LEO NIMEKUMBUKA MJI WA IRINGA NILIPOKUWA MTOTO sehemu ya 11


Babu Raphael Kimwagutangu Kitime (aliyekaa kushoto) akiwa na waalimu wenzie Iringa Goverment School (Mlandege) mwaka 1954

Nyumba ambapo kilipo kilabu cha Barabara Mbili, ilikuwa nyumba ya babu yangu, aliijenga kati ya mwaka 1952 na 1954. Nina nakala za barua yake ya tarehe 31 Agosti mwaka 1953, akiomba kupata uhamisho kutoka shule ya NA Middle School, Ikolo, Kyela (NA ilikuwa kifupi cha Native Authority), kwenda Iringa Goverment School (Mlandege), sababu ikiwa kutayarisha nyumba yake kabla ya kustaafu. Alikuja kustaafu mwaka 1954 na kupewa kiinua mgongo cha shilingi 5,366 na senti 7. Kwa maelezo aliyowahi kunipa yeye mwenyewe kiwanja chake kilikuwa karibu na makaburi. Kama nilivyoeleza awali stendi iliyopo katikati ya mji ni eneo lililokuwa ni makaburi. Katikati ya kiwanja alichopewa, kilichokuwa ni kiwanja na 31 Block P Makorongoni, kulikuwa na mti mkubwa ulioitwa kwa Kihehe Mlangali. Wenyeji walimkanya asiukate ule mti kwani wachawi walikuwa wakiutumia mti ule kama kijiwe chao, na wakamuonya kuwa atapata matatizo makubwa akiukata.

Mlangali

Babu aliukata Mlangali ule na kweli ulipoanguka alikuta umening’inizwa tunguli na vifaa vingine vya kushirikina, alichuma mti ule na kuendelea na ujenzi na hakuwahi kupata shida yoyote kama ilivyotabiriwa. Kuishi na babu yangu ilikuwa raha sana, nina uhakika kuwa ni pamoja na juhudi zake mimi nilikuja kuwa msanii, wakati naishi nae kila Jumamosi alikuwa akinionyesha picha kutoka kwenye vitabu vyake na kuniambia niichore. Alininunulia rangi za maji, wakati huo zilikuwa zikiuzwa shilingi moja na senti hamsini, nilinunua filimbi yangu ya kwanza wakati nikiishi na babu. Kulikuwa na siku tulikuwa tukiteremka mpaka mtoni Ruaha, kwanza tulipita pale darajani, daraja la zamani lile lenye nguzo za chuma siku hizi linatumika kwa watembea miguu tu, (daraja hili lilikuwa muhimu katika barabara iliyotoka Capetown Afrika ya Kusini mapaka Cairo Misri), hapa darajani kulikuwa na biashara nyingi, kulikuwa na watu wakifanya biashara ya kuuza bagia, sukari guru, mahindi ya kuchoma na walikuweko wafanyabiashara ya kuchoma nyama kuanzia asubuhi. Tulikuwa tukinunua nyama na pia tulikuwa tukinunua ndoano, baada ya hapo tulitafuta sehemu nzuri kando ya mto na hapo babu akanifundisha kuvua samaki, wakati navua yeye alikuwa kipenda sana kukaa pembeni kufanya hesabu za mafumbo za algebra, alikuwa akijitungia maswali na kuyajibu mwenyewe!!. Vitabu vyake vingi vilijaa maandishi akiwa anafanya hesabu hizo. Baada ya kuvua tulikula nyama tuliyonunua darajani na kurudi mjini na samaki tuliovua kwa ajili ya kitoeo nyumbani.
Siku za kawaida babu aliondoka nyumbani baada ya chakula cha mchana na kuelekea Kijiweni ambako alikunywa pombe mpaka saa 11 hivi na kurudi nyumbani hakuwahi kurudi usiku hata siku moja. Hata hivyo sheria zilikuwa bado za mkoloni, vilabu vya pombe za kienyeji ilikuwa lazima viwe vimefungwa kufikia saa kumi na mbili jioni. Alipofika nyumbani alikuwa akitoa kiti chake cha mhegamo na kukaa kibarazani akiangalia wapita njia na watoto tukicheza. Usiku nilikuwa nahadithiwa hadithi, historia za familia, nafundishwa nyimbo za Kihehe na kadhalika.
Siku moja mwaka 1967 mwezi wa saba hivi kama kawaida yake alienda kilabuni Kijiweni akiwa amesindikizani na ndugu yake. Walifika katika sehemu ambayo mama mmoja waliyekuwa wakifahamiana sana, sitamtaja jina, akaonja pombe kama ilivyo kawaida ya pombe za kienyeji, baada ya kuonja tua akajisikia vibaya akamwambia nduguye warudi nyumbani haraka, kwani anahisi amekunywa sumu. Alimuita rafiki yake ambaye alimpa dawa ya kutapika ile sumu. Babu aliendelea kudhoofika na tarehe 17 Septemba 1967 kama saa 11 jioni babu alifariki hospitali ya serikali Iringa, kesho yake akazikwa jirani na kaburi la baba yake katika kijiji cha Mgama…….ITAENDELEA

Categories: Iringa

1 reply

  1. Nmeipenda kiukweli hadithi nzuri japo inasikitisha lakini Ina mafunzo ndani yake hongera kuwa na babu aliyekuwa bora

    Like

Leave a reply to Anonymous Cancel reply