LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 32


Mr F D Ntemo

Kufikia mwaka 1970, Aga Khan Secondary School ilikuwa rasmi sasa inaitwa Lugalo Secondary School, kilikuwa kipindi cha mwamko mpya wa uzalendo na siasa ya Ujamaa ilikuwa ndio inaanza. Shuleni kulikuwa na tawi kubwa la TANU Youth League, chini ya mwenyekiti Maneno Mbugi na Katibu wake Andrew Mtweve, jamaa aliyekuwa na heshima hata kwa sisi wanafunzi wenzie.
Tulianza kusoma vitabu vya Mwalimu Nyerere hasa kile kilichoitwa Ujamaa. Shughuli mbalimbali zilizo lenga kuelewa Ujamaa na Kujitegemea zikawa zinahamasishwa. Pamoja na Mwalimu Kikudo kuwa anafundisha ‘Siasa’, kazi za kilimo zikahamasishwa na kukaanzishwa shamba la shule na mradi wa bwawa la samaki, ambalo sikumbuki kama lilifanikiwa. Nyuma ya shule kulikuwa na mambanda ya kuku wa mayai na pia kukawa na duka la shule kwenye kona moja ya jingo la Domestic Science. Jengo la hilo ndilo lililo karibu na round-about lilijengwa mwaka 1969. Nilishwawahi kuwa muuza duka hilo la shule, na baadae nikapewa jukumu la kulisha kuku siku za week end kwa kuwa nilikuwa naishi jirani na shule. Shamba lilifanikiwa na kulipandwa mahindi, na ninakumbuka yalistawi vizuri sana. Kuna siku moja enzi za Mr Ntemo ambapo wanafunzi wa kidato cha pili walikuwa shambani na wengine kuanza kutafuna ‘migagi’ ya mahindi ya shule. Binti wa kihindi aliyekuwa headgirl wakati ule  alishuka kule chini shambani sijui kutafuta nini, lakini akafanyiwa fujo na baadhi ya wanafunzi kwa kutupiwa madongo. Akaenda kushtaki kwa Mr Ntemo. Form 2 tuliitwa kwenye ule ukumbi wa Domestic Science, na  kesi ikaanza. Kosa la kwanza lilikuwa kutafuna ‘migagi’ ya shule. Nakumbuka kabisa jibu la Andrew ‘Kojo’ Pili, ambalo liliungwa mkono na Elly Mwambenja kuwa wao kabila lao huwa hawali mabua ya mahindi. Kosa la pili lilikuwa ni kumrushia madongo Headgirl, kwa kuwa kwa makosa yote ilikuwa vigumu kumkamata mhusika, kama kawaida ya shuleni tulipata adhabu ya ujumla, ajabu sikumbuki ile adhabu nadhani ilikuwa ndogo mno kulinganisha na utundu wetu.

Kitabu cha Historia
Kitabu cha Ujamaa
Kitabu cha Biology


Waalimu wetu walikuwa wengi na walikuwa wakibadilika, na kama ilivyo kwa wanafunzi nao walikuwa na mambo yao yaliyowafanya wapate nafasi katika kumbukumbu zangu, ngoja nianze kuwataja baadhi najua wenzangu tuliokuwa nao wataniongezea majina mengi ambayo yamenitoka.
Mr F D Ntemo : Headmaster aliyekuja kuchukua nafasi ya Mr Sheikh na ni katika zama zake ndipo jina la shule kuhama kutoka Aga Khan Secondary kuwa Lugalo Secondary. Alikuwa akiishi kwenye nyumba ya kona inayoangaliana na uwanja wa Saba saba. Aliendelea na maisha hata kuja kuwa balozi wa Tanzania nchini Sweden. Alikuwa na Volkswagen nyekundu kwa ajili ya usafiri wake. Mzee Ntemo alifia Dodoma
Mr S Hassan: Headmaster ambaye alichukua nafasi ya Mr Ntemo.
Mr Kikudo:  Mwalimu huyu ambaye daima sigara ilikuwa mdomoni alikuwa pia hapati tabu kutembeza viboko. Alikuwa mwalimu wa Kiswahili na siasa. Jina la utani lilikuwa Kipili
Mr Kanole: Mwalimu wa Jiografia
Mr Ladha: Mwalimu wa Jiografia
Mrs Ladha: Mke wa huyo juu
Mr Sandhu: Mwalimu wa physics na chemistry, mvuta sigara mwingine aliyekuwa mkimya kwa tabia, na ndie alikuwa anaendesha projector ya sinema.
Mr Maulaga mwalimu wa Biology na mcheza hockey mzuri. Jina la utani Mackean, jina lililokuwa la mwandishi wa kitabu cha biology tulichokuwa tukitumia wakati huo ‘Introduction to Biology’. Pia alikuwa akifundisha physics na sentensi yake aliyokuwa kiirudia rudia  ‘Moving an immovable body with an irresistible force”
Mr Stone: Huyu alikuwa Mu Irish, mwalimu wa Kiingereza aliyekuwa mrefu kiasi aliishi kwenye nyumba ya serikali ya ghorofa  iliyokuwa karibu na makaburi ya ‘wazungu’.
Miss Uschina: Mwalimu wa kike wa Kirusi aliyekuwa bingwa wa hesabu, pengine hata sie wengine ambao hesabu zilikuwa kama uchawi Fulani has zile za sine na cosine hatukufeli sana hesabu kwenye mtihani wa Form 4 kwa sababu ya mwalimu huyu. Nae aliishi nyumba moja na Mr Stone. Miss Uschina alikuwa mwalimu wa Additional Mathem,atics (Pure Maths).
Mr Olle Ille huyu alikuwa Mnorwegian nae alikuwa mwalimu wa hesabu
Mr Verma: Chemistry na hesabu
Mrs Dawn mwalimu wa Chemistry
Mr Hert  na Mrs Hert: Hawa walikuwa Wamarekani na nadhani Mr Hert ndie aliyefanya watu wakaanza kuvaa kaptura za bichikomba.
Mrs Rodrigues: Mgoa huyu mwalimu wa Historia
Mrs Stanley: Huyu alikuwa Mmarekani alifundisha Biology na hata Kiingereza. Kwa harakaharaka naweza kuwakumbuka hawa.

KAMA UNA HADITHI AU PICHA ZA ENZI NINAYOZUNGUMZIA NA AMBAZO UNGEPENDA WATU WAKUMBUKE NITUMIE jkitime@gmail.com au utoe maoni yako katika eneo la comment chini ya habari hii.

Categories: Iringa

4 replies

  1. Hakika John kumbu zimefifia au kutoweka kabisa………katika orodha ya walimu pia walikuwepo;
    1. Mr Jiran Mwalimu wa kemia maarufu sana wa kutema mate (kikolosi?)…huyu tulimkuta kwenye maabara ya kemia …..
    2. Mrs Hoja….sikumbuki Mwalimu wa nini(civics?) …huju tulimkuta kwenye chumba cha domestic science. Alikuwa na michapo kuhusu maisha ya wanafunzi na aliahidi kuwa angetufanyia social evening na wanafunzi wa Iringa Girls…….baadae alikwenda kuwa Headmistress wa Iringa girls na ile ahadi yake hakuwahi kuitimiza…..hakika UWANA ITAMWA!….
    3. Mr Mvungi Mwalimu wa ……geograph? huyu alikuwa akicheza basket ball na wanafunzi…akina Mkusa, Msolla, Kipate, Mhekwah, n.k.
    4. Mr Magelewanya…sikumbuki kama alitufundisha lakini naamini alikuwa Mwalimu wa hesabu na fizikia maana miaka ya baadae Lugalo alijulikana kama “Magelewanya Fomular”

    Mwalimu Kikudo miaka ya 2000 nilikutana nae Magogoni akiwa anafundisha pale (TPSC).

    Mwalimu Sandhu ambaye umemtaja sana pia alitufundisha biology na miaka ya baadae alihamishiwa Dodoma (Bihawana?) kwa taarifa nilizozipata baadae nikiwa Morogoro.

    Ulimtaja Mr Hert Mwalimu wetu…..moja wa wanafunzi aliye kuwa mbele yetu alikuwa inspired sana na Mr Hert …….huyu siyo mwingine ila STEVEN MATONGO aliekuja kuwa Mwalimu wa kingereza pale Morogoro International school..,..Mara ya mwisho nilionana nae mwishoni miaka ya 90….. …Asante John umefanya nijione yule kijani wa Shamba Mtwivila enzi hizo…..

    Like

  2. Asante sana Kaka John Kitime…Nimeshare hii simulizi kwa wenzangu niliosoma nao Lugalo Secondary Iringa Miaka ya Themanini!!!

    Like

Leave a reply to MATHAYO MWAKAGAMBA Cancel reply