorized
KUTOKA KWA EDMUND MYAVA…EX STUDENT LUGALO……Hakika John….. namkumbuka John Mponzi (the late) ambae tulisoma wote St. Mary’s. Aliacha shule tukiwa Form 2 akapata Kazi ya bwana afya. Nakumbuka hata shuleni pale St Mary’s alikuwa prefect anaeshugulikia usafi………baadae miaka ya 80 nilikutana nae Mbeya akiwa Bwana Afya wa Wilaya. Kisyeri Chambiri tulisoma nae Kibaha wakati huo akitokea Ifunda. Saleh Ahmed alikuwa rafiki yangu mda wote tuliokuwa Lugalo na baadae nilikutana nae miaka ya 90 mwishoni Morogoro akiwa mfanyabiashara wa pamba na baadae alihamia Mwanza au Shinyanga……ASANTE KWA KUMBU NZURI
LikeLike
Naboth mbembati , Emmanuel Mkusa, John Mzungu villikuwa vichwa balaa! huyu naboth na Emmanuel Mkusa wakl wapi jamani ila John Mzungu nilikutana nae Dar es salaam siku moja mtaa wa Samora nikamwita kwa jina lake hiyo akashangaa sana. baada ya kusalimiana na mazungumzo mafupi aliniambia yuko mwanza au shinyanga nimesahau kidogo. Emmanuel Mkusa namkumbuka akifanya mchezo wa maigizo nimesahau ni igizo gani lakini akishika fimbo na kuita “ikwela ! ikwela !. Bwana Kitime unakumbusha mengi sana na library yako ya kumbukumbu imesheheni.
LikeLike