LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 29


St Mary’s Primary School

Kutokana na kumbukumbu hizi kuna wachangiaji wawili wamejitokeza wa kwanza ni Engineer na Mwanasheria EDMUND MYAVA…Bwana Myava tulikuwa darasa moja pale Lugalo Secondary School. Tulizoea kumuita Umfundisi, kutokana na jina jingine la Pastor Steven Kumalo aliyekuwemo katika kitabu cha Cry the Beloved Country, Pastor Kumalo aliitwa Umfundisi na watu wake waliompenda na kumheshimu, kwangu mimi Myava kila siku ni Umfundisi. Hivyo basi Umfundisi ameandika hivi ‘Hakika John….. namkumbuka John Mponzi (the late) ambae tulisoma wote St. Mary’s. Aliacha shule tukiwa Form 2 akapata Kazi ya bwana afya. Nakumbuka hata shuleni pale St Mary’s alikuwa prefect anaeshugulikia usafi………baadae miaka ya 80 nilikutana nae Mbeya akiwa Bwana Afya wa Wilaya. Kisyeri Chambiri tulisoma nae Kibaha wakati huo akitokea Ifunda. Saleh Ahmed alikuwa rafiki yangu mda wote tuliokuwa Lugalo na baadae nilikutana nae miaka ya 90 mwishoni Morogoro akiwa mfanyabiashara wa pamba na baadae alihamia Mwanza au Shinyanga……ASANTE KWA KUMBUKUMBU NZURI” John Mponzi alikuwa mwenzetu ambaye alikuwa na tabia zake tofauti kwanza nakumbuka kawaida yake ya kusimamisha kola ya shati yake kitu kilichokuwa kikiashiria umwamba nyakati hizo. Tulipofika form two alitueleza kabisa kuwa anaacha shule aende akawe Medical Assistant. Kuwa Medical Assistant miaka hiyo lilikuwa jambo kubwa. Na kama alivyosema Umfundisi, John alikwishaanza kuwa prefect wa usafi shuleni kwao wakiwa bado shule ya msingi, mwenzetu alitambua alichokuwa akikitaka mapema sana. Nilikutana na John Chunya kati ya mwaka 1988 au 89, hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza toka alipotuacha mwaka 1969, Alikuwa Afisa Afya wa Wilaya. Alinipokea vizuri tukawa na mengi ya kuongea na baada ya hapo sikumuona tena. Mungu amlaze pema peponi.
Katika maelezo yake Umfundisi ametaja shule ya St Mary’s Primary School. Hii ilikuwa shule iliyoendeshwa na kanisa Katoliki, shule hii ilikuja kuitwa Kichangani Primary School. Sisi tulikuwa wanafunzi tuliojikuta katika yale mabadiliko ya kutaifishwa kwa shule binafsi. Hivyo Consolata iliyokuwa inaendeshwa na kanisa katoliki ikawa Chemchem, High Ridge iliyokuwa ikiendeshwa na Wabaniani ikaja kuwa Wilolesi, Aga Khan Secondary ikaja kuwa Lugalo, na nakumbuka kuna wanafunzi hawakupenda kabisa jina hilo jipya. St George and St Michael ikaja kuwa Mkwawa, Aga Khan Primary ikaja kuwa Shabaha Primary.
Kisyeri Chambili ndiye niliyemtaja kuwa tulikuwa darasa moja primary na sisi wawili tulikuwa Waafrika wawili tuliochaguliwa kwenda sekondari kutoka shule ya msingi ya Aga Khan. Tulianza wote sekondari nae kama ilivyokuwa kwa John Mponzi alifahamu anataka kuwa nini. Nakumbuka kabisa akinieleza kuwa anataka kuwa ‘Engineer’, hivyo basi aliomba uhamisho na kuhamia shule ya sekondari ya ufundi Ifunda wiki chache baada ya kuingia sekondari. Tukiwa bado form 1, Kisyeri aliwahi kuniandikia barua kuwa wana project wa kutengenza Hoovercraft shuleni kwao. Nae hatimae alikuja kuwa civil engineer kama alivyopanga na pia kuingia katika siasa na kuwa Mbunge zaidi ya mara moja.
Saleh Ahmed alikuwa Mwarabu, familia yake walikuwa na duka lililoangaliana na soko la zamani la Iringa , nae pamoja na Kisyeri tulikuwa wote Aga Khan Primary, na kuchaguliwa kujiunga na Aga Khan Secondary. Kuna wakati alienda Uarabuni nadhani ilikuwa Yemen, akawa anafanya kazi huko, siku moja aliporudi Tanzania nilimuuliza kama tunaweza kusindikizana huko ili nitafute kazi, alinambia ‘Kazi za kule huziwezi’. Baadaye nilipokuja kuelewa zaidi kuhusu mazingira ya Yemen nilikuja kuelewa kwanini alikataa nisiende huko. Niliwahi kukutana nae Morogoro pia miaka mingi iliyopita sijui yu wapi siku hizi.

*********************************************************************************************************************************************

Mchangiaji wa pili ni Mwanasheria SHUKURU MOHAMED, Shukuru alikuwa mwana Barabara Mbili mwenzangu, sisi wote tulikuwa watoto wa Makorongoni, na kama alivyosema mwenyewe babu yangu Mzee Raphael Kitime alikuwa mwalimu wake wa tuition ya Kiingereza. Mimi na Shukuru tulipenda sana kashata za nazi, wakati ule zilikuwa zikipatikana hasa kwa rangi tatu, njano, pinki na nyeupe, ninaamini zilikuwa zikitengenezwa vizuri kuliko hizi kashata za siku hizi. Halafu ikumbukwe kuwa Iringa hakuna minazi.
Shukuru ameandika hivi “Naboth mbembati , Emmanuel Mkusa, John Mzungu villikuwa vichwa balaa! huyu Naboth na Emmanuel Mkusa wako wapi jamani? Ila John Mzungu nilikutana nae Dar es salaam siku moja mtaa wa Samora nikamwita kwa jina lake hilo, akashangaa sana. baada ya kusalimiana na mazungumzo mafupi aliniambia yuko Mwanza au Shinyanga nimesahau kidogo. Emmanuel Mkusa namkumbuka akifanya mchezo wa maigizo nimesahau ni igizo gani lakini akishika fimbo na kuita “ikwela ! ikwela !. Bwana Kitime unakumbusha mengi sana na library yako ya kumbukumbu imesheheni”.
Naboth Mbembati na Emmanuel ‘Katuluta’ Mkusa tulikuwa darasa moja Consolata Primary School darasa la tatu na la nne kabla sijahamia Mbeya. John ‘Mzungu’ Komba alikuwa madarasa ya mbele. Na ni kweli watu hawa walikuwa ‘vichwa’. Tulipokuwa form 2 au 3 Emmanuel alikuwa bingwa wa hesabu na hata kupata zawadi kwa kuwa wa kwanza katika mashindano ya hesabu yaliyokusanya mabingwa wa hesabu toka Kenya Uganda na Zambia. Toka enzi hizo za darasa la tatu Naboth alikuwa mshika namba moja. Emmanuel alikuwa 3A, mimi, Naboth, Chesus Lutego, Pius Mlowe tulikuwa 3B. Tulikuja kutana tena sekondari baada ya miaka mingi. Kati ya siku nakumbuka ambazo Naboth alionyesha ukali wake ni siku moja ambapo tulikuwa na waalimu waliokuwa kwenye mazoezi, mmoja akawa anatufundisha Geometry, zile hesabu za Proove that…… Basi mwalimu alihangaika na hesabu moja mpaka karibu ya mwisho wa kipindi akawa haja proove, kila akifika katikati anajikuta kakosea akawa anafuta ubao, wahuni wakaanza kukohoa eti vumbi la chaki limezidi, ndipo Naboth akanyoosha kidole na kwenda mbele na kuimaliza hesabu ile. Ndipo mwalimu nae akaunganisha,’Thats right QED. Quite easily done’
Sijui hadithi ilitoka wapi, lakini japo hatukuwa darasa moja na John Mzungu, sisi tulikuwa wadogo tuko darasa la 3 yeye nadhani alikuwa darasa la 5 au la 6, tulikuwa tukiambiwa alikuwa na akili sana darasani, nakumbuka tulikuwa tuna hadithiana kuwa ana kitabu kikubwa aliletewa toka Ulaya, kilikuwa na majibu ya mitihani yote ndio maana ana pasi. Binafsi John alikuwa role model wangu wa kuanza kutumikia kanisani, nilikuwa ninamwona anapendeza sana na zile kanzu za kutumikia, bado nina picha ya John akiwa ameshika cheteso akitumikia huku Padri Oli akisoma Misa. John nilikuja mkuta Aga Khan Secondary tena nilipoingia kidato cha kwanza, nae nimeshawahi kukutana nae miaka mingi iliyopita akanambia yuko Mwanza. Sina Uhakika yuko wapi.
Naboth Mbembati au kwa wadhifa wake wa sasa Profesa Mbembati, yupo Dar es Salaam amestaafu. Alikuwa mwalimu chuo cha udaktari MUHAS. Huyu ananidai shilingi yake. Baada ya kupewa zawadi ya kamera kwa kuchaguliwa kuingia sekondari, nilianza biashara ya kupiga picha wakati tukiwa form 1, nikamwambia kuwa naweza kumpiga picha, na nikafanya hivyo lakini picha ‘ikaungua’ na hela aliokwisha kunipa nilikuwa nimeisha ila.
Katika ukumbi wa Lugalo kulikuwa na siku zinaonyeshwa sinema mbalimbali, wanafunzi tulikuwa tukichanga ili sinema ziweze kupatikana, madirisha ya ukumbi yawekwa mapazia meusi, kukawa na giza tosha la kuweza kuangalia sinema. Mwalimu wetu Mr Sandhu ndie alikuwa mtaalamu wa mashie ile ya kuonyesha sinema. Filamu zilizosisimua na kuacha hadithi zilikuwa 100 Rifles ya Jim Brown na Raquel Welch, nadhani kwa kuwa kulikuwa na kipande Jim Brown alionekana akiashiria kufanya mapenzi na Raquel Welch. Hadithi nyingi zilianza kuhusu utengenezaji wa kipande kile cha filamu.Kulikuwa na sinema za Dracula, sinema za kutisha, kunyonya damu, kuchinja watu na kadhalika, Emmanuel akaanza kutunga michezo ya kuigiza yenye kutisha kama zile sinema za Dracula, nakumbuka character mmoja alikuwa akiitwa Lulapangilo, huyu ndie aliyekuwa na nguvu za kupigana na nguvu za giza katika michezo aliyoandika Emmanuel. Tulikuwa tukienda maktaba ya pale mjini kuazima vitabu vya mtunzi aliyeitwa Dennis Wheatley ili tujue zaidi kuhusu hadithi za kichawi kwa ajili ya kuboresha mchezo. Nakumbuka vitabu vichache tulivyovisoma navyo ni The Devil rides out,The Satanist na The Haunting of Toby Jugg. Vitabu hivyo ndio vilisaidia kutengeneza michezo kadhaa ambayo ilichezwa pale shuleni na nakumbuka pia Iringa girls, na ilionekana kutisha hasa kwa kuwa kulikuwa namatumizi ya taa za rangi, juisi ya zambarau badala ya damu na kadhalika. Nafikiri ni wakati huu Emmanuel alipoanza kusisitiza kutumia jina la kati la Lundere pia.
Ndugu yangu Shukuru,nasikitika kukwambia kuwa Emmanuel Lundere Mkusa alifariki tarehe 17 July 2017 huko Namibia na akazikwa hukohuko kwani familia yake iko huko.

Categories: Iringa

4 replies

  1. Asante Sana Baba yangu kwa historia nzuri ya Marehemu Baba yangu ndugu John Mponzi nashukuru pia na yeye amewahi kunisimulia ushindani wenu wa kimasomo hapo lugalo na kichangani primary school. Namba yangu mm mtoto wa John 0688123608 ninaomba stori zinu zaidi mm kama kijana wenu ni weze kuzitunza vizuri kwa faida ya vizazi vyetu kwani historia ni dila ya maisha Asante Sana baba na mungu akubariki

    Like

    • Naomba kama Ina wezekana nipe NBA ya mtu aliye Soma na baba yangu John Mponzi Marehemu hili niulize mengi na mm nipate kutunza kumbu kumbu za baba kuhusu huyo engineer baba kashawahi tudokeza na alisema ikuwa Bora Sana darasan hata yeye alikuwa bright Sana amekufa Ana degree ya cuo kikuu Cha dar nazani taifa Lilijua kipawa chake hasa alipenda kusoma Sana

      Like

  2. Ninaomba picha hiyo ya John nipige copy baba yangu na amini John mungu alimpa kipaji kutokana na mitihani aliyo pitia katika maisha yake yule amezaliwa yatima. Nazani ata mungu Ali mpenda Sanaalimpakazi nzuri yoyote takayetaka kunipa story ya baba 0688123708 alikuwa kichwa answer ata kwenye masomo yake ya kuchukuwa degree mwaka semanini hapo chuo kikuu Cha daresalaam Alikuwa best student he was very genius person.

    Like

Leave a reply to Charles John mponzi Cancel reply