Kama kawaida ya watoto wote duniani, watoto wa Iringa tulikuwa na michezo mingi sana, mingine ya salama mingine hatari kabisa. Wakati tukiwa wadogo hatujui hili wala lile tulicheza sana mchezo wa baba na mama, na mara nyingine tunaanza na maandamano ya harusi kisha mnakuwa baba na mama, mnakuwa na watoto mama anapika wakati baba anaenda kazini, tulikuwa tunaiga yale tuliyoyaon kwa wazazi wetu. Nilipoingia darasa la kwanza na kuanza kujuana na watoto wengine na michezo ikawa mingi zaidi kulikuwa na michezo kama ‘mbinga’ huu ulikuwa mchezo ambao tulikuwa tunachukua vizibo na kutoboa matundu mawili kisha kupitisha uzi na kuzungusha kisha kuvuta, basi kizibo kilikuwa kikizunguka na kamba ikivutika kama mpira. Kuna wenzetu walikuwa wakichonga ‘mbinga’ za miti, na zilikuwa zikitoa mvumo uliokuwa ukitufurahisha. Mchezo huu ni wazi ulikuwa ukichezwa toka zamani na babu zetu kwani kulikuweko na wimbo wa Kihehe wa kuimba wakati unazungusha ‘mbinga’ ulikuwa na maneno haya;
Mbinga ya mayombwe kumatanana
Vaitovaga ibume kumatanana
Kulikuweko na pipi pia ambazo tuliziita ‘peremende mbinga’, hizi zilikuwa zikija na uzi wake kabisa. Unachezea kisha unakula mchezo umekwisha.

Kulikuwa na mchezo wa pia, kijiti kilichochongwa na ncha nacho ilikuwa ni kukipiga kwa kamba ili kizunguke, na kulikuwa na mabingwa wa mchezo huo pia. Awali tulikuwa tukichonga pia wenyewe baadae zikaanza kuja pia zilizochongwa kwa mashine na kuuzwa madukani

Kulikuwa na michezo mbalimbali ya goroli, ikiwemo ex, au kucheza za plei, ambapo watoto walikuwa wakilambishwa plei na zinazaliana hakuna kurudi kwenu mpaka ulipe plei si mara moja tuliona mtu analambishwa plei mpaka analia au akatakiwa alipe kitu ndio asamehewe, watu walikuwa wakinyang’anywa hata nguo na kurudi makwao kukutana na makubwa kwa wazazi wao.

Kulikuwa na mchezo wa kuzungushwa ndani ya tairi, hu ulikuwa mchezo ambao mtoto mmoja aliinga kwenye tairi jisha wenzie kuanza kulizungusha mchezo

Kulikuwa na mchezo unaitwa Nyonga membe, kuna miti fulani ambayo ilikuwa inawezekana kuondoa mti wa ndani na likabaki gamba b likiwa kama bomba. Kwenye bomba hilo ukiweka bua mwanzo na mwisho kisha ukasumukuma kwa nguvu bua moia wapo kwa kutumia kijiti, hewa iliyokatikati ya haya mabua mawili ilisababisha bua lisilosukumwa kutoka kwa nguvu na hizo tuliita bunduki. Mchezo huo ulikuwa ukipendeza zaidi mkicheza wakati mnaogelea. Hivyo ulikuwa maarufu sana tuliposhuka chini Ruaha kwenda kuogelea, na miti husika ilikuwa mingi sana kule chini Ruaha.
Badala ya kutumia mabua mara nyingi tulitumia aina ya nyanya pori zilizoitwa ndula.
Kyulikuwa na mchezo unaitwa ‘nago’ huu ulichezwa kwa kutumia mawe yaliyokuwa bapa ambayo yalipangwa haraka kwa kukwepa kupigwa na mpira.

Kulikuwa na mchezo wa kudoda kwa ajili hasa ya wasichana, japo kulikuwa na wavulana mabingwa wa mchezo huu pia.

Sekondari kulikuwa na michezo mingi ya kigeni zaidi na kulikuwa na vifaa vingi vya michezo. Kulikuwa na magongo ya kuchezea Hockey au mpira wa magongo , kulikuwa na vifaa vya kuchezea mchezo wa cricket, basket ball, volley ball, netball, vifaa vya michezo ya riadha kama kutupa tufe, kutupa kisahani, kutupa mkuki, magongo maalumu ya Pole vault, sehemu ya high jump na long jump, na uwanja wa mashindano ya mbio uliokuwa ukiwekewa mistari mata kwa mara. Kulikuwa na utaratibu wa mashindano ya ndani ya shule yaliyofanyika baina ya makundi yaliyokuwa yamegawanywa na kupewa majina ya milima ya Meru House, Kibo House, Mawenzi House na Rungwe House kama kumbukumbu zangu bado ni nzuri. Matokeo ya mashindano hayo yaliweza kutengeneza timu za shule za michezo mbalimbali kwani baada ya hapo kulikuwa na mashindano mengi kati ya shule moja na nyingine, na mara moja kwa mwaka kulikuwa na mashindano ya shule zote za sekondari. Niliwahi kubahatika kuwemo katika timu ya shule ya cricket katika mashindano ya shule kadhaa za sekondari. Mashindano haya yaliyofanyika katika viwanja vya Mkwawa sekondari, yalihusisha timu za shule ya Mkwawa , Iyunga ya Mbeya na shule yetu ya Lugalo. Tulikuja kuwa washindi wa pili Iyunga ikichukua kikombe. Katika mchezo ambao sitausahau ulikuwa ni wakati nilipochaguliwa katika timu ya hockey ya mkoa wa Iringa, mashindano yalikuwa yafanyike Zanzibar. Kwanza kipindi hicho Iringa ilikuwa kwenye karantini ya ugonjwa wa Kipindupindu, kutoka nje ya mji ilikuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa daktari wa mkoa. Kibali hicho ilipatikana, lakini kwa mbinde alamanusra tufutwe kwenye yale mashindano. Tulifika Dar es salaam na kusafiri kwenda Zanzibar kwa ndege ndogo, nauli shilingi kumi na tano. Tulipofika Zanzibar tulikuta timu za wenzetu kutoka mikoa mingine wamekabidhiwa vyumba katika magorofa yaliyoko Michenzani. Ilikuwa mtu unatafuta chumba unachoona kinafaa kulala, vyumba vilikuwa vingi tu. Majengo haya yaliyojengwa na serikali yalikuwa pia na vitanda vyenye magodoro, majiko ya umeme, lakini yalikuwa matupu hayana watu. Kuna vitu viwili vilinitokea kwa mara ya kwanza maishani katika safari hiyo. Kwanza kupanda ndege, na pili ilikuwa ratiba ya chakula tulioikuta Zanzibar. Jioni tulikaribishwa chakula , tukaletewa chai na maandazi, tukayala vizuri tukajua ni mwanzo halafu ndio kitakuja chakula cha jioni, tukashangaa tulipoambiwa hicho ndicho chakula cha jioni, tuonane kesho yake.
Tulipofika uwanjani tukajikuta tunaitwa Team Kipindupindu, wenzetu walijua hatutafika kwa ajili ya kipindupindu. Baada ya hapo jina likapata maana zaidi kwani sisi tukawa ndio vibonde ambapo kila timu ilitufunga si chini ya magoli matano. Mechi yetu ya mwisho ilikuwa baina ya sisi na timu kutoka Tanga. Timu hiyo ingekuwa na pointi sawa na timu ya Dar es Salaam baada ya kutufunga, jambo ambalo lilikuwa halina ubishi, hivyo Dar es Salaam wakatuomba sana tusikubali kufungwa magoli mengi ili wao washinde kwa idadi ya magoli. Tulijitahidi sana, Dar es Salaam wakitushangilia kwa nguvu zote, mwisho wa mchezo tulifungwa goli moja tu, huwezi kuamini tulikuwa tunajishangilia utadhani ndio tuliochukua kombe.
Nadhani ilikuwa mwaka 1969 au 70 kukawa na mashindano ya shule za sekondari yaliyofanyika Ifunda Technical School. Wanamichezo tulikuja kuchukuliwa na basi la Relwe pale shuleni kupelekwa Ifunda, sasa kulitokea jambo la ajabu sana mjini, ikaja habari kuwa kuna watu wawili walikuwa wakifanya mapenzi wakanatana na walikuwa wamepelekwa hospitali ya serikali Iringa. Hayo yakawa mazungumzo ndani ya basi kuhusu kinachofanyika mpaka watu wananasana. Ilisemekana ni uchawi wa Kihehe unaitwa Lutambulilo.
Kati ya timu maarufu za shule za soka zilikuwa Malangali Secondary na Tosamaganga Secondar. Iringa mjini kulikuwa na timu nyingi zenye watu maarufu wengi, nianze na timu ya Boni, hii ilikuwa ni timu ya waliojiita wazazwa wa Iringa mjini ilikuwa kifupicha Born Town Football Club, ilikuwa timu ya watemi kweli, kulikuweko na ukoo uliokuwa ukiogopwa wa akina Kibasila, jezi ya timu hii ilikuwa mashati meusi. Hawakuwa na shida kukatisha mchezo katikati na kuondoka na mpira kama waliona wanafungwa. Kulikuwa na timu ya Relwe timu ambayo nayo ilikuwa nzuri na pia ilikuwa na watu watemi sana,timu nyingine ya kukumbuka ilikuwa Santos, hii ilikuwa chini ya Mreno mmoja aliyekuwa na gereji iliyoitwa Santos Garage, mwenyewe ndie alikuwa golikipa wa timu. Santos alikuja kufukuzwa nchini baada ya kufanyika majaribio ya kulipua kituo cha mafuta cha TAZAMA pale Lugalo na pia bomu moja kukutwa limetegwa kwenye daraja Ruaha ambalo halikulipuka. Nyakati hizo zilikuwa ndizo za kupigania Uhuru nchi zilizo kusini mwa Afrika. Zambia tu ndio ilikuwa huru, Msumbiji ilikuwa bado Mozambique, Zimbabwe ilikuwa bado Rhodesia, Namibia ilikuwa bado South West Africa, mambo mengi yalikuwa yakifanyika kuhujumu Tanzania iliyojulikana kama kituo cha wapigania Uhuru. Kulikuwa na golikipa Muhindi Manji nadhani alikuwa akidakia timu ya African Wanderers football club klabu nyingine kongwe ya Iringa.
Categories: Iringa
Safi sana kumbukumbu hiyo hata mimi umenikumbusha mbali sana. Nimeifurahiya sana .
LikeLike