LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 41


Kasha la biskuti

Kwa wale walionaza kufatilia mikasa yangu tangu mwanzo watakumbuka kuwa nilianza kumpenda ‘mchumba’ wa kwanza wakati nikiwa aidha nursery au darasa la kwanza. Mchumba wangu huyu alikuwa mwanafunzi pale Iringa Middle School, shule iliyokuwa mahala ulipo uwanja wa Samora kwa sasa. Kwa vyovyote alikuwa mkubwa sana kwangu kwani shule ya Middle ilianzia darasa la tano hadi la nane. Ninachokumbuka ni kuwa alikuwa akiitwa Lidya. Sikuwa naona aibu kuwambia wanafunzi wenzie kuwa namtafuta Lidya na nitamuoa, nadhani walikuwa wakinicheka sana. Bahati mbaya hata sura ya Lidya siikumbuki. Wakati huohuo nikawa na mchumba mwingine, huyu alikuwa rafiki mkubwa wa mama yangu mzazi. Aliitwa Mwalimu Lea, nadhani Mwalimu Lea ndie aliyeanza kunitania kuniita mchumba, na mimi nikalichukulia jambo lile ‘vere serious’. We fikiria nilikuwa nikienda kwake, alikuwa akinipa chai ya maziwa na biskuti za Marie. Hizi biskuti zilikuwa zikiuzwa kwenye videbe vidogo na zilikuwa tamu sana. Siku moja mume wa mwalimu Lea alinikuta na kunywa chai, kwa sauti yake ya bezi yenye mikwaruzo akanambia, ‘Nasikia unataka kumuoa mke wangu?’ Nilipogopa sana nikatimka na kukimbia nyumbani na kufanya jambo ambalo wanaume wengi waliofumaniwa hulifanya, nikajificha uvunguni mwa kitanda, kilikuwa kitanda cha chuma aina ya Banco. Mama aliponiuliza ninafanya nini uvunguni mwa kitanda, nikamwambia namuogopa Mzee Joseph amesema nataka kumuoa mke wake. Nilichekwa muda mrefu sana kwa woga.
Nilihadithia pia nilipopata ‘mchumba’ wa kihindi aliyeitwa Noor, nae huyu raha yangu ilikuwa kumuangalia akitoka ndani ya nyumba yao na kuingia kwenye gari yao aina ya Volkswagen na mama yake na kuondoka, hakujua hata kama mimi natoka kwetu mitaa ya mbali kumuangalia, uchumba wa Noor ulikufa baada ya rafiki yangu Shukuku kuwataarifu nyumbani siku moja kuwa nimeenda kwa mchumba wangu, adhabu niliyopata ikawa talaka tosha.
Nilikuwa Form 3 nilipokuja na mimi kumpata wangu wa kikwelikweli. Kama ilivyokuwa kwa wavulana wengine wa shule za sekondari, siku za Jumapili tulikuwa tunaenda kutembea Iringa Girls, maarufu kwa jina la Zoo. Sikumbuki ilikuwaje lakini nikaanza urafiki na binti aliyeitwa Asumpta. Muda wa wageni ulikuwa kati ya saa nane mpaka saa kumi, nina uhakika saa za wakati ule zilikuwa fupi sana maana hata kabla hatujaongea la maana kengele ya kwanza ya kuondoa wageni ililia. Na sheria ilikuwa kengele ya pili ikilia lazima wageni wote wawe nje ya geti. Mazungumzo yalikuwa zaidi kuhusu masomo, tabia za waalimu na kadhalika. Siku moja alinipa picha yake, dahh nilikuwa nayo kila mahala. Na zama hizo zilikuwa bado za picha za Black and white, picha za rangi zilikuwa nadra sana. Nakumbuka kuwa na picha ile miaka kumi baadae.
Siku zilizokuwa nzuri ilikuwa siku za sherehe, maana siku hizo wasichana wa Iringa Girls walikuja mjini kwa maandamano lakini wakati wa kurudi walirudi bila mpangilio, lakini hata hivyo hawakuruhusiwa kuonekana wakisindikizana na wavulana. Tayari miaka ya hiyo sherehe zilishaanza kufanyika uwanja wa Samora, hivyo tulianza kwa kuwasindikiza wachumba kwa mbalimbali toka uwanjani mpaka pale kanisa la Mshindo, kisha hapo wasindikizaji tuliingia katika uchochoro mrefu ambao ulianzia hapo na kuishia ilipo NR Hotel. Wapenzi hawakuruhusiwa kuchepuka walikuwa wakitembea barabara kuu wakati sie tuko vichochori. Tukifika kwa Hans Poppe tunaibuka na kusindikiza kiunjanja na hata kuwapa keki au pipi . Kwa mtindo huu tulikuwa tukisindikiza mpaka maeneo ya shule ya Highlands kisha kuwaacha na kuona roho imesuuzika kabisa. Jumapili unavaa vizuri pecos yako na saa nane uko getini unaingia kwa mikogo ili mwenyeji wako ajisikie fahari. Alipoondoka Iringa Girls hatukuwasiliana tena.
Nilikuwa na mjomba wangu ambaye nae alikuwa anakwenda Zoo kila Jumapili, lakini yeye alikuwa ‘serious’ zaidi alikuwa anatafuta mchumba, na alikuwa kamuona Headgirl kanisani na ndoto yake ikawa hapo. Yeye alikuwa anaingia na baiskeli yake spoti, jambo ambalo halikumsaidia kwani Headgirl alikuwa na hamsini zake, kwa kuwa hadithi hii tuliifahamu, tukikutana na yule headgirl mpaka leo huwa namtania kuwa asingemringia mjomba wangu, angekuwa shangazi yangu.

Categories: Iringa

2 replies

Leave a reply to rhumbatz Cancel reply